Ujumbe Maalum wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume: Umuhimu wa Mikutano miku ya Mashirika. Ujumbe Maalum wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume: Umuhimu wa Mikutano miku ya Mashirika. 

Papa Francisko: Ujumbe Maalum: Mikutano Mikuu ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume

Ni fursa kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wao kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano. Lengo kuu ni watawa kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mama Kanisa anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu wanaoteseka kutokana na vita sehemu mbalimbali za dunia. Watawa wakumbuke kwamba, kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa zimechafua sana maisha na utume wa Kanisa, kumbe, kuanzia sasa hakuna mtu yeyote atayevulimiwa ikiwa kama atakamatwa kwa kujihusisha na vitendo hivi viovu vinavyonyanyasa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mikitano mikuu ya mashirika ina umuhimu wake katika maisha na utume wao
Mikitano mikuu ya mashirika ina umuhimu wake katika maisha na utume wao

Huu ni ujumbe mzito uliotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na watawa wa Mashirika matatu yaani: Shirika la Watawa wa Mama wa Mungu: Shirika la Watawa wa Mtakatifu Josephat kutoka Brazil pamoja na Shirika la Utume. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kwa niaba ya Mama Kanisa kuwashukuru watawa kwa huduma na ushuhuda wanaoutoa sehemu mbalimbali za dunia, kwa maisha yao ya kuwekwa wakfu. Viongozi wanaochaguliwa kwenye Mashirika haya watambue kwamba, dhamana yao kubwa inapaswa kuwa ni huduma kwa watawa wenzao, ili waweze kujenga na kudumisha umoja, ushiriki na utume wa Kanisa. Mashirika mengi ya kitawa na kazi za kitume, yameanza kuadhimisha mikutano mikuu baada ya kuwa imesitishwa kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambao umesababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Maadhimisho ya mkutano mkuu, ni fursa ya kukutana na kuweza kuangaliana uso kwa uso; lakini zaidi, kusali na kutafakari Neno la Mungu kwa pamoja na hatimaye, kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, tayari kutoka kifua mbele ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Mkutano mkuu wa Shirika ni kipindi maalum cha kufanya mang’amuzi ya kishirika, ili kwa msaada wa Roho Mtakatifu, waweze kufanya upembuzi yakinifu, ili kugundua ni kwa kiasi gani wamekuwa waaminifu kwa karama ya Shirika. Ni wakati muafaka wa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu, ili aweze kuwaonesha njia ya kufuata katika kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, walipokutana kwenye Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu. Hii ndiyo dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, kuimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha na utume wao katika ulimwengu mamboleo. Lengo kuu ni kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kila Shirika kadiri ya Karama yake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila karama ya Shirika inapaswa kusaidia uinjilishaji na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hii ni asili na utume wa Mama Kanisa tangu awali, kama anavyokazia Mtakatifu Paulo VI katika Waraka wake wa Kitume wa “Evangelii nuntiandi” yaani “Kutangaza Injili.”

Ushuhuda aminifu ni kivutio kikuu cha uinjilishaji duniani
Ushuhuda aminifu ni kivutio kikuu cha uinjilishaji duniani

Ni wito na furaha ya Mama Kanisa kuinjilisha, changamoto kwa watawa ni kuendelea kujifunza kutoka kwa watakatifu waanzilishi wa Mashirika yao, waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuinjilisha katika roho na huduma ya kazi na wala bila kufanya wongofu wa shuruti. Mama Kanisa anahimiza msukumo mpya wa kimisionari katika mchakato wa uinjilishaji, kwa sababu Kanisa linawahitaji wainjilishaji waliojaa Roho Mtakatifu, wanaosali na kufanya kazi. Mawazo ya kimisitiki bila ya kuwa na mwelekeo thabiti na wa kimisionari wa kutoka nje hayasaidii mchakato wa uinjilishaji na wala tasnifu, matendo ya kijamii au ya kichungaji yasiyokuwa na tasaufi au elimuroho, si mali kitu katika mchakato wa uinjilishaji. Ushuhuda wenye mvuto na mashiko; maisha ya kiroho, tafakari ya Neno la Mungu na maisha ya sala ni muhimu sana katika Uinjilishaji unaopaswa kutekeleza kwa kujikita katika maisha ya kijumuiya na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Na kwa njia hii, watu watawatambua kwamba, wamekuwa ni wanafunzi wa Kristo Yesu, ikiwa kama wataoneshana upendo wa dhati. Rej. Yn 13:35. Maisha ya kijumuiya ni changamoto pevu hasa katika ulimwengu mamboleo unaoelekea kuzama katika uchoyo na ubinafsi. Huu ni mwaliko wa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu na kiasi, kwa kuendelea kujenga udugu wa kibinadamu, katika uhuru unaowajibisha; kwa kutambua umoja na tofauti zao msingi, kila mtu akijitahidi kuwa ni chombo na shuhuda makini wa furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Watawa washiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji
Watawa washiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji

Hakuna mwamini anayezaliwa kama Muasisi wa Shirika fulani. Ni Kristo Yesu anayewavuta, katika hali ya unyenyekevu na kiasi, ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vyake vya uinjilishaji. Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kusimama katika ukweli na uwazi kwa kuondokana na tabia ya majungu inayokera na kuchafua utu, heshima na sifa njema za watawa wengine. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko katika Barua binafsi “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni Nuru ya Ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia; anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara. Kanisa litaendelea kuwa ni Mama na Mwalimu kwa kukazia toba na wongofu wa ndani, ili watoto wake waweze kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Hakuna atakayevumiliwa ndani ya Kanisa akibainika kwamba, anajihusisha na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia. Mwishoni, Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewahakikishia watu wa Mungu sehemu mbalimbal za dunia, wanaokabiliana na vita, mshikamano na ukaribu wa Kanisa katika maisha yao.

Mikutano Mikuu ya Kitawa
16 July 2022, 16:10