Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Mkutano wa Vijana Kuhusu Utalii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, UNWTO, kuanzia tarehe 27 Juni hadi tarehe 3 Julai 2022 limekua likiadhimisha Mkutano wa Kimataifa wa Vijana kuhusu Utalii huko mjini Sorrento, nchini Italia kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Utalii endelevu wa kimataifa.” Ni mkutano ambao unawashirikisha vijana wenye umri kati ya miaka 12 hadi 14 ambao wamepata fursa ya kuelezea mawazo na fikra zao kuhusu mustakabali wa sekta ya utalii duniani. Mkutano huu pia umewahusisha wanasiasa na viongozi wakuu kutoka katika sekta ya utalii duniani pamoja na watu mashuhuri kutoka katika tasnia ya burudani na michezo. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Mkutano huu, Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kuwatumia ujumbe kwa njia ya video washiriki wote, huku akiwatakia mapumziko mema wakati huu wa kipindi cha kiangazi, ambapo shule zimefungwa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, washiriki wa mkutano huu, watakuwa na kumbukumbu endelevu hasa kutokana na ushiriki wao katika kazi za kujitolea kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kuna baadhi ya vijana wanatumia kipindi cha likizo, kwa ajili ya kujitafutia ajira za muda, ili kujipatia kipato kidogo, ili hatimaye, kupunguza machungu ya hali nguvu ya uchumi na ukata wa fedha kwa familia nyingi, au kama sehemu ya kuchangia gharama za shule.
Baadhi ya vijana wanautumia muda wa likizo kwa kusali na kutafakari Neno la Mungu, ili liweze kuwa ni dira na mwongozo thabiti wa maisha. Katika hali na mazingira mbalimbali, Baba Mtakatifu anawataka vijana kuhakikisha kwamba, wanatumia kikamilifu rasilimali muda kwa kuwajibika zaidi. Na kwa njia hii, watakuwa wanajiandalia mazingira murua ya kuweza kubeba majukumu makubwa kwa siku za usoni. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Imekuwa ni fursa pia kwa wajumbe kutoka katika Mashirika ya Umoja Mataifa kushiriki kikamilifu ili kusikiliza na kujibu hoja za vijana wa kizazi kipya. Wajumbe wamegusia pamoja na mambo mengine, shughuli mbalimbali shirikishi kama zilivyobainishwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 na jinsi zinavyoingiliana na utalii duniani. Vijana hawa wameshirikishwa jinsi ya kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kusababisha majanga na maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ikumbukwe kwamba, utalii ni sekta muhimu sana inayotoa fursa za ajira kwa vijana wa kizazi kipya, kiasi cha kuchangia nguvu na mnepo zaidi.
Changamoto kubwa kwa wakati huu ni kuanza mchakato wa mabadiliko ya utalii, kuanzia kwenye jumuiya za ndani. Wajumbe wamepata uzoefu, wamebadilishana mawazo, tayari kuanza kujizatiti katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Itakumbukwa kwamba, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani!