Alpha Youth Camp 2022: Uinjilishaji wa Vijana wa Kizazi Kipya: Ushuhuda Wa Maisha Adili
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kikundi cha vijana zaidi ya 400 kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya Italia kijulikanacho kama “Alpha Youth Camp 2022” ni juhudi za Askofu Camillo Cibotti wa Jimbo Katoliki la Isernia-Venefro lililoko nchini Italia katika mchakato wa kuwainjilisha vijana wa kizazi kipya, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ni fursa ya kujenga urafiki kati ya vijana, kushirikishana mang’amuzi na kuota ndoto ya pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni fursa kwa vijana kuanzia tarehe 31 Julai hadi 7 Agosti 2022 kukutana na kujadiliana, ili hatimaye, kushirikishana mang’amuzi na uzoefu wa maisha ya ujana pamoja na changamoto zake, ili kwa pamoja kutangaza Injili ya matumaini kwa vijana waliovunjika na kupondeka moyo! Wawezeshaji ni watu kutoka katika medani mbalimbali za maisha. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 5 Agosti 2022 amekutana na kuzungumza na Vijana wa Kikundi cha “Alpha Youth Camp 2022.” Katika hotuba yake amejitahidi kujibu maswali msingi yanayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo za vijana wa kizazi kipya. Amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha mahusiano na Mwenyezi Mungu, Kazi ya Uumbaji pamoja na jirani zao. Amegusia kuhusu Wosia wake wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” na uinjilishaji wa vijana unaotekelezwa na “Alpha Youth Camp 2022” kama chimbuko la amani na usalama wa vijana wa kizazi kipya.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, vijana ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Kanisa. Anawashukuru na kuwapongeza kwa uwepo wao. Anasema, ujana ni kipindi kinachosheheni maswali msingi ya maisha: asili na hatima ya maisha ya mwanadamu; mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia na hasa watoto wadogo; maana ya maisha katika ujana wao. Ujana ni kipindi cha udadisi kwa maswali mengi. Kwa wale vijana ambao hawana maswali, watambue kwamba, tayari uzee umeanza kuwanyemelea. Baba Mtakatifu anasema, akiwa nchini Canada wakati wa hija yake ya kitume, alibahatika kukutana na kuzungumza na wazee pamoja na vijana wa Canada ambao kwa kiasi kikubwa wameathirika na mifumo mbalimbali ya ukoloni. Ni vijana wanaojitambua na wanataka kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii na jirani zao pamoja na mazingira nyumba ya wote, huku wakikuza na kudumisha uhuru, ukarimu, sadaka na majitoleo binafsi, kama sehemu ya kutegemeana na kukamilishana, ili kupata utimilifu wa maisha na furaha ya kweli.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Machi 2019 akiwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, aliweka sahihi kwenye Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”. Wosia huu umezinduliwa rasmi, tarehe 2 Aprili 2019. Wosia huu ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito”. Huu pia ni mwendelezo wa mchakato wa Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia, kwani utume wa Kanisa kwa familia na vijana ni sawa na chanda na pete; unategemeana na kukamilishana! Wosia huu wa kitume umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana na Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini ya vijana wa kizazi kipya. Anawaita, ili kuwatia shime, kuwafariji na kuwakirimia nguvu ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, kama ilivyokuwa kwa Mitume wake. Kristo Yesu ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho na kwamba, Nyakati zote ni zake. Ana nguvu za kuweza kumwokoa mwanadamu, kwa sababu ni chemchemi ya maisha na upendo mkamilifu.
Kwa kushikamana na kuandamana na Kristo Yesu, vijana wataweza kukua na kukomaa na hivyo kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi, na hivyo kuwathamini wengine jinsi walivyo na katika utu, heshima na haki zao msingi. Ni kwa njia hii, vijana waweza kuwajibika barabara, huku wakijitahidi kufuata nyayo zake. Kristo Yesu ni chemchemi ya amani na utulivu wa ndani na anamtaka kila mmoja wao, afikie ukomavu kama ilivyokuwa kwa Mwenyeheri Carlo Acutis, kijana aliyependa “kuvaa jeans”, alikuwa ni “mchawi wa Computer”, lakini alikuwa na upendo wa pekee sana kwa Kristo Yesu, kiasi cha kujenga utamaduni na mazoea ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ambayo kwake, ilikuwa ni njia ya kumpeleka mbinguni, tangu siku ile alipopokea kwa mara ya kwanza Ekaristi Takatifu. Kristo Yesu, akawa ni rafiki na mwandani wa safari ya maisha yake hapa duniani.