Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Toba, Wongofu na Utakatifu wa Mapadre
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Utakatifu wa Mapadre ni hitaji muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa sababu wao wamepewa dhamana na jukumu la: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifu watu wa Mungu. Ukweli huu wa imani katika maisha na utume wa Mama Kanisa, unagusa hata maisha ya waamini walei ambao usiku na mchana wanatafuta kuona na kushuhudia utakatifu wao, kwa kutambua au kwa kutokujua kutoka kwa mtu wa Mungu. Waamini wanamwona Padre kuwa ni mshauri wa maisha ya kiroho, mpatanishi na mjenziwa haki wa amani; rafiki mwaminifu na mnyoofu; mtu mwenye hekima na busara. Ni kiongozi makini na salama ambaye watu wa Mungu wanaweza kujiaminisha kwake nyakati ngumu na katika majaribu ya maisha, ili kuonja na hatimaye, kupata faraja na usalama wao. Mwongozo wa Utume na Maisha ya Mapadre ni rejea muhimu sana katika maadhimisho kama haya. Mapadre watambue kwamba, Upadre ni wito na zawadi inayokita mizizi yake katika Sakramenti na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Mkazo unawekwa zaidi katika ushiriki wa Mapadre katika maisha ya watu wa Mungu.
Na kwamba, utambulisho wa Mapadre unafumbatwa kwa namna ya pekee katika: Sala, upendo katika shughuli za kichungaji; Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha bila kusahau katekesi, Sakramenti za Kanisa; Maisha ya kijumuiya ambayo yana changamoto zake. Useja, utii na ufukara ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utambulisho wa Mapadre, bila kusahau Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Mama Kanisa anakazia umuhimu wa majiundo endelevu yatakayogusa medani mbalimbali ya maisha na utume wa Mapadre. Yote haya unaweza kujipatia kwa kufanya rejea kwenye Mwongozo wa Utume na Maisha ya Mapadre. (Rej. CONGREGATION FOR THE CLERGY DIRECTORY ON THE MINISTRY AND LIFE OF PRIESTS.) Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari alipomchoma Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka!
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Mapadre kujichotea utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika Waraka wa Kitume wa Papa Pio XII, “Haurietis acqua” wa Mwaka 1956 kuhusu “Moyo Mtakatifu wa Yesu kiini cha huruma ya Mungu”. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya: imani, upendo, huruma, msamaha, uvumilivu, uaminifu na unyenyekevu wa Mungu, aliyejinyenyekesha na kujifanya kuwa mdogo, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake unaoleta maisha na uzima wa milele! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 22 Juni 2022 amewakumbusha waamini kwamba Ijumaa tarehe 24 Juni 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hii pia ni Siku ya Kuwaombea Mapadre: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Mwenyezi Mungu amependa kukutana na binadamu wote kwa njia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini wote kuendelea kujiaminisha kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu chemchemi ya huruma na upendo kwa kusema “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na moyo wako.” Tarehe 25 Juni 2022, Kanisa linaadhimisha pia Kumbukumbu ya Moyo Safi wa Bikira Maria. Hii ni fursa kwa waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria kwa kuendelea kutumainia maombezi yake.
Waamini wanogeshe sala zao hasa zaidi wakati wa Mwezi Juni, uliotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Waamini wamwombe Kristo Yesu ili aweze kuwafundisha kumpenda Mungu na jirani. Kwa wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya, watambue kwamba, Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kisima cha huruma na upendo wa Mungu unaopaswa kuwashwa duniani. Hapa ni mahali ambapo, waamini wanaweza kujichotea imani, matumaini na mapendo thabiti. Baba Mtakatifu anawashauri waamini wasione woga kumtolea Kristo Yesu shida na mahangaiko, wasiwasi, hofu na udhaifu wa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni Sherehe inayopendwa sana na watu wa Mungu. Ni wakati wa kuvumbua amana na utajiri unaohifadhiwa kwenye “sakafu” ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili hatimaye, kujifunza kumpenda Mungu na jirani na hivyo, kujenga utamaduni wa upendo. Waamini wamwombe Kristo Yesu neema na baraka ili waweze kutakatifuza nyoyo zao na hivyo kuondoa makando kando yanayokwamisha ustawi na maendeleo yao ya kiroho. Wamwombe Kristo Yesu kuondokana na kiburi na hali ya kukosa utaratibu katika maisha. Na badala yake, ajaze nyoyo zao upendo na hofu ya Mungu, ili hatimaye, nyoyo za waamini ziweze kupata amani, faraja na utulivu wa ndani.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 26 Juni 2019 aliwakumbusha waamini kwamba, Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni ukumbusho kwamba, Kristo Yesu anaishi “Christus vivit”. Kristo Yesu anawapenda waja wake, anaendelea kujisadaka kama chemchemi ya huruma, upendo, msamaha na wokovu wa walimwengu. Baba Mtakatifu anasema, huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia ili kuweza kupata: hifadhi, amani na utulivu wa ndani kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Waamini wajitahidi kwenda kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa Sakramenti ya Upatanisho. Kamwe waamini wasisite kujiaminisha chini ya Moyo Mtakatifu wa Yesu katika hija ya maisha yao hapa duniani! Waamini wavutwe na hisia za upendo wa kweli unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Watumie siku hii kwa ajili ya kuombea toba, wongofu na utakatifu wa Mapadre na wanapofanya hivi, wamkumbuke hata yeye katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili maisha na utume wao wote, upate chapa ya upendo wa Mungu kwa wanadamu wote!
Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 alitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu. Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mapadre wasikubali kumezwa na malimwengu, bali: utii, useja na ufukara, viwe ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre kuendelea kukesha kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Upatanisho mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha wongofu wa shughuli za kichungaji. Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu ni dalili kwamba, wito na utume huu mtakatifu umehifadhiwa katika chombo cha udongo. Mapadre wanaopitia vipindi vigumu vya maisha na utume wao, wanapaswa kusindikizwa kwa huruma na upole; wasikilizwe kwa makini; wasaidiwe kufikia mang’amuzi na ukomavu katika maisha. Huu ni wajibu wa kwanza kwa Maaskofu mahalia, lakini hata kwa Jumuiya nzima ya waamini pamoja na familia zao, ambazo mara nyingi zinabeba Msalaba mzito! Wakleri ni watu ambao wanapaswa pia kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa katika maisha na utume wao! Kamwe Mapadre wasidhaniwe kuwa ni mashine za kutolea huduma ya mambo matakatifu! Mapadre wapendwe katika ukweli na uwazi; wasaidiwe kupata mahitaji yao msingi. Waamini walei, wakishirikiana, wakisaidiana na kushauriana na Mapadre wao, maisha na utume wa Kanisa vitasonga mbele kwa ari kubwa zaidi!
Pale Mapadre wanapoonekana kuchoka na kuanza kukata tamaa, waamini wawe mstari wa mbele kuwaenzi kwa sala na sadaka zao; kwa kutambua na kuthamini huduma zao pamoja na ushauri wa udugu wa kibinadamu. Siku ya Kuombea Utakatifu wa Mapadre, iwe ni fursa ya kuwasindikiza Mapadre katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Katika majitoleo kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mama Kanisa anawaalika watoto wake katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: kushiriki Misa Takatifu, kupokea Ekaristi Takatifu na kutenda matendo ya huruma, kusali sala iliyoelekezwa na Mama Kanisa kama njia ya kulipia madhulumu dhidi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu yafanywayo na watu mbalimbali na hasa kwa kukosa heshima kwa Sakramenti Kuu, yaani Ekaristi Takatifu. Matunda ya majitoleo hayo ni neema zibubujikazo kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu! Ahadi zinazobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu: Nitawajalia neema zote watakazozihitaji katika hali yao ya maisha. Nitawajalia amani katika familia zao. Nitawafariji katika magumu yao yote. Nitakuwa kimbilio lao salama wakati wa maisha yao, na zaidi sana katika saa yao ya kufa. Nitawapa baraka tele katika shughuli zao zote. Wakosefu watapata katika Moyo wangu chanzo na bahari ya huruma isiyo na mwisho. Waamini walio vuguvugu watakuwa na bidii. Waamini wenye bidii watakwea kwa upesi katika ngazi za juu za ukamilifu. “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na moyo wako.”