Papa ametangaza kuwa atateua wanawake wawili katika Baraza la Kipapa la Maaskofu
Vatican News
Katika mahojiano na Shirika la Habari la Reuter, lililofanywa na Phil Pullella, Papa Francisko alifichua kwamba anakaribia kuwateua wanawake wawili katika Baraza la Kipapa la Maaskofu, ambao kwa hiyo watahusika katika mchakato wa kuwachagua wachungaji wapya wa majimbo. Papa alijibu swali kuhusiana na uwepo wa wanawake Vatican, juu ya masharti ya katiba mpya ya kitume "Praedicate Evangelium" yaani Hubirini Injili ambayo imefanya marekebisha ya Curia Romana na ni Baraza lipi katika siku zijazo linaweza kukabidhiwa mwanaume au mwanawake mlei.
"Mimi niko wazi kwamba ziwepo fursa. Kwa sasa Mwenyekiti anakuwa na naibu mwanamke"… Kwa sasa katika Baraza la Kipapa la Maaskofu, katika mchakato wa tume ya kuwachagua maaskofu, wanawake wawili watachaguliwa kwa mara ya kwanza. "Kwa namna hiyo kidogo inafunguliwa”. Papa Francisko aliongeza kusema kwamba katika siku zijazo anaona uwezekano wa kuteuliwa kwa walei kuongoza mabaraza kama vile ya Walei, Familia na Maisha, ile ya Utamaduni na Elimu, au Maktaba, ambayo karibu ni kama Baraza”.
Papa Francisko kwa njia hiyo katika mahojiano hayo alikumbuka kwamba mwaka jana, kwa mara ya kwanza, alimteua mwanamke kushika nafasi ya pili katika Utawala wa Mji wa Vatican, Sr. Raffaella Petrini. Pamoja na hayo, Papa Fransisko alimteua Sr. Nathalie Becquart, Mfaransa wa Shirika la Wamisionari wa Xavier, kuwa Katibu Msaidizi wa Sinodi ya Maaskofu na Sr. Alessandra Smerilli, wa Shirika la Binti wa Maria wa Msaada wa Wakristo, kuwa Katibu wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Frungamani ya Binadamu. Miongoni mwa wanawake walei ambao tayari wana nyadhifa za juu katika Vatican ni pamoja na Francesca Di Giovanni, katibu msaidizi wa sekta ya kimataifa ya Kitengo cha Mahusiano na Sekretarieti ya Vatican,Wakati Baraza la Kipapa Mashirika ya Kitawa na vyama vya kutume katibu msaidizi ni Sr Carmen Ros Norten, Linda Gisoni na Gabriella Gambino wote wawili makatibu wasaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei Familia na Maisha, Profesa Emile Cuda kwa ajili ta Tume ya Kipapa kwa ajili ya Bara la Amerika ya Kusini; Barbara Jatta, mkurugenzi wa kwanza mwanamke katika Majumba ya Makumbusho Vatican, Nataša Govekar, mkurugenzi wa mwongozo wa Kitaalimungu-Kichungaji wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano na Cristiane Murray, Naibu Mkurugenzi wa Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican. Wote wawili waliteuliwa na Papa wa sasa Francisko.
Mwezi uliopita, Kadinali Kevin Joseph Farrell, Rais wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, alitania kwamba, kwa kutangazwa kwa katiba mpya kwenye Curia Romana, anaweza kuwa Kiongozi kuhani wa mwisho kuongoza Baraza hilo.