Baraza la Makardinali Ni Washauri Wakuu Wa Khalifa wa Mt. Petro
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema lengo la kuwa na wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwenye Baraza la Makardinali ni kuweza kushuhudia Kanisa moja, takatifu, katoliki na la Mitume; kuendeleza umoja wa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Makanisa mahalia. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba kusudi uaskofu uwe na umoja usiogawanyika, Kristo Yesu alimweka Mtakatifu Petro, juu ya mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi unaodumu na unaoonekana wa umoja wa imani na ushirika wa Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kwa nguvu ya Ukatoliki (Catholicitatis) huu kila sehemu huvipeleka vipaji vyake yenyewe kwa sehemu nyingine na kwa Kanisa lote, hivi kwamba sehemu zote pamoja, na kila moja pia, hukithiri kwa kushirikiana zenyewe kwa zenyewe na kufanya juhudi ili kupata ukamilifu katika umoja. Mamlaka kuu ya Kiti cha Mtakatifu Petro imepewa dhamana ya kusimamia ushirika wote wa mapendo, hulinda tofauti za haki zilizopo kwa kukazia ushirika katika mema na huduma makini kwa watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 13.
Urika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba Mtakatifu, aliye Mwandamizi wa Petro, Mtakatifu na Mtume; kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu kabisa na iwahusuyo wote (plenam, supremama et universalem potestatem) ambayo anaweza kuyatimiza kwa uhuru. Urika wa Maaskofu ni urithi wa urika wa Mitume katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 22-27. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Makardinali hawa wapya kwa sasa ni sehemu ya viongozi wa Kanisa la Roma na watashiriki katika huduma ya kitume. Makardinali wapya wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Kristo na Injili yake sehemu mbalimbali za dunia. Wanatekeleza dhamana na wajibu wao kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Makardinali wapya watakiri kanuni ya imani na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Watavikwa kofia nyekundu ya Kikardinali alama na kielelezo cha heshima ya Ukardinali.
Lakini, ikumbukwe kwamba, alama nyekundu maana yake ni kwamba, wao wako tayari kujisadaka kiasi hata cha kumwaga damu yao kwa ajili ya imani na usalama wa watu wa Mungu; wako tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya uhuru na uenezaji wa Kanisa Katoliki. Makardinali watavikwa pete rasmi, alama ya upendo wao kwa Mtakatifu Petro, ili waweze kuimarisha na kudumisha upendo wao kwa Kanisa la Kristo. Mwishoni, Makardinali wapya watapangiwa Makanisa ya huduma ndani ya Jimbo kuu la Roma, kwani tangu sasa wao ni sehemu ya familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma. Hatimaye, kila Kardinali atapewa Waraka unaomwonesha kuteuliwa na hatimaye kusimikwa kama Kardinali na hivyo kuwa ni kati ya washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu, kwa ajili ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.