Papa Francisko Mlipuko wa Lebanon 2020: Faraja Katika: Imani, Haki na Ukweli
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Usiku wa kinzani na migogoro utoweke; mapambazuko ya matumaini yaangaze, chuki na uhasama vikome, Lebanon irejee tena kuangaza nuru ya amani. Hii ndiyo sala ya Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon aliyoitoa tarehe 1 Julai 2021; Siku Maalum ya Sala, Kufunga na Kutafakari Kuhusu Hatima ya Lebanon. Siku hiyo ilinogeshwa na kauli mbiu: “Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani.” Sote kwa pamoja kwa ajili ya Lebanon. Yer 29: 11. Ilikuwa ni fursa ya kusikiliza matumaini na matarajio ya watu wa Mungu kutoka Lebanon, waliokuwa wamechoka, wakapondeka nyoyo na kukata tamaa ya maisha. Walimwomba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awakirimie mwanga wa matumaini na hivyo kuvuka kipeo hiki cha mateso na mahangaiko makubwa. Baba Mtakatifu Francisko alichangia kiasi cha Euro 250, 000, ili kulisaidia Kanisa kuweza kukabiliana na changamoto zilizojitokeza kutokana na mlipuko uliotokea kwenye eneo la bandari ya Beirut, tarehe 4 Agosti 2020. Watu zaidi ya 150 walipoteza maisha na wengine 5, 000 kujeruhiwa vibaya na watu 3, 000 kukosa makazi baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na mlipuko huo.
Baba Mtakatifu Jumatano tarehe 3 Agosti 2022 mara baada ya Katekesi kuhusu Hija yake ya Kitume nchini Canada kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 30 Julai, 2022, aligusia kumbukizi la miaka miwili tangu mlipuko wa Bandari ya Beirut ulipotokea tarehe 4 Agosti 2020 na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Lebanon walioathirika kutokana na mlipuko huo. Anawaombea ili wafarijike kwa imani, haki na ukweli ambao kamwe hauwezi kufichama. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kuisaidia Lebanon ili kuanza tena upya, kwa kuendelea kusimama kidete katika uaminifu wake mintarafu amani na maridhiano ya watu wa Mungu ili kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 4 Agosti 2021, Mwaka mmoja tangu Mlipuko wa Lebanon alisema, bado ametia nia ya kutembelea Lebanon na kamwe hachoki kusali na kuwaombea, ili Lebanon iweze kurejea tena kuwa ni ujumbe wa amani na udugu wa kibinadamu huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikishwa na mlipuko huo, kiasi cha kupoteza: maisha, makazi, fursa za ajira na ndoto ya kuendelea kuishi. Baba Mtakatifu ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi ili kuisaidia Lebanon, ili iweze “kufufuka tena” kwa vitendo na wala si kwa maneno matupu! IBaba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Watu wa Mungu nchini Lebanon alioutoa wakati wa Liturujia ya Kiekumene kwa ajili ya kuombea amani; aliomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu kwa niaba ya viongozi wa Makanisa walioshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Alisema, nchi ya Lebanon ni amana na utajiri wa ustaarabu pamoja na tasaufi ambayo imekuwa ni chemchemi ya maridhiano na amani.
Ni wito na dhamana ya Lebanon kuwa ni nchi inayokita mizizi yake katika uzoefu wa amani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Lebanon kuzamisha mizizi yao katika ndoto ya amani, tayari kung’arisha mwanga wa matumaini. Anasema, kamwe wasichoke kumlilia Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, ili aweze kuwakirimia waja wake amani ya kudumu. Nchi ya Lebanon ni amana na utajiri wa ustaarabu pamoja na tasaufi ambayo imekuwa ni chemchemi ya maridhiano na amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ujumbe unaosikika kwa wakati huu kutoka Mashariki ya Kati ni amani na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani; anao mpango mkakati kwa ajili ya amani huko Lebanon na huu ni mradi unaopaswa kudumu katika amani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kumezwa na malimwengu. Lebanon na Mashariki ya Kati katika ujumla wake, “lisiwe ni pango la wevi” kwa ajili ya masilahi ya watu wachache, wanaotaka faida na utajiri wa haraka haraka.
Baba Mtakatifu anawakumbusha watu wa Mungu nchini Lebanon kwamba, Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani; anao mpango mkakati kwa ajili ya amani huko Lebanon. Umoja na tofauti zao msingi ziliwawezesha wahenga wa Lebanon kuishi kwa umoja, upendo na maridhiano. Huu ni wakati wa kuzamisha mizizi kwa ajili ya ndoto ya amani, kwa kushirikiana na wengine. Wananchi wasikate tamaa bali waendelee kuwa na matumaini. Viongozi wa kisiasa kadiri ya wajibu wao watafute majibu ya matatizo na changamoto za kiuchumi kwa kujikita katika haki kama msingi wa amani. Wananchi wa diaspora kutoka Lebanon, wajifunge kibwewe kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zao huko Lebanon. Jumuiya ya Kimataifa isaidie juhudi za kufufua uchumi nchini Lebanon; yote haya ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kama Lebanon inataka kujenga na kudumisha amani; wote wanapaswa kuungana na kushikamana ili kutenda katika umoja, upendo na huruma.
Wakristo wanaitwa na kuchangamotishwa kuwa ni wapanzi wa amani na wajenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kuwajibika kikamilifu sanjari na kuendelea kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika njia ya amani. Majadiliano ya kidini na kiekumene yaimarishe mchakato wa umoja na mshikamano, tayari kufanya kazi kwa pamoja kama ndugu! Katika amani hakuna mshindi wala anayeshindwa. Ni wakati wa kunogesha majadiliano, kukuza na kudumisha elimu na mshikamano wa kweli. Katika pazia la usiku wa giza nene, kuna mapambazuko ya matumaini kama walivyoonesha vijana waliowakabidhi viongozi wa kidini mishumaa inayowaka, kielelezo cha matumaini kwa sasa na kwa siku zijazo. Katika mchakato wa kufanya maamuzi, viongozi watambue na kukumbuka kwamba, watu wanataka kuona mwanga wa matumaini ukiwashwa katika safari ya maisha yao. Viongozi waongozwe na mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika dhamiri nyofu, ili kuwashirikisha watu wa Mungu matumaini mapya. Wanawake wathaminiwe na kushirikishwa katika vikao vyote vinavyotoa maamuzi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Lebanon. Katika kipindi hiki cha kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii, changamoto kubwa ni wote kushikamana na kuungana ili kuwa ni kitu kimoja. Kwa njia hii wataweza kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; ili kuendeleza nia njema, ili hatimaye, kuwasha mwanga wa matumaini pale penye giza. Mwishoni mwa ujumbe wake kwa watu wa Mungu nchini Lebanon, Baba Mtakatifu aliwaaminisha wote chini ya ulinzi na tunza ya Kristo Yesu, Mfalme wa amani, ili awakirimie huruma na matumaini! Usiku wa kinzani na migogoro utoweke; mapambazuko ya matumaini yaangaze, chuki na uhasama vikome, Lebanon irejee tena kuangaza nuru ya amani.