Tafuta

Mama Kanisa tarehe 26 Juni 2022 ameadhimisha Siku ya Mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya ushuhuda wa Injili ya huduma na mapendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Mama Kanisa tarehe 26 Juni 2022 ameadhimisha Siku ya Mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya ushuhuda wa Injili ya huduma na mapendo kwa maskini na wahitaji zaidi. 

Sadaka ya Mtakatifu Petro Ni Kwa Ajili ya Huduma ya Upendo Na Mshikamano wa Kidugu

Papa Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo anawaalika waamini kuonesha moyo wa faraja, huruma na upendo kwa waathirika wa UVIKO-19, vita, majanga asilia pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni sadaka inayosaidia kujenga udugu wa mshikamano wa upendo na watu wanaoteseka kwa ujinga, umaskini na njaa sehemu mbalimbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba wa imani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni ni siku ambayo pia, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kwa namna ya pekee, kuonesha upendo na mshikamano na Baba Mtakatifu kwa kuchangia kwa hali na mali katika huduma ya upendo inayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa maskini na wahitaji zaidi, kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa namna ya pekee katika mwaka huu wa 2022 ni waathirika wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambao umesababisha majanga makubwa katika maisha ya watu wengi. Kuna waathirika wa vita, kinzani pamoja na majanga asilia. Mchango huu ni muhimu sana kama sehemu ya ushuhuda na utambulisho wa Injili ya huruma na mapendo.

Sadaka ya Mtakatifu Petro ni kielelezo cha ushiriki wa waamini katika maisha na utume wa Papa
Sadaka ya Mtakatifu Petro ni kielelezo cha ushiriki wa waamini katika maisha na utume wa Papa

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia vultus” yaani “Uso wa Huruma” anasema, Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani. Ni sharti la wokovu na ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huruma ni njia ya inayowaunganisha Mungu na mwanadamu kwa njia ya Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. “Sadaka ya Mtakatifu Petro “L'Obolo di San Pietro” au kwa Lugha ya Kiingereza “Peter’s Pence” au “Denarius Sancti Petri” ulianzishwa na Mwenyeheri Papa Pio IX tarehe 5 Agosti 1871, ili kumjengea Khalifa wa Mtakatifu Petro nguvu ya kiuchumi. Hii ni sadaka inayotolewa na waamini wote wa Kanisa Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Lengo ni kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu; haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Sadaka hii tangu wakati huo imekuwa ni kilelezo cha mshikamano wa huduma ya upendo na Khalifa wa Mtakatifu Petro inayopata chimbuko lake katika Maandiko Mtakatifu. “Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo.” Lk 3:11. Lakini toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.” Lk 11: 41 na kwamba imani bila matendo imefuka. Yak 2:15-16. Kwa mwaka huu, Sadaka ya Mtakatifu Petro inakusanywa tarehe 26 Juni 2022.

Mshikamano wa huruma na upendo kwa maskini na wahitaji zaidi.
Mshikamano wa huruma na upendo kwa maskini na wahitaji zaidi.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliwahi kusema “Sadaka ya Mtakatifu Petro” ni kielelezo muafaka cha ushiriki mkamilifu wa waamini kwa ajili ya huduma upendo inayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni alama ya ushirika na Khalifa wa Mtakatifu kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wahitaji zaidi. Hii ni huduma muhimu sana ya Kikanisa. Mshikamano wa udugu wa kibinadamu unapata chimbuko lake katika mfano wa Msamaria Mwema. Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo kwa Mwaka 2022 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha moyo wa faraja, huruma na upendo kwa waathirika wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Vita inayoendelea huko Ukraine, majanga asilia pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni sadaka inayosaidia kujenga udugu wa mshikamano wa upendo na wale wote wanaoteseka kwa ujinga, umaskini na baa la njaa sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni sadaka inayopania kujenga, kukuza na kudumisha misingi ya: uhuru, haki na amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Sadaka ya Mt. Petro

 

27 June 2022, 15:00