Mwaka wa Mtakatifu Yakobo Mtume: Siku ya 38 ya Vijana Duniani, Lisbon, Ureno, 2023
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mwaka wa Mtakatifu Yakobo Mkuu ulizinduliwa rasmi tarehe 31 Desemba 2020 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Ondoka katika nchi yako. Mtume anakungoja”. Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko alitoa mwaliko kwa waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kukutana na Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Ni fursa ya kukutana na kutembea pamoja na jirani. Ni mwanya wa kumfuasa Kristo Yesu aliye: Njia, Ukweli na Uzima, ili kuonja upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka. Baba Mtakatifu anatambua udhaifu na hali ya dhambi inayomwandama mwanadamu na kwamba, waamini wakijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu wanaweza kuanza tena upya kutembea katika njia ya haki. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 7 Agosti 2022, amewapongeza vijana kutoka sehemu mbalimbali za Bara la Ulaya waliohitimisha hija yao kwenye Madhabahu ya Santiago de Compostella, Hispania kuanzia tarehe 4-8 Agosti 2022. Hili ni tukio ambalo lilisheheni Katekesi za kina. Ikumbukwe kwamba, Katekesi ni mafundisho yaliyo katika utaratibu wa Mafundisho ya Kanisa katika ukamilifu, kwa nia ya kuwatayarisha waamini kwa maisha kamili ya Kiinjili.
Lengo kuu ni kujenga na kudumisha ushirika, mshikamano na udugu wa kibinadamu kwa karibu na katika undani na Kristo Yesu. Hija hii, iliwakutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali za Bara la Ulaya, ili kushirikishana ndoto, mang’amuzi na vipaumbele katika maisha yao. Ilikuwa ni fursa pia ya kusoma, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Hija hii, imewawezesha vijana kusherehekea Injili ya uhai. Itakumbukwa kwamba, Mwaka wa Mtakatifu Yakobo Mtume ilikuwa ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu, kwa kumtambua jirani yao kuwa ni zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hapa jambo la msingi ni kujenga na kudumisha utu na heshima ya binadamu anayepewa kipaumbela cha kwanza na wala si vitu vinavyopita. Mahujaji wanaotembelea nchini Hispania ni watu wanatoka katika mataifa, lugha na tamaduni mbalimbali. Kumbe, katika mazingira haya, wote kwa pamoja wajisikie kuwa ni sehemu ya wamisionari mitume, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kuanzia mahali wanapoishi hadi miisho ya dunia.
Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kutekeleza hija hii kwa moyo wa imani, matumaini na mapendo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Iwe ni fursa ya kutafakari Uso wa huruma ya Mungu; waguswe na maisha na utakatifu wa Yakobo Mtume, kwa kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi na kwamba, wote ni watoto wa Mungu wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili. Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yakobo Mtume, nchini Hispania yaliathirika sana kutokana na kuenea kwa maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Idadi ya mahujaji imepungua kwa kiasi kikubwa kwa hofu ya masharti ya UVIKO-19. Ni kutokana na mazingira haya, Baba Mtakatifu Francisko alitoa kibali kwamba, maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yakobo yaendelee hata katika kipindi cha Mwaka 2022. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umekuwa ni tishio katika maisha ya kiroho kwa waamini wengi kutokana na madhara yake: kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata katika maisha ya kiroho. Kuna wimbi kubwa la ukoloni wa kiitikadi linalotishia Injili ya uhai sanjari na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Maaskofu wa Hispania wanasema, kuna haja ya kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi kipya wanatangaziwa na kurithishwa imani kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Hili ni jukumu linaloweza kutekelezwa kwa ufanisi zaidi kwa njia ya waamini walei, waliofundwa barabara katika: Imani, Katekesi, Amri za Mungu na Maisha ya Sala. Kwa maneno mafupi, ni waamini wanaoifahamu vyema Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Maaskofu wanaendelea kuwekeza zaidi katika maisha na utume wa waamini walei kwa kutambua kwamba, wanao wajibu na dhamana ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Kimsingi hija ya vijana wa Ulaya kwenye Madhabahu ya Santiago de Compostella, Hispania kuanzia tarehe 4-8 Agosti 2022 ni sehemu ya maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani, itakayoanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 1 hadi 6 Agosti 2023 Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39.
Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha vijana kwamba wao ni matumaini na jeuri ya maisha na utume wa Kanisa, kumbe, wanapaswa kuwa makini zaidi katika maisha yao ya kila siku, huku wakiwa na ndoto na matamanio halali ya maisha. Kamwe vijana “wasimwagilie nyoyo na akili zao” kwa litania ya malalamiko yasiyokuwa na kichwa wala miguu. Wajenge na kudumisha utamaduni wa kushirikiana na kushirikishana na wengine amana na utajiri ambao Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha. Wajenge ari na moyo wa kujadiliana na wengine katika ukweli na uwazi; wawe tayari kuwasikiliza wengine wanapozungumza, ili kuthamini mchango, hekima na busara yao. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, maisha yao daima ni safari pamoja na Kristo Yesu, kuelekea kwa Mwenyezi Mungu; kuelekea kwa ndugu na jamaa; kimsingi ni safari ya huduma na furaha!