Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha Mapadre na Viongozi wote wa Kanisa kuwa ni wachungaji wema kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yohane Maria Vianney katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha Mapadre na Viongozi wote wa Kanisa kuwa ni wachungaji wema kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yohane Maria Vianney katika maisha na utume wake. 

Kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney: Mchungaji Mwema!

Mtakatifu Yohane Maria Vianney alizaliwa mwaka 1786. Kwa taabu sana akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 12 Agosti 1815 na kufariki dunia Agosti 1859 akiwa na umri wa miaka 73. Tarehe 8 Januari 1905 akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Pio X. Mwaka 1925 Papa Pio wa XI akamtangaza kuwa Mtakatifu na mwaka 1929 akamtangaza kuwa ni Msimamizi wa Maparoko duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa, tarehe 4 Agosti ya kila mwaka anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney, changamoto na mwaliko kwa Mapadre wote, kuiga mfano wa Kristo Yesu mchungaji mwema. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, Kristo Yesu ni mchungaji mwema kwa sababu anawapenda upeo. Ni katika muktadha huu, Mapadre na viongozi wa Kanisa katika ujumla wao, wanapaswa kuonesha ule moyo wa ukarimu kwa kulisha Kondoo wa Kristo, ili kuwatangazia na kuwashuhudia huruma na upendo wake, kutokana na madonda ambayo kila mmoja wao anayo! Katika maadhimisho ya Miaka 150 tangu Mtakatifu Yohane Maria Vianney alipofariki dunia, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akatangaza Maadhimisho ya Mwaka wa Mapadre Duniani. Huu ukawa ni muda wa kufanya tafakari ya kina kuhusu: Ukuu, Utakatifu, Wito na Maisha ya Kipadre ndani ya Kanisa. Mapadre walikumbushwa kwamba, utambulisho na uhuru wa wafuasi wa Kristo Yesu ni mambo makuu mawili yanayowawezesha hata Mapadre katika maisha na utume wao, kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Kama binadamu wanatambua udhaifu na uwepo wa dhambi katika maisha yao, changamoto ya kutubu na kuongoka, ili kuanza hija ya utakatifu inayokita mizizi yake katika mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu.

Mapadre ni wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa
Mapadre ni wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa

Mapadre wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, kwa mfano wa utakatifu wa maisha yao, wawasaidie waamini walei kuiona njia ya hija ya utakatifu wa maisha, kwa kukazia umoja, maisha ya kisakramenti, kazi na utume wa mashirika na vyama mbalimbali vya kitume parokiani, bila kusahau, nidhamu na wajibu wa kila mwamini. Uaminifu wa Mapadre na walei uwawezeshe kuuona utakatifu, kwa njia ya maisha ya kisakramenti, liturujia na sala, kila upande ukijitahidi kutekeleza wajibu wake. Mama Kanisa, tarehe 4 Agosti 2019 aliadhimisha kumbukumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney. Papa Pio XI kunako mwaka 1929 akamtangaza kuwa ni Msimamizi na Mwombezi wa Maparoko Duniani. Ni Padre ambaye kwa muda wa miaka 40 alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watu wake kwa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa; akajitakatifuza kwa sala, toba na wongofu wa ndani, uliofumbatwa katika maisha ya unyenyekevu. Akajitahidi kuwaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha, kuelekea kwenye furaha ya uzima wa milele. Katika Maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko aliwaandikia Mapadre wote duniani, barua ya upendo na mshikamano wa kibaba, akiguswa na furaha ya huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbalimbali za dunia, kila kukicha! Hawa ni mapadre ambao wengine wamechoka na kudhohofu kwa afya mbaya na changamoto za maisha; kuna baadhi yao wametumbukia katika mateso na mahangaiko makubwa ya ndani kutokana na huduma yao kwa familia ya Mungu.

Mapadre wawe ni chumvi na mwanga wa ulimwenfu kwa njia ya maisha adili.
Mapadre wawe ni chumvi na mwanga wa ulimwenfu kwa njia ya maisha adili.

Licha ya mambo yote hayo, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mapadre wanaendelea kuandika kurasa za maisha na utume wa Kipadre sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu katika barua hii anapenda kuwashukuru na kuwatia moyo Mapadre, wote wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni marafiki wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, ameyaona mateso na mahangaiko ya watu wake, anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mapadre, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji wote katika nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha yao. Ushuhuda wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Maria Vianney uwe ni mfano bora wa sadaka na majitoleo ya maisha na utume wa Kipadre katika ulimwengu mamboleo. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Maria Vianney alizaliwa kunako tarehe 8 Mei 1786. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi kwa shida kubwa, alipewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 12 Agosti 1815. Akafariki dunia tarehe 4 Agosti 1859 akiwa na umri wa miaka 73. Tarehe 8 Januari 1905 akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Pio X. Ilikuwa ni tarehe 31 Mei 1925 Papa Pio wa XI akamtangaza kuwa Mtakatifu na kunako mwaka 1929 akamtangaza kuwa ni Msimamizi wa Maparoko duniani.

Maparoko

 

04 August 2022, 15:45