Papa Francisko: Simameni kidete kulitanda na kutangaza Injili ya familia Papa Francisko: Simameni kidete kulitanda na kutangaza Injili ya familia 

Siku ya X ya Familia Duniani: Ujumbe Kwa Familia Nchini Uruguay: Ulinzi wa Familia

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa familia nchini Uruguay, amewataka wadau wa shughuli za kichungaji, utume wa familia kuhakikisha kwamba, wanajizatiti kuzihudumia familia kwa kusimama kidete kuzilinda, kwani familia ndilo chimbuko la maisha ya mwanadamu, ambalo lina historia yake kutoka katika kazi ya uumbaji. Ushuhuda wa tunu msingi za familia ni muhimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ya ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani mjini Roma, Jumatano tarehe 22 Juni 2022, alipata nafasi ya kusikiliza kwa makini shuhuda, uzoefu na mang’amuzi ya familia zinazoishi katika hali ya wasi wasi; furaha, mateso na matumaini. Ni jambo muhimu kwa wanandoa na familia kuanza hija ya kutembea pamoja kama wanandoa, kama wanafamilia; kutembea pamoja na majirani na Kanisa katika ujumla wake kwa kujikita katika ujirani mwema, huruma, ukaribu ukarimu na mapendo, kwa kuondokana na utamaduni wa kutojali shida na mahangaiko ya wengine. Ni mwaliko wa kuchukua na kuambata Msalaba, ukweli katika upendo; tayari kusamehe na kusahau. Baba Mtakatifu anasema msamaha ni zawadi ya Mungu kwa wanandoa, inayopaswa kuadhimishwa na familia nzima, pale panapotokea “patashika nguo kuchanika”. Familia zijenge utamaduni wa ukarimu na upendo; kwa kuwathamini na kuwajali jirani. Familia zenye ukarimu na mapendo, ni chemchemi ya furaha, amani, upendo na matumaini kwa jamii.

familia yenye ukarimu ni chemchemi ya furaha, amani na upendo
familia yenye ukarimu ni chemchemi ya furaha, amani na upendo

Baba Mtakatifu anawachangamotisha wanandoa kujenga utamaduni wa udugu wa kibinadamu. Wanandoa wanapoishi kwa pamoja, wajenge pia utamaduni wa: kuheshimiana, kuthaminiana, kuaminiana na kupendana; kwani kila mmoja wao ni zawadi kwa mwenza wake wa ndoa. Furaha na upendo ndani ya familia inajengwa kwa kusikilizana, kupendana na kuthaminiana. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu, kufunga Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” amekazia kuhusu: uhuru wa ndani unaowataka wanandoa kutumikiana kwa upendo, kwani unapata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kwa wafu. Familia ni mahali pa kwanza ambako mtu anajifunza, kupenda, kusamehe na kuhudumia. Wanandoa wakuze na kudumisha mafungamano baina ya kizazi na kizazi ili kurithishana amana na tunu msingi za maisha ya ndoa, familia na imani ya Kikristo. Wanandoa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Wazazi wajitahidi kuwarithisa watoto wao: imani, maadili na utu wema, ili kukabiliana na changamoto za maisha na hatimaye, wajenge ulimwengu ulio bora zaidi.

Wazazi wawarithishe watoto wao: imani, maadili na utu wema
Wazazi wawarithishe watoto wao: imani, maadili na utu wema

Wanandoa wawe ni mashuhuda na watangazaji wa upendo, uaminifu na ukweli. Penye shida, mahangaiko na changamoto za maisha ya ndoa, wanandoa wajitahidi kupokeana, kufahamiana ili kupyaisha upendo na sadaka ya maisha, daima wakijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao ya kila siku. Upendo wa kweli anasema Baba Mtakatifu unamwilishwa katika huduma ya upendo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa familia nchini Uruguay, amewataka wadau wa shughuli za kichungaji, utume wa familia kuhakikisha kwamba, wanajizatiti kuzihudumia familia kwa kusimama kidete kuzilinda, kwani familia ndilo chimbuko la maisha ya mwanadamu, ambalo lina historia yake kutoka katika kazi ya uumbaji. Hii ndiyo dhamana ambayo Mwenyezi Mungu anawataka waja wake kuivalia njuga, ili kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ambazo ni kielelezo cha: Ukuu, uzuri, utakatifu na ushuhuda wa Injili ya familia unaobubujika kutoka katika sura na mfano wa Mungu. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Waamini wasiogope kuwekeza katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

familia Uruguay

 

01 July 2022, 16:11