Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Canada pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kutembelea nchi yao  kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022. Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Canada pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kutembelea nchi yao kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Canada: Toba, Wongofu wa Ndani na Upatanisho

Hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Haya ni matembezi yanayohitaji kuwa na mwelekeo na lengo maalum yaani upatanisho unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu na haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Canada pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kutembelea nchi yao kuanzia Jumapili tarehe 24 Julai hadi Jumamosi tarehe 30 Julai 2022 atakaporejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake. Akiwa nchini Canada, Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na watu asilia wa Canada, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu; ataadhimisha Liturujia ya Neno la Mungu, dira na mwongozo wa maisha ya waamini. Anatarajia kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa watu asilia nchini Canada pamoja na wanadiplomasia wanao ziwakilisha nchi na mashirika ya Kimataifa nchini Canada. Baba Mtakatifu atakutana pia na kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi, katika maadhimisho ya Masifu ya jioni, Alhamisi tarehe 28 Julai 2022. Akiwa mjini Quèbec atakutana na “kuchonga” kwa faragha na Wayesuit wanaoishi na kufanya utume wao nchini Canada hasa wakati huu wanapoadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Baba Mtakatifu kabla ya kurejea mjini Vatican, atakutana na kuzungumza na wawakilishi wa watu asilia nchini Canada. Baadaye atazungumza na wanafunzi wa zamani, vijana na kuhitimisha hija ya kitume nchini Canada kwa kuzungumza na wazee wenzake. Anatarajiwa kuwasili mjini Roma, Jumamosi tarehe 30 Julai 2022.

Hija ya Papa Francisko Canada: Toba, wongofu na upatanisho
Hija ya Papa Francisko Canada: Toba, wongofu na upatanisho

Hija hii ya kitume, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Haya ni matembezi yanayohitaji kuwa na mwelekeo na lengo maalum yaani upatanisho unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 17 Julai 2022, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliwaambia waamini kwamba, tarehe 24 Julai 2022 anatarajia kufanya hija ya kitume nchini Canada, ili kukutana na kuzungumza na watu asilia nchini Canada na hivyo kuchangia katika safari ya uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu anatambua mchango uliotolewa na Wakristo wengi katika mchakato wa utamadunisho, lakini pia kuna taasisi za kidini ambazo zilichangia sera ambazo zimekwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Katika jitihada za kutembea pamoja, Baba Mtakatifu amekwisha kukutana na kuzungumza na wawakilishi wa watu asilia wa Canada, ili kuonesha machungu yaliyogandamana na sakafu ya moyo wake na mshikamano kwa matatizo waliyokumbana nayo. Kumbe, hija hii ya kitume nchini Canada ni mchakato wa kutembea pamoja kwa ajili ya uponyaji na upatanisho wa Kitaifa ambao tayari umekwisha kuanza.

Baba Mtakatifu Francisko, tangu sasa anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa wale wote wanaochakarika usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, hija hii ya kitume inafanikiwa. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumsindikiza kwa sala na sadaka zao katika hija hii ya kitume. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 28 Machi 2022 alikutana na kuzungumza na ujumbe wa watu 10 kutoka Baraza la Watu Asilia wa Canada “Mètis National Council, MNC” Kikundi cha “Inuit” waliokuwa wamesindikizwa na baadhi ya Maaskofu Katoliki kutoka nchini Canada. Baba Mtakatifu alitenga muda maalum wa kuwasikiliza wahanga wa ubaguzi wa rangi ili kutambua ukweli na hivyo kuanza mchakato wa ujenzi wa msingi wa haki, uponyaji na upatanisho wa kitaifa. Si rahisi sana kuweza kufuta mateso, machungu na changamoto walizokutana nazo katika historia na maisha yao. Jumuiya ya Watu Asilia nchini Canada inasema kwamba, ina uthibitisho wa makaburi ya wanafunzi 215 waliozikwa kwenye shule ya “British Columbia School”, moja ya shule zilizokuwa zimetengwa ili kutoa nafasi kwa wazawa kuweza kushiriki katika maisha ya jamii nzima.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada limekwisha anzisha mchakato wa upatanisho
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada limekwisha anzisha mchakato wa upatanisho

Makaburi haya yamegunduliwa kwenye eneo la “Kamloops Indian Residential School” iliyofanya kazi zake kuanzia mwaka 1890 hadi mwaka 1970. Hawa ni wanafunzi waliopotea katika mazingira ya kutatanisha na wazazi na walezi wao hawakupatiwa maelezo ya kutosha. Shule kama hizi zilikuwa zinaongozwa na kuendeshwa na Makanisa nchini Canada. Tume ya Haki na Upatanisho wa Kitaifa nchini Canada inasema kuna zaidi ya wanafunzi 4, 100 waliofariki dunia katika mazingira ya kutatanisha. “Kamloops Indian Residential School” ni kati ya shule kubwa nchini Canada iliyokuwa inaongozwa na Kanisa Katoliki, ikiwa na wanafunzi zaidi ya 500 kabla ya Serikali kuanza kuingoza kunako mwaka 1969. Shule hizi kwa ajili ya wazawa nchini Canada zilipelekea mauaji ya kimbari. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana Wetu Yesu Kristo, “Corpus Domini”, 6 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alisema kwamba, alikuwa anafuatilia kwa uchungu mkubwa habari zilizokuwa zinamfikia kutoka Nchini Canada. Hii ni baada ya kugunduliwa kwa masalia ya wanafunzi 215 kutoka katika shule ya “Kamloops Indian Residential School” waliofariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.

Baba Mtakatifu alipenda kuchukua fursa hii, kujiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada na watu wa Mungu nchini Canada katika ujumla wao, kuonesha uwepo wake wa karibu kutokana na habari hizi zinazohuzunisha na kutia simanzi moyoni. Baba Mtakatifu aliwahamasisha viongozi wa Serikali na Kidini nchini Canada kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili hatimaye, ukweli uweze kufahamika, na huo uwe ni mwanzo wa mchakato wa upatanisho na uponyaji wa kitaifa. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuondokana na tabia ya ukoloni na hata ukoloni wa kiitikadi, kwa kutambua na kuthamini: utu, heshima na haki msingi za binadamu; tunu na amana za kitamaduni kwa watu wote wa Mungu nchini Canada. Baba Mtakatifu aliziweka nyoyo za marehemu watoto hao 215 chini ya huruma ya Mungu. Anaendelea kuiombea Jumuiya ya Watu Asilia nchini Canada ili iweze kupokea changamoto hii kwa moyo wa utulivu. Baraza la Watu Asilia wa Canada “Mètis National Council, MNC” lina mshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kutenga muda wake ili kusikiliza kilio chao cha ndani, ili kuanza hija ya ukweli, haki, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, dhamana inayopaswa pia kutekelezwa kwa makini katika ngazi ya mtu binafsi.

Papa Canada
19 July 2022, 15:14