Papa Francisko Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V kuendelea hadi tarehe 28 Agosti 2023. Papa Francisko Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V kuendelea hadi tarehe 28 Agosti 2023. 

Papa Francisko: Mwaka wa Msamaha wa Celestin V Kufungwa Rasmi Tarehe 28 Agosti 2023

Baba Mtakatifu Francisko amemua kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Huruma ya Papa Celestine V, yataendelea na hatima yake ni tarehe 28 Agosti 2023. Waamini na mahujaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia watakaotembelea Kanisa kuu la Jimbo kuu la L’Aquila la “Santa Maria wa Collemaggio” wakifuata sheria, kanuni na taratibu wanaweza kujipatia rehema kamili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 28 Agosti 2022 amezindua rasmi Maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V, kwa kufungua lango la Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio” Jimbo kuu la Aquila, nchini Italia. Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Dominika ya 22 ya Mwaka C wa Kanisa na baadaye, kuongoza Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio.” Amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Asasi za kiraia pamoja na waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 6 Aprili 2009 mjini L’Aquila. Takwimu zinaonesha kwamba watu 309 walipoteza maisha, watu wengine 1,600 kujeruhiwa vibaya na watu 80, 000 wakabaki bila makazi maalum baada ya nyumba zao kubomolewa na kutofaa tena kwa matumizi ya binadamu. Msamaha wa Celestin ni tukio la kihistoria na kidini linaloadhimishwa kila mwaka huko L'Aquila nchini Italia kuanzia tarehe 28 na 29 Agosti. Sherehe hii ilianzishwa na Papa Celestine V kunako mwaka 1294 kwa kuchapisha Waraka wa Kitume “Inter Sanctorum Solemnia”; Waraka huu unajulikana pia kama “Msamaha wa Celestin” unaojikita katika huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa watu wote. Waamini wanaweza kujipatia rehema kamili, ikiwa kama watafuata masharti, kanuni na taratibu zilizowekwa na Mama Kanisa. Kwa kuingia na kushiriki katika Ibada kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la L’Aquila la “Santa Maria wa Collemaggio” Masifu ya jioni ya tarehe 28 Agosti hadi masifu ya jioni ya tarehe 29 Agosti.

Mwaka wa Msamaha wa Celestin kufungwa 28.2.2023
Mwaka wa Msamaha wa Celestin kufungwa 28.2.2023

Maadhimisho haya yalizinduliwa tarehe 23 na kilele chake ni tarehe 30 Agosti 2022. Kilele cha Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V kimekuwa kikiadhimishwa ili kuwakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuchuchumilia na kuambata amani, kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu. Maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Huruma ya Papa Celestine V, yamepitia katika vitongoji mbalimbali vya Jimbo kuu la L’Aquila yaani: “Eremo del Morrone, Sulmona na hatimaye Kanisa kuu la L’Aquila. Mada ambazo zimekuwa zikijadiliwa ni pamoja na: Dhana ya Msamaha katika maisha ya mwamini; Dhana ya Kanisa kama chombo cha huruma na matumaini kuanzia kwa Papa Celestine V hadi Baba Mtakatifu Francisko; Uhuru wa watu wa Mungu kukutana katika ukweli na haki na hatimaye ni tema kuhusu Papa Celestin V. Maadhimisho haya yanatoa pia mkazo kwa majadiliano ya kiekumene, haki, amani, msamaha na maridhiano. Ni katika muktadha wa umuhimu wa waamini kuendelea kujikita katika msingi wa haki, amani na maridhiano, Baba Mtakatifu Francisko amemua kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestine V, yataendelea na hatima yake ni tarehe 28 Agosti 2023. Waamini na mahujaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia watakaotembelea Kanisa kuu la Jimbo kuu la L’Aquila la “Santa Maria wa Collemaggio” wakifuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Mama Kanisa wanaweza kujipatia rehema kamili.

Waamini wajibidiishe kutafuta haki, amani, msamaha na upatanisho
Waamini wajibidiishe kutafuta haki, amani, msamaha na upatanisho

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, ameonesha matumaini makubwa kwamba, mji wa L’Aquila utaweza kugeuka na kuwa ni mji mkuu wa: msamaha, amani na maridhiano. Uwe ni chachu ya mageuzi kama yanavyoimbwa na Bikira Maria kwenye utenzi wake wa “Magnificat”: “Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.” Lk 1: 51-53. Na Kristo Yesu katika Injili anakaza kusema, “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” Lk 14: 11. Bikira Maria anaheshimiwa na watu wa Mungu Jimboni humo kama Wokovu wa Watu wa L’Aquila, mwaliko na changamoto kwa waamini kumwilisha Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha yao, ili Bikira Maria aweze kuombea msamaha na amani kwa dunia nzima. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu alikuja ulimwenguni ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, ili wote watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba yao na anawapenda wote upeo. Hiki ndicho kiini cha Injili na ushuhuda wa Injili hii ni Fumbo la Umwilisho, kwani Kristo Yesu ni Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Maadhimisho ya Dominika ya 22 ya Mwaka C wa Kanisa kwa mwaka 2022 yanachukua uzito wa pekee kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la L’Aquilla, kwani Mama Kanisa anaadhimisha Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V, uliozinduliwa kwa kufungua lango la Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio” Jimbo kuu la Aquila. Papa Celestin V ni kielelezo cha sehemu ya Maandiko Matakatifu isemavyo “kadiri ulivyo mkuu uzidi kujinyenyesha, nawe utapata kibali machoni pa Bwana”. YbS 3:18. Papa Celestin V alikuwa ni kiongozi mwenye utashi thabiti, aliyejitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wake, kwa kujivika fadhila ya unyenyekevu iliyomwezesha kutambua na hatimaye, kutekeleza mapenzi ya Mungu, kwa kupata kibali machoni pa Bwana, kwa maana rehema zake Bwana zi kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu. Rej. YbS 3: 19-20.

Mwaka wa Msamaha

 

29 August 2022, 17:06