Papa Francisko Azungumza Kwa Simu na Rais Zelensky wa Ukraine: Madhara ya Vita
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea kutoka kwenye hija yake ya kitume nchini Canada katika mahojiano na waandishi wa habari alisema ataendelea kufanya hija za kitume kama njia ya kuwahudumia watu watakatifu wateule wa Mungu na kuwaonesha ukaribu wake kwao. Anakaza kusema, bado ametia nia ya kutembelea Ukraine, Kazakhstan, Sudan ya Kusini na DRC. Hija ya Kitume Sudan ya Kusini, ina mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa. Hija hizi, pengine zinaweza kutekelezwa mwaka 2023, kwa sasa bado anasikilizia maumivu ya miguu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anataka kutembelea mji wa Kiev, nchini Ukraine kama kielelezo cha uwepo wake na mshikamano wa dhati na watu wa Mungu nchini Ukraine wanaoteseka kutokana na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urussi tangu tarehe 24 Februari 2022. Kwa mara nyingine tena, Ijumaa tarehe 12 Agosti 2022, Baba Mtakatifu Francisko amezungumza kwa njia ya simu na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kuhusu madhara ya vita nchini humo.
Rais Volodymyr Zelensky katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa sala, uwepo pamoja na mialiko mbalimbali ya kusitisha vita nchini Ukraine. Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii Balozi Andrii Yurash, mwakilishi wa Ukraine mjini Vatican amesema, watu wa Mungu nchini humo wanasubiri kwa hamu kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye ametia nia kweli ya kutembelea mji wa Kiev, nchini Ukraine. Baba Mtakatifu Francisko mara kadhaa, ameonesha masikitiko yake makuu kutokana na athari za vita nchini Ukraine na kuwataka wahusika kuachana na falsafa ya kutumia mtutu wa bunduki kama suluhu ya matatizo na changamoto zilizopo na badala yake, wajikite katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika nchi hizi mbili. Katika kipindi hiki cha vita na chenye changamoto nyingi katika maisha, wananchi wa Ukraine, wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo na ushuhuda wake unaowatia shime katika maisha yao ya kiroho, kusonga mbele.
Baba Mtakatifu anasikita kuona kwamba, vita kati ya Ukraine na Urussi inaendelea kuzalisha makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi wanaohitaji: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Balozi Andrii Yurash, mwakilishi wa Ukraine mjini Vatican, hivi karibuni alikutana kwa faragha na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican na kusema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko bado ametia nia ya kutembelea Ukraine hasa kutokana na madhara makubwa ya vita kwa watu wa Mungu nchini Ukraine. Kwa upande wake, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nje na ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa hivi karibuni katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Italia Tg1, tarehe 8 Julai 2022 alithibitisha kwamba, Baba Mtakatifu ametia nia ya kutembelea Kiev, Ukraine na angependa kutembelea pia Urussi ili kukutana na viongozi wakuu wa Urussi na ikiwezekana kukutana na Patriaki Cyril wa Moscow na Russia nzima kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu: kiroho na kimwili. Jambo la msingi ni majadiliano katika ukweli na uwazi.