Mshikamano wa Papa Francisko Na Wananchi wa Libya na Ukraine: Vita na Hali Ngumu ya Uchumi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tangu mwaka 2011baada ya mauaji ya Rais Muammar Gadaffi, Libya imejikuta ikitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kwa miaka kadhaa nchi hiyo imegawanyika katika tawala mbili hasimu na zinazosigana upande wa mashariki na magharibi, zote zikiungwa mkono na makundi tofauti ya wapiganaji na serikali za kigeni kwa maslahi yao binafsi na wala si kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Libya. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 10 Julai 2022, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliyaelekeza mawazo yake kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na wale wanaoteseka nchini Libya kutokana na machafuko ya kisiasa sanjari na hali ngumu ya uchumi inayoendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kutoa wito kwa pande zote zinazosigana, kukaa pamoja na kujadiliana kuhusu mustakabali wa familia ya Mungu nchini Libya.
Kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa, wadau wote katika mgogoro wa Libya, wajizatiti kutafuta suluhu ya pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Libya. Kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi, waweze kufikia mchakato wa upatanisho wa Kitaifa nchini Libya. Baba Mtakatifu Francisko ametumia pia fursa hii, kuonesha uwepo na ukaribu wake kwa watu wa Mungu nchini Ukraine wanaoendelea kuteseka kwa vita kati ya Urussi na Ukraine. Waathirika wakuu wa mashambulizi ya kijeshi nchini Ukraine ni raia wa kawaida, watoto, wazee na wanawake. Baba Mtakatifu anasema kwamba anaendelea kuwaombea, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaonesha njia ya kusitisha vita hii na hatimaye, amani, ustawi na maendeleo ya kweli yaweze kushika tena mkondo wake.