Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Achonga na Kusali na Wanahabari: Upatanisho
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 24 Julai 2022 ameanza hija ya 37 ya Kitume nchini Canada itakayohitimishwa hapo Jumamosi tarehe 30 Julai 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo kuu la hija hii ni kusaidia kunogesha mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, kwa kugusa madonda ya ukosefu wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, mambo ambayo walitendewa watu asilia wa Canada katika maisha na historia yao. Baba Mtakatifu, kwa niaba ya Mama Kanisa anataka kuomba tena msamaha unaopania kuwa ni mwanga angavu wa hija ya matumaini na upatanisho wa Kitaifa, unaofumbatwa katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kuleta utakaso wa kumbukumbu na hatimaye, kuendelea kujikita katika uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu. Msafara wa Baba Mtakatifu nchini Canada umesheheni waandishi wa habari 80 kutoka katika Mataifa 10, ili kushuhudia na hatimaye, kuwajuza watu wa Mungu, yale yanayoendelea kujiri katika hija hii ya toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa.
Baba Mtakatifu amewasalimia waandishi wote mmoja mmoja. Jambo la msingi ni kukumbuka kwamba, hii ni hija ya toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa. Hii ndiyo dira na mwongozo wa hija hii 37 Kimataifa. Ametumia fursa hii, kusali pamoja nao Sala ya Malaika wa Bwana, akitilia mkazo umuhimu wa Mababu kushikamana na kushirikiana na wajukuu wao, ili waweze kuzamisha mizizi ya utu, heshima yao, tayari kuzaa matunda ya wongofu na utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha kwamba, hata kwa mapadre na watawa wazee ni warithishaji wa tunu msingi za maisha kuwekwa wakfu kwa mapadre na watawa vijana. Majandokasisi, wanavosi, wapostulanti na watakaji, wanapaswa kuchota hekima na busara kutoka kwa mapadre na watawa wazee. Wote hawa wamekumbukwa na kuombewa na wadau watasnia ya mawasiliano ambao wako kwenye msafara wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada. Wazee wanayo kumbu kumbu hai ya historia na mapokeo yao!
Baba Mtakatifu akiwa njiani kuelekea Edmonton, Canada amepitia katika anga la Italia, Uswiss, Ufaransa, Uingereza, Ireland, Denmark na hatimaye, akaingia nchini Canada. Baba Mtakatifu katika salam na matashi mema aliyomtumia Rais Sergio Mattarella wa Italia, amemshirikisha kwamba, hii ni hija inayomwezesha kukutana na kuzungumza na watu asilia wa Canada. Kumbe, anamwomba, aweze kumsindikiza kwa sala katika hija hii ya kitume inayobeba uzito wa hali ya juu katika maisha na utume wake. Amemwomba, umfikishie salam na matashi mema, kwa watu wa Mungu nchini Italia. Kwa ujumla Baba Mtakatifu anawatakia watu wote heri na baraka; nguvu na amani, utulivu na furaha tele na kwamba, anapenda kuwahakikishia watu wote wa Mungu katika nchi zao sala zake. Itakumbukwa kwamba, hii ni hija ya 37 ya Kimataifa inayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye hadi wakati huu, amekwisha kutembelea nchi 56 duniani. Canada imekwisha kutembelewa mara tatu na Mtakatifu Yohane Paulo II na hii ni safari ya nne, inayompeleka Canada kama hujaji wa toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho wa Kitaifa.