Kanisa ni Sakramenti ya wokovu, ni chombo na shuhuda wa upatanisho, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu dhamana ambayo limepewa na Kristo Yesu! Kanisa ni Sakramenti ya wokovu, ni chombo na shuhuda wa upatanisho, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu dhamana ambayo limepewa na Kristo Yesu!  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Dhima ya Upatanisho

Kanisa linapaswa kuwa ni nyumba ya familia ya watoto wote wa Mungu, mahali wanapoweza kushiriki Karamu ya uzima wa milele, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Fumbo la Msalaba, wote wamepatanishwa na Mungu. Upatanisho ni sehemu ya vinasaba vya maisha, utume na utambulisho wa Kanisa na kwamba, Kanisa ni Fumbo la Mwili hai wa upatanisho; sala, upendo na huduma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa ni Sakramenti ya wokovu, ni chombo na shuhuda wa upatanisho, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu dhamana ambayo limepewa na Kristo Yesu! Kanisa linawaalika na kuwahimiza waamini kujipatanisha na Mungu, jirani zao pamoja na mazingira, nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa linapaswa kuwa ni nyumba ya familia ya watoto wote wa Mungu bila ubaguzi wala maamuzi mbele, mahali wanapoweza kushiriki Karamu ya uzima wa milele, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Fumbo la Msalaba, wote wamepatanishwa na Mungu. Upatanisho ni sehemu ya vinasaba vya maisha, utume na utambulisho wa Kanisa na kwamba, Kanisa ni Fumbo la Mwili hai wa upatanisho; mahali ambapo, watoto wa Mungu wanaweza kukutana tena kwa upendo na huduma; kusali na kusaidiana kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu ameamua kutengeneza makao yake kati pamoja na binadamu! Kwa hakika Mwenyezi Mungu anataka kukaa katika Kanisa ambalo ni nyumba ya upatanisho! Kwa muhtasari huu ndio ujumbe uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na watu asilia wa Canada pamoja na wajumbe wa Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo kuu la Edmonton, Canada.

Kanisa ni chombo cha upatanisho, sala, upendo na huduma
Kanisa ni chombo cha upatanisho, sala, upendo na huduma

Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa ni nyumba ya familia ya watoto wa Mungu, mahali ambapo ukarimu unapewa msukumo wa pekee, kwa kuthamini na kuenzi tunu msingi za maisha ya watu asilia, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho. Kanisa ni mahali ambapo, waamini wanashirikisha historia za maisha yao na kumwilisha imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Kanisa ni Takatifu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu, lakini watoto wake wanakabiliwa na dhambi pamoja na udhaifu wa kibinadamu. Ni katika muktadha wa dhambi na udhaifu wa kibinadamu, Baba Mtakatifu ameamua kufanya hija ya kitume nchini Canada, ili kunogesha mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa. Ni fursa ya kuombea msamaha kutokana na makosa yaliyojitokeza miongoni mwa Mihimili ya uinjilishaji kwa kushibana na wakoloni na matokeo yake, mfumo wa elimu ukawa ni chanzo cha ukatili, dhuluma na nyanyaso.

Elimu haina budi kusimikwa katika misingi ya kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja. Isaidie kukuza na kudumisha karama na mapaji ya watu, ili yaweze kufikia kilele chake, kwa kumsaidia mwanadamu kutambua maana ya maisha yake na hivyo kujikita katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Upatanisho ni chemchemi ya amani na utulivu wa ndani. “Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya Msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo Msalaba.” Efe 2: 14-16. Kwa hakika Msalaba ni chemchemi ya maisha, huruma na upendo wa Kristo Yesu. Msalaba wa Kristo Yesu, uwawezeshe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira, nyumba ya wote. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu anapaswa kuwa ni kiini cha utamadunisho wa kweli unaosimikwa katika mchakato wa uponyaji na amani. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae, na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu ya Msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.” Kol 1: 19-20.

Msalaba wa Kristo Yesu ni chombo cha upatanisho
Msalaba wa Kristo Yesu ni chombo cha upatanisho

Baba Mtakatifu amewataka watu asilia wa Canada kumwona Kristo Yesu akiendelea kusulubiwa miongoni mwa watoto wa shule za makazi ya watu asilia, changamoto kwa wao sasa ni kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao; kwa kumwachia Kristo Yesu aguse na kuponya madonda ya dhuluma, ubaguzi na nyanyaso na kwamba, amani ya kweli imelala juu ya Altare ya Kristo. Msalaba wa Kristo Yesu ni mti wa maisha dhidi ya kifo; ni chemchemi ya furaha ya kweli dhidi ya huzuni, ni chimbuko la matumaini mapya badala ya kukata tamaa na ni mahali pa ujenzi wa ushirika mkamilifu na udugu wa kibinadamu badala ya kuelemewa na chuki, uchoyo na ubinafsi. Upatanisho ni zawadi kutoka kwa Kristo Mfufuka. Kanisa ni Fumbo hai la Mwili wa Upatanisho, unaowaunganisha watu katika upendo; unaowaokoa watu na kuwaweka huru kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kinyume kabisa cha wongofu wa shuruti. Kristo Yesu ameupatanisha ulimwengu wote kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Kishawishi kikubwa kilikuwa ni kwa watu kumtaka Kristo Yesu ashuke kutoka Msalabani, lakini akaendelea kutangaza Habari Njema kwa uhuru na ukweli.

Kanisa liwe ni chombo cha kuwakutanisha watu wa Mungu, ili kushirikisha historia, tamaduni, mila na desturi njema za watu. Ni mahali pa kushirikishana “tone” la upendo linalomwilishwa katika huduma, ili kweli hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: toba, wongofu wa ndani, amani na upatanisho katika ngazi mbalimbali za maisha ya watu. Kanisa liwe ni mahali pa waamini kukutanika kwa ajili ya sala, kusaidiana na kushirikishana mang’amuzi mbalimbali ya maisha, tayari kufungua malango ya upatanisho ambayo kimsingi ni kazi ya Mwenyezi Mungu. Waisraeli katika safari ya kutoka utumwani Misri kuelekea Nchi ya ahadi, walikuwa wanakutana na Mungu kwenye hema takatifu. Na kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu ameamua kutengeneza makazi yake kati pamoja na binadamu kwa njia ya Kristo Yesu. Kumbe, Kanisa linapaswa kuwa ni nyumba ya upatanisho.

Upatanisho, haki, amani, upendo na mshikamano ni muhimu sana
Upatanisho, haki, amani, upendo na mshikamano ni muhimu sana

Kwa upande wake Padre Susai Jesu, OMI, Paroko wa Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, amemwelezea Baba Mtakatifu, historia ya Parokia hii iliyoanzishwa kunako mwaka 1913 na mwaka 1991 ikatengwa rasmi kwa ajili ya huduma kwa watu asilia wa Canada na wageni waliokuwa wanahamia katika Jimbo kuu la Edmonton. Kwa kiasi kikubwa, Parokia hii iliwahudumia maskini na wale watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni Parokia maskini, lakini kutokana na ukarimu na upendo wa watu wa Mungu, Parokia inaweza kutoa huduma kwa watu wengi zaidi. Hapa ni mahali ambapo waamini wanapata faraja, upatanisho, ushauri nasaha na uponyaji wa ndani. Waamini wanampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watoto sehemu mbalimbali za dunia. Parokia pia inaunga mkono juhudi zake za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Papa Upatanisho

 

26 July 2022, 16:24