Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Watakatifu Joakim na Anna: Wazazi wa Bikira Maria
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai. Hii ndiyo familia ambamo Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa amechota fadhila mbalimbali zilizomwezesha kupata upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu, kiasi cha kukingiwa dhambi ya asili na hatimaye, kupalizwa mbinguni mwili na roho, kama tunda la kwanza la kazi ya ukombozi. Kumbe, Ibada na heshima kwa watakatifu Joakim na Anna ni mwendelezo wa Ibada kwa Bikira Maria na hatimaye, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Mama Kanisa daima anapenda kuwambusha watu watakatifu na wateule wa Mungu kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.
Wazazi wake Bikira Maria, wanaonesha umuhimu wa familia kama shule ya upendo, imani na utakatifu wa maisha. Kumbukumbu hii ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwani ni fursa ya kuwashukuru na kuwabariki wazee kutokana na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Maadhimisho ya kumbukumbu hii kwa mwaka 2022 yanakwenda sanjari na Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022. Hija hii inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa ni nyumba ya familia ya watoto wa Mungu, mahali ambapo ukarimu unapewa msukumo wa pekee, kwa kuthamini na kuenzi tunu msingi za maisha ya watu asilia, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho. Kanisa ni mahali ambapo, waamini wanashirikisha historia za maisha yao na kumwilisha imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, 26 Julai 2022, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Jumuiya ya Madola “Commonwealth Stadium”, huko Edmonton, Canada na kuhudhuriwa na umati wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za Canada. Katika muktadha wa hija yake ya kitume nchini Canada, Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu mawili yanayopaswa kuzingatiwa. Waamini watambue kwamba, wao ni watoto wa historia inayopaswa kulindwa na kudumishwa, hatimaye, kuirithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Pili watambue kwamba, wao ni wadau muhimu sana katika kuandika historia ya maisha na utume wao ambayo kimsingi bado haijaandikwa, kwani wao ni chemchemi ya maisha, tayari kumkaribisha Kristo Yesu, ili kutangaza na kushuhudia uwepo wake angavu kati pamoja nao! Watakatifu Joakim na Anna wawe ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa ujenzi wa tunu inayochipusha maisha. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amesema kwamba, Kristo Yesu katika maisha yake, alijifunza ukaribu na ujirani mwema; upendo na hekima na kwamba, watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo watambue kwamba, wao ni watoto wa historia inayopaswa kulindwa na kudumishwa; kwa kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii, si katika mazoea, uongozi, akili au katika kipaji cha ubunifu, bali ni mahusiano yanayofumbatwa katika uadilifu na uaminifu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu.
Hii ni amana na hazina ambayo wazazi na walezi wanapaswa kuwarithisha watoto wao, ili hatimaye, waweze kufanya maamuzi magumu katika maisha. Wazazi na walezi wametekeleza dhamana na wajibu wao kiasi kwamba, leo hii, watu wengi wamejifunza: Utu wema, upendo na busara; mambo ambayo yamekita mizizi yake katika maisha ya mwanadamu, kiasi cha kuzigeuza familia kuwa ni nyumba ya imani. Kimsingi imani inapaswa kurithishwa kutoka nyumbani, ili watoto waweze kutiwa shime kujifunza kupenda, kulinda na kujenga ujirani mwema. Wazazi na walezi waliwakirimia watoto wao, utu, upendo pasi na shuruti, kama ilivyokuwa kwa Watakatifu Joakim na Anna walioonesha upendo wa pekee kwa Kristo Yesu. Wakampenda na kumsindikiza katika maisha na utume wake wa maisha ya hadhara; wakaheshimu na kuthamini maamuzi na uhuru wake. Changamoto na mwaliko kwa waamini ni kulinda na kudumisha historia, kwa kuendeleza kumbukumbu hai, sanjari na kuwatunza wale ambao wamekabidhiwa kwao na Mwenyezi Mungu. Waamini wajifunze kupenda na kudumisha upendo huu katika mazingira ya kifamilia. Baba Mtakatifu Francisko anawauliza waamini ikiwa kama wako tayari kurithisha tunu msingi za maisha ya kijamii walizopokea kutoka kwa wazazi wao? Kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kutunza kumbukumbu hai zinazobubujika kutoka katika Tafakari ya Neno la Mungu na Ibada ya Rozari Takatifu? Katika shida na mahangaiko mbalimbali waamini wajifunze kusimika maisha yao katika mizizi ya tamaduni, desturi na mila njema walizorithishwa. Wajenge moyo wa sala na ibada, ili hatimaye, mti wa familia uweze kukua na kuchanua.
Pili, waamini na watu wote wenye mapenzi mema watambue kwamba, wao ni wadau muhimu sana katika kuandika historia ya maisha na utume wao ambayo kimsingi bado haijaandikwa, kwani wao ni chemchemi ya maisha, tayari kumkaribisha Kristo Yesu, ili kutangaza na kushuhudia uwepo wake angavu kati pamoja nao! Watu wa Mungu wajibidiishe kufanya tafakari ya kina itakayowasaidia kurithisha imani na tunu msingi za maisha kwa watoto wao, daima wakijitahidi kuondokana na uchoyo na ubinafsi, ili kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika: haki, amani na utulivu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Watu walinde na kutunza: tamaduni, mila na desturi njema kutoka kwa wazazi wao, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati kwa kuondokana na mazoea. Kama waamini wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha na shughuli zao kama kielelezo makini cha imani hai na tendaji. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni chemchemi ya uhai na maisha mapya; tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi, daima wakitegemea msaada wa Mungu, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Waamini wajenge utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; wajenge mahusiano na mafungamano ya kijamii miongoni mwa watu wa rika mbalimbali, ili wakiwa wameshikamana, waweze kutembea kwa pamoja, huku wakiwaumbuka wazee wao waliowatangulia katika usingizi wa amani.
Kwa upande wake, Askofu mkuu Richard William Smith wa Jimbo kuu la Edmonton, Canada, kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Canada "The Canadian Conference of Catholic Bishops (CCCB)” ametumia fursa ya Ibada hii, kumkaribisha rasmi Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada, kama kielelezo cha uwepo wake wa karibu kwa watu asilia wa Canada. Maaskofu Katoliki Canada wanampongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwa nao bega bega kwa maisha na utume wao na kwamba, uwepo wake miongoni mwao ni muhimu sana katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Bado kuna mambo mengi yanayopaswa kutekelezwa kama sehemu ya mchakato wa upatanisho wa Kitaifa. Lakini kwa upendo na uwepo wa Baba Mtakatifu, Maaskofu wanayo matumaini ya kusonga mbele, huku wakiendelea kutumainia neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kuweza kutekeleza vyema dhamana na majukumu yao. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linatambua na kuthamini uwepo wa watu asilia wa Canada, uzuri, utamaduni, hekima na busara zao. Wanaimarishwa kwa sala na maombezi ya Watakatifu Joakim na Anna sanjari na msaada kutoka kwa Baba Mtakatifu kusonga mbele katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa pamoja na watu asilia wa Canada.