PAPA: Mkutano wa 8 wa Baraza la Makardinali 27-30 Agosti 2022 : Kura Kwa Watakatifu Wapya!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 27 Agosti 2022 majira ya jioni, ataongoza mkutano wa Baraza la Makardinali na kuwasimika Makardinali wapya 21 walioteuliwa tarehe 29 Mei 2022. Makardinali pia watawapigia kura wenyeheri wafuatao wanaotarajiwa kutangazwa na kuwekwa kwenye orodha ya watakatifu wa Kanisa Katoliki. Nao ni: Padre Giovanni Battista Scalabrini aliyetangazwa kuwa Mwenye heri na Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 9 Novemba 1997. Alizaliwa tarehe 8 Julai 1839 na hatimaye kufariki dunia tarehe Mosi Juni 1905. Alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Piacenza-Bobbio, Italia na Mwanzilishi wa Mashirika ya Wamisionari wa Mtakatifu Carlo Borromeo, maarufu kama Wascalabriani na pia ni Muasisi wa Taasisi ya waamini Walei Wascalabrini, iliyoanzishwa kunako mwaka 1961. Pamoja na Mwenyeheri Artemide Zatti, Bruda wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco aliyezaliwa tarehe 12 Oktoba 1880, nchini Italia. Akafariki dunia tarehe 15 Machi 1951 huko Viedma nchini Argentina. Utakatifu wake unapata chimbuko lake katika huduma kwa maskini kwa kuongoza hospitali na duka la dawa kwa ajili ya maskini kwa muda wa miaka 40. Tarehe 14 Aprili 2002 atakatangzwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Mwenyeheri.
Itakumbukwa kwamba, huu ni mkutano wa nane wa Baraza la Makardinali kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013. Kati ya Makardinali wateule ni: Arthur Roche, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, Lazzaro You Heung-sik, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri pamoja na Fernando Vèrgez Alzaga, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Mji na Serikali ya Vatican. Askofu Peter Eberechukwu Okpaleke wa Jimbo Katoliki la Ekwulobia, anayetoka eneo la Mashariki mwa Nigeria ambaye historia ya maisha na utume wake kama Askofu imewaacha wengi wakiwa wamepigwa bumbuwazi! Richard Kuuia Baawobr, M. Afr. Askofu Wa Jimbo Katoliki la Wa, Ghana ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 28 Agosti 2022 atazindua rasmi maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Huruma ya Papa Celestine V, kwa kukazia umuhimu wa Mama Kanisa kuendelea kujikita katika huruma na matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo, ili waonje tena upendo wa Baba wa milele. Jumatatu tarehe 29 na Jumanne tarehe 30 Agosti 2022 ataongoza mkutano wa Baraza la Makardinali, ili kufanya tafakari ya kina kuhusu Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.”
Katiba imeanza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022, Sherehe ya Pentekoste na hivyo kuchukua nafasi ya Katiba ya Kitume “Pastor bonus” ya tarehe 28 Juni 1988 iliyoanza kutumika rasmi 1 Machi 1989. Jumanne tarehe 30 Agosti 2022 majira ya saa 11:30 kwa Saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu akishirikiana na Makardinali wapya 21 pamoja na Baraza la Makardinali. Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.
Katiba hii mpya ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Baraza la Makardinali katika mikutano yake elekezi kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro uliofanyika mwaka 2013. Haya ni matunda ya kazi kubwa iliyotekelezwa na Baraza la Makardinali Washauri kuanzia mwezi Oktoba 2013 hadi Februari 2022 na hatimaye, kuchapishwa tarehe 19 Machi 2022 chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko bila kusahau mchango uliotolewa na Makanisa mahalia kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Katiba hii kwa sasa inatekeleza mabadiliko makubwa yanayofanyiwa na Baba Mtakatifu tangu alipoteuliwa kuliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013. Kuna baadhi ya Mabaraza ya Kipapa yameunganishwa ili kuongeza tija, ubora na ufanisi katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu, sanjari na kuunda Mabaraza mapya ya Kipapa. Sekretarieti kuu ya Vatican inayojulikana kama “Curia Romana” inaundwa na Sekretarieti ya mji wa Vatican, Mabaraza ya Kipapa na Ofisi mbalimbali zenye haki sawa katika utendaji wake. Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, lililokuwa linajulikana kama “Apostolic Elemosineria” yaani “Idara ya Sadaka ya Kitume” limeanzishwa ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili, yanayotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbalimbali za dunia.
Katiba ya Kitume “Hubirini Injili” inayagawanya Mabaraza ya Kipapa katika makundi makuu matatu: Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Uinjilishaji. Pili, Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Tatu ni Baraza ya Kipapa kwa Ajili ya Huduma ya Upendo. Mabadiliko mengine makubwa ni kuhusu Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi kwa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ambayo kwa sasa itakuwa chini ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na itaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zake pamoja na kuwa na Rais na Katibu wake. Sehemu kubwa ya Katiba ya Kitume ya “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” inajikita katika sheria, kanuni na taratibu na kwamba, kila Mkristo kwa Ubatizo wake ni Mtume mmisionari anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema. Ni katika muktadha huu, hata waamini walei wenye sifa zinazohitajika wanaweza kuteuliwa kuchukua nafasi za uongozi kwenye Sekretarieti kuu kadiri ya Mamlaka aliyokabidhiwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katiba ya Kitume inabainisha vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa ili Mkristo aweze kuteuliwa kutoa huduma katika “Curia Romana.” Hii ni huduma kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro inayomwajibisha mwamini kujenga na kudumisha ushirika sanjari na kutoa huduma kwa utume wa Maaskofu, Makanisa Mahalia, Mabaraza ya Maaskofu na Miundombinu ya Makanisa ya Mashariki.
Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapewa kipaumbele cha pekee. Sekretarieti kuu ya Vatican sanjari na dhana ya Mtume mmisionari ni hata kwa wale ambao wameteuliwa kufanya kazi kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Haya ni mambo makuu mawili yanayopaswa kuendelea kumwilishwa mintarafu Katiba ya Kitume ya “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili.” Hawa ni waamini wanaopaswa kuwa na tasaufi imara, maadili, ujuzi na weledi; mwenye uwezo wa kushirikiana na kwamba, uteuzi wa wafanyakazi wa Sekretarieti kuu, ni utambulisho wa Ukatoliki wa Kanisa na kwamba hauna budi kujidhihirisha bila shaka. Wakleri na watawa wataweza kutoa huduma yao kwa muda wa miaka mitano na mkataba huu, unaweza kurudiwa tena katika kipindi cha miaka mitano, baada ya hapo, mhusika atapaswa kurejea Jimboni au Shirikani mwake. Katiba hii mpya inaweka mkazo kwamba, hii ni “Sekretarieti ya Kipapa”. Kumbe, kuna uwezekano mkubwa kwa wafanyakazi wa Sekretarieri kuu ya Vatican kuhamishiwa kutoka Idara moja kwenda Idara nyingine, kadiri ya mahitaji na ufafanuzi kutoka kwenye Sekretarieti ya Uchumi, SPE au maelekezo yatakayotolewa na Msimamizi wa Urithi na Mali ya Kitume, APSA.