Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Tamko La Baraza la Maaskofu Katoliki Canada
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya Kitume ya 37 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa nchini Canada kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 30 Julai 2022 imenogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo hasa lilikuwa ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Baba Mtakatifu, kwa niaba ya Mama Kanisa ameomba tena msamaha unaopania kuleta mwanga angavu wa hija ya: toba, wongofu wa ndani, matumaini na upatanisho wa Kitaifa, unaofumbatwa katika misingi ya ukweli na uwazi. Nia ni kuleta utakaso wa kumbukumbu na hatimaye, kuendelea kujikita katika uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 31 Julai 2022 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewashukuru watu wote wa Mungu waliojisadaka kwa ajili ya hija yake ya Kitume nchini Canada. Kwa namna ya pekee, anawashukuru viongozi wa Serikali, watu asilia wa Canada, Maaskofu na watu wote wa Mungu katika ujumla wao. Anawashukuru wote waliomsindikiza kwa sala na sadaka yao wakati wote wa hija yake ya Kitume nchini Canada.
Kama sehemu ya desturi na utamaduni wake, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 30 Julai 2022, baada ya kuwasili mjini Roma, alikwenda moja kwa moja kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma, ili kumshukuru Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya kimama wakati wote wa hija yake ya Kitume nchini Canada. Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kutoka mjini Iqaluit, Canada, amepitia katika anga la: Denmark, Ireland, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Uswiss na hatimaye Italia. Wakati akiondoka nchini Canada, Baba Mtakatifu amemtumia salam za shukrani Mheshimiwa Mary Simon, Gavana Mkuu wa Canada. Baba Mtakatifu anamshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka alizomkiria wakati wa hija yake nchini Canada. Anawashukuru watu wa Mungu nchini Canada kwa wema na ukarimu wao na kwamba, anawaahidia sala na sadaka yake, katika mchakato mzima wa upatanisho na amani. Kwa viongozi na wakuu wengine wa nchi alimopia, amewatakia: neema na baraka; amani, furaha na ustawi, maendeleo na mafao ya watu wao, huku wakiendelea kukoleza umoja wa Kitaifa. Baba Mtakatifu katika salam na matashi mema aliyomtumia Rais Sergio Mattarella wa Italia, amemwelezea kuridhishwa kwake kwa amana na utajiri ambao amejichotea nchini Canada kwa kukutana na kuzungumza na watu asilia wa Canada katika uhalisia wa maisha na mazingira yao. Anawatakia watu wa Mungu nchini Italia, amani, utulivu, ustawi na maendeleo na kwamba, anapenda kuwahakikishia sala na sadaka yake.
Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Canada "The Canadian Conference of Catholic Bishops (CCCB)” lililoanzishwa kunako mwaka 1943 na kutambuliwa rasmi na Vatican mwaka 1948, lina mpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kufanikisha hija yake ya kitume nchini Canada, hatua muhimu sana katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Wanampongeza kwa ujasiri na moyo mkuu aliouonesha katika hija hii ya kitume, kwa kuthubutu kuomba msamaha kwa dhambi na udhaifu uliotendwa na mihimili ya uinjilishaji katika historia na maisha ya watu asilia wa Canada. Kwa hakika, Baba Mtakatifu amesikitishwa na kuhuzunishwa na madhara makubwa yaliyotendwa na mifumo mbalimbali ya ukoloni, yaani ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo na kwa sasa ukoloni wa kiitikadi katika maisha ya watu wa Mungu ndani na nje ya Canada. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, linakiri madhara yaliyojitokeza kwenye shule za makazi ya watu asilia wa Canada, dhuluma na nyanyaso za kijinsia, ambazo kimsingi zimeacha makovu makubwa katika maisha ya watu asilia nchini Canada. Maaskofu Katoliki Canada tangu mkutano wao mkuu wa mwaka 2021 katika mazungumzo na majadiliano yao na watu asilia wa Canada, wamekazia kuhusu: ukweli na uwazi mintarafu shule za makazi kwa watu asilia wa Canada, utengenezaji wa makumbusho yatakayohifadhiwa kwenye Jumba la Makumbusho la Vatican; kufafanua ukweli wa kile kinachoitwa “Mafundisho Kuhusu Ugunduzi wa Amerika ya Kusini” na mifumo mbalimbali ya ukoloni kwani ni kati ya mambo yaliyochangia kufifisha utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada, kiasi hata cha kung’olewa kutoka katika ardhi yao asilia.
Itakumbukwa kwamba, Canada kama taifa lilizaliwa kunako mwaka 1867. “Mafundisho ya Ugunduzi” pia ni dhana ya sheria ya kimataifa ya umma ambayo ilitangazwa na Kanisa Katoliki na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ili kuhalalisha ukoloni na uinjilishaji nje ya Bara la Ulaya. Sheria hii iliwaruhusu watawala kukwapua ardhi kutoka kwa watu asilia. Kumbe, Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linapania kutembea pamoja na watu asilia wa Canada, kuwajengea uwezo wa kufikia nyaraka za kihistoria, kuendelea kuwekeza katika malezi na makuzi ya Mihimili ya Uinjilishaji. Baraza limetoa kiasi cha dola milioni 30 kwa ajili ya Mfuko wa Upatanisho na Watu Asilia wa Canada. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawashukuru na kuwapongeza wadau wote waliosaidia kufanikisha azma hii na kwamba, linatambua changamoto pevu zilizoko mbele yake. Safari ya toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa ni mchako unaowahusu watu wote wa Mungu nchini Canada. Maaskofu wanawashukuru na kuwapongeza wahanga kwa kuwa wakweli na wa wazi wakati walipokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada lina mshukuru Mungu kwa kuwa ni sehemu ya toba, wongofu wa ndani, uponyaji na hatimaye upatanisho wa Kitaifa. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko imepyaisha matumaini kwa watu asilia wa Canada kwa ajili ya leo na kesho iliyo bora zaidi.