Tafuta

Hayati Kardinali Jozef Tomko, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais mstaafu wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa amefariki dunia tarehe 8.8.2022. Hayati Kardinali Jozef Tomko, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais mstaafu wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa amefariki dunia tarehe 8.8.2022. 

Kardinali Jozef Tomko 11 Machi 1924 Hadi 8 Agosti 2022: Huduma

Katika maisha na utume wake, aliihudumia Injili ya Kristo na Kanisa lake kwa unyenyekevu na uadilifu mkuu. Mama Kanisa anapenda kutoa shukrani kwa Mtumishi wake mwaminifu Hayati Kardinali Jozef Tomko, ambaye alitekeleza dhamana na wajibu wake kwa muda mrefu akishirikiana na watangulizi wake. Kwa hakika, alikuwa ni mtu wa sala na ibada kwa Bikira Maria, Rozari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Jozef Tomko, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais mstaafu wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa, aliyefariki dunia tarehe 8 Agosti 2022 mjini Roma, akiwa na umri wa miaka 98. Baba Mtakatifu katika salam za rambirambi alizomtumia Askofu mkuu Bernard Bober wa Jimbo kuu la Košice nchini Slovakia, ndugu, jamaa na waamini wote katika ujumla wao anasema, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wote walioguswa na msiba huu mzito nchini Slovakia. Baba Mtakatifu anamkumbuka ndugu yake katika Kristo Yesu, Kardinali Jozef Tomko, mwenye hekima na busara, aliyekirimiwa zawadi ya imani thabiti na mwenye maono ya mbali katika maisha. Katika maisha na utume wake, aliihudumia Injili ya Kristo na Kanisa lake kwa unyenyekevu na uadilifu mkuu. Mama Kanisa anapenda kutoa shukrani kwa Mtumishi wake mwaminifu Hayati Kardinali Jozef Tomko, ambaye alitekeleza dhamana na wajibu wake kwa muda mrefu akishirikiana na watangulizi wake. Kwa hakika, alikuwa ni mtu wa sala na hata katika uzee wake, aliendelea kubaki daima akisali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya kazi ya ukombozi na mahujaji waliokuwa wakifika jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na hivyo kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Bikira Maria Mama wa Mungu.

KardinaliJozef Tomko 11-Machi 1924 hadi 8 Agosti 2022.
KardinaliJozef Tomko 11-Machi 1924 hadi 8 Agosti 2022.

Baba Mtakatifu anamwomba sasa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kumpokea na kumkaribisha Mtumishi mwaminifu huko kwenye Yerusalemu ya mbinguni. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko ametoa baraka zake za kitume kwa wale wote wanaoomboleza na watakaoshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya Mazishi, itakayoongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Makardinali, Alhamisi tarehe 11 Agosti 2022 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtatakatifu anawapongeza na kuwashukuru kwa namna ya pekee kabisa Watawa wa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo, Satma, waliokuwa wanamtunza kwa upendo na ukarimu mkuu. Itakumbukwa kwamba, Hayati Kardinali Jozef Tomko, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais mstaafu wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa alizaliwa tarehe 11 Machi 1924 huko mjini Udavské, Jimbo kuu la Košice, nchini Slovakia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 12 Machi 1949 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kati ya mwaka 1962 hadi mwaka 1966 aliteuliwa kuwa ni Afisa mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Desemba mwaka 1979, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu.

Kardinali Tomko alikuwa ni mtaalam wa Sinodi na Majadiliano ya Kiekumene
Kardinali Tomko alikuwa ni mtaalam wa Sinodi na Majadiliano ya Kiekumene

Tarehe 12 Julai 1979, akateuliwa kuwa Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu na kupandishwa hadhi kuwa Askofu mkuu na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 15 Septemba 1979. Katika maisha na utume wake, alijipambanua kama mtaalam ya Sinodi za Maaskofu na kunako mwaka 1985 akapewa dhamana ya kuandaa kumbukizi la Miaka 20 tangu kufungwa kwa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya waamini walei iliyoadhimishwa kunako mwaka 1987. Alijiekeza pia katika maisha na utume wa kiekumene, n amara nyingi aliteuliwa kuwa ni kiongozi wa ujumbe wa Vatican katika majadiliano ya kiekumene kati ya Vatican na Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, The Lutheran World Federation, LWF; Kwa lugha ya Kijerumani “Lutherischer Weltbund.” Ni kiongozi aliyejisadaka sana katika majiundo endelevu ili kuhakikisha kwamba, anaendelea kusoma alama za nyakati, licha ya ratiba yake “kubanana sana.”

Hayati Kardinali Jozef Tomko, alipenda pia kutoa huduma za kichungaji kwenye Parokia mbalimbali za Jimbo kuu la Roma kadiri ya mahitaji. Amewahi kuwa ni Mwakilishi wa Vatican kwenye Mikutano ya Kanda ya Makanisa Katoliki Barani Asia, huko Manila mwaka 1970, Mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Oceania, Sydney mwaka 1973, Mkutano wa Puebla wa Mwaka 1979, Jubilei ya Miaka 25 ya CELM mwaka 1980 na Mkutano wa SECAM ulioadhimishwa mjini Yaoundè Cameroon kunako mwaka 1981. Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili akamteuwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kuanzia tarehe 27 Mei 1985 hadi 9 Aprili 2001. Mwaka 1980 aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Rais Mwakilishi wa Sinodi ya Maaskofu kwa Ajili ya Bara la Ulaya. Kati ya tarehe 15 Oktoba 2002 hadi tarehe 1 Oktoba 2007 aliteuliwa kuwa ni Rais wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa. Ilikuwa ni tarehe 25 Mei 1985 Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteuwa na kumsimika kuwa ni Kardinali. Tarehe 8 Agosti 2022 akafariki dunia. Sasa Apumzike katika usingizi wa amani akiwa na tumaini la maisha na uzima wa milele. Amina.

Kardinali Tomko
09 August 2022, 15:21