Papa Francisko:Wito wa kuwasiliana ni mada kuu kati ya watu na dunia ya utandawazi
Na Angella.Rwezaula - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amekutana na washiriki wa Mkutano mkuu wa Jumuiya ya Mtakatifu Paulo, Jumamosi tarehe 18 Juni 2022 na akawakaribisha na kumshukuru Mkuu wa Shirika. Katika hotuba yake, amependelea kuzungumza bila kusoma na akawakabidhi aliyokuwa ameiandaa. Na katika hotuba aliyowakabidh Papa Francisko amebainisha jinsi ambavyo wao wameongozwa kwenye mkutano na mada: “mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. (Warumi 12:2). Walioitwa kuwa mafundi wa muungano ili kutangaza kinabii furaha ya Injili katika utamaduni wa mawasiliano ”. Katika mstari wa Waraka kwa Warumi ulioongoza siku zao za mkutano mtume Paulo anawaalika wote wasifuate mawazo ya ulimwengu, bali wajiruhusu kubadilishwa kwa kubadili njia zao za kufikiri. Paulo hasemi “geuzeni ulimwengu”, badala yake, “mgeuzwe”, yaani, watoe nafasi kwa fundisho la pekee linaloweza kuwageuza wao kwa njia ya Roho Mtakatifu na Neema ya Mungu ya kubadilisha ulimwengu unaotuzunguka.
Usemi wa kupyaisha njia ya kufikiri Baba Mtakatifu anasema ni kiini cha pendekezo la maisha ya kiroho na ya kitume ambacho Mwanzilishi wao Mwenyeheri James Alberone, alifafanua na kuratibu kwa ajili yao akianza kwa usahihi kutokana na uzoefu wa Mtakatifu Paulo. Mwenyeheri aliandika hivi: “Kila kitu kinatoka akilini. Iwapo mtu anafanya kazi nzuri ni kwa sababu aliifikiria kisha akaitamani kisha akaifanya. Kwa hivyo kila wakati, jambo la kwanza la kuangalia ni akili. Kwa maana hiyo, kwanza kabisa ni fikra inayopaswa kubadilishwa, kugeuzwa, kufananishwa na ile ya Bwana Yesu, ili kusaidia kueneza namna ya kufikiri na kuishi kwa kutegemea Injili katika jamii. Ni changamoto kubwa kwa Kanisa na kwa Wapaulini, inayojulikana na karama ya kitaasisi ya mawasiliano. Kwa hakika, haitoshi kutumia njia za mawasiliano ili kueneza ujumbe wa Kikristo na Majisterio ya Kanisa; bali ni muhimu kuunganisha ujumbe wenyewe katika utamaduni mpya unaoundwa na mawasiliano ya kisasa. Utamaduni unaozaliwa, hata kabla ya yaliyomo, kutokana na ukweli kwamba kuna njia mpya za kuwasiliana na lugha mpya, mbinu mpya na mitazamo mpya ya kisaikolojia(Rej. Redemptoris missio, 37,).
Papa Fracisko anaandika kwamba Mada kuu katika suala hilo ni ile ya mahusiano baina ya watu katika ulimwengu wa utandawazi na wenye uhusiano mkubwa. Ni mada kuu katika ngazi ya kibinadamu na kijamii, na katika ngazi ya kikanisa, kwa sababu maisha yote ya Kikristo huanza na kustawi kupitia uhusiano kati ya mtu na mtu. Na sasa, baada ya siku za mwanzo za ubunifu wa kiteknolojia, Papa amsema tunafahamu kuwa haitoshi kuishi mtandaoni au kuunganishwa, bali tunahitaji kuona ni kwa kiasi gani mawasiliano yetu, yaliyoboreshwa na mazingira ya kidigitali, yanajenga madaraja na yanachangia ujenzi wa utamaduni wa kukutana. Kwa ajili ya utume wao mahususi wa uinjilishaji katika ulimwengu wa mawasiliano, Padre Alberione alitaka wao wawe watu waliowekwa wakfu, walioitwa kushuhudia Injili kwa kujitolea bila kujibakiza katika utume. Kwa sababu hiyo, lazima watazame mtume Paulo kama kielelezo cha mwanadamu aliyevutiwa na Kristo na kusukumwa na upendo wake katika barabara za ulimwengu. Kutoka kwa mtume Paulo daima wajifunze kwa upya shauku ya Injili na roho ya kimisionari, ambayo, kwa kuzaliwa kutoka kwa moyo wake wa kichungaji" ilimsukuma kujifanya kuwa kila kitu kwa kila mtu kwa wote.
Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba na jambo moja ambalo, kwa kuzungumzia juu ya Paulo, lina hatari ya kupuuzwa, lakini ambalo kiukweli linaonekana wazi kutoka katika barua zake, ni kwamba hakutenda peke yake, kama shujaa wa pekee, lakini siku zote kwa ushirikiano na wamisionari wenzake. Kwa hiyo, kutoka kwake wao pia wajifunze kufanya kazi pamoja na wengine, kufanya kazi kwenye mtandao, kuwa mafundi wa umoja, wakitumia njia bora zaidi na za kisasa za mawasiliano ili kufikia watu na Habari Njema na wanaishi wapi na jinsi gani wanavyoishi. Baba Mtakatifu Francisko amewashauri wajaribu kusitawisha mtindo huuo wa muungano kwanza kati yao, katika jumuiya zao na katika Shirika, wakitekeleza ka vitendo sinodi ambayo katika Kanisa lote tumejiwekea kuimarisha na zaidi ya yote kufanya mazoezi katika kila ngazi.
[ Photo Embed: PAPA NA WASHIRIKI WA MKUTANO MKUU WA SHIRIKA LA MT PAULO]
Akizungumza juu yao, Papa Francisko amewaomba waweka karama yao katika huduma ya mchakato huo, yaani, kulisaidia Kanisa kutembea pamoja kwa kutumia vyema njia za mawasiliano. Ni huduma ambayo imewaona wakiwa makini kila wakati, lakini ambayo katika awamu hii inawaomba kufikiriwa na kujifunza zaidi kwa njia ya mada. Kwa kifupi Papa amebainisha kwamba maneno mawili mada ni sinodi na mawasiliano. Lakini hata hivyo Papa mebainisha kwamba hapendelei wajisikie wakizingatiwa tu kwa kiwango hicho yaani ya utaalam, uwezo wao maalum. Hapana, wao wanaitwa kuishi mungani kwa kawaida katika udugu, katika mahusiano na jumuiya za kijimbo ambamo wanaishi, na bila shaka na Familia kubwa na tofauti ya Paulini. Upeo wao daima na lazima uwe ule wa Mtakatifu Paulo, yaani, wanadamu wote wa wakati wetu, ambao Injili ya Kristo imekusudiwa, hasa wale wanaoonekana kuwa mbali, wasio jali na hata maadui.
Mara nyingi, kwa uchunguzi wa karibu, watu hawa huficha ndani yao hamu ya Mungu, kiu ya upendo na ukweli. Hatimaye katika hotuba hiyo aliyoikabidhi, Papa anawashukuru kwa ziara yao na zaidi ya yote kwa kujitoa kwao kwa huduma ya Kanisa na uinjilishaji. Maria, Malkia wa Mitume, pamoja na ulinzi wake wa kimama, awasindikize daima katika safari yao. Amewabariki sana wote na washirika wao. Na ameaomba wamkumbuka katika sala zao.