Papa kwa Kbs:Utayari wa kwenda Korea Kaskazini kwa jina la Udugu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara tu atakapopata mwaliko Papa Francisko, atakwenda nchini Korea Kaskazini bila kusita kwa jina la udugu. Aliyethibitishwa hayo ni yeye mwenyewe katika mahojiano yaliyofanyika mnamo tarehe 24 Agosti iliyopita na kuchapishwa tatehe 27 Agosti katika Luninga ya Baraza la Maaskofu wa Korea Kusini (KBS), ambapo amerudia kuzungumzia juu ya mada pendwa zilizo kwenye Waraka wa Fratelli tutti.
Amani ni zawadi ambayo lazima kuifanyia kazi kila siku
Kwa mujibu wa Papa Francisko, katika mahojiano hayo amebainisha kuwa bila udugu kunazaliwa vita; kinyume chake kila mmoja anapaswa kushiriki katika kupanda udugu, ukaribu, tabasamu na kuunga mkono. Kwa bahati mbaya aliongeza, tuko tunaishi katika vita vipya vya ulimwengu, vita ya tatu katika karne kuzalisha silaha. Sayari nzima iko kwenye vita amesisitiza Baba Mtakatifu, huku akikumbusha migogoro iliyosahauliwa kama vile nchini Siria na Yemen na kwingineko. Na ndiyo maana amesema kuwa haitakiwi kamwe kuacha kufanya kazi kwa ajili ya amani ambayo ni zawadi, ni wito na wakati huo huo ni heri!
Makuhani na vijana wa bara la Asia
Kwa mtazamo huo Baba Mtakatifu, anawaalika makuhani wa Korea daima wawe wahudumu wa amani, hata kwa kwenda katika utume ambapo kuna haja ya kutoa msaada wa kidini. Kutokana na hilo hata Kardinali mteule Lazzaro You Heung-sik, Mwenyekiti Mpya wa Baraza la Kipapa la Makleri ametoa neno kwa kusisitiza kuwa "Papa Francisko kwa hakika anao ukaribu mkubwa na mapadre".
Katika Mchakato wa mahojiano ya Papa, wazo lake lilielekezwa pia kwa vijana wa Kikorea,na kuwashauri wasisahu mizizi yao ili kufanya kuonesha wazi tunu msingi ya uzoefu wa wazee, na kuweza kugeuka kama mti mwema ambao unamwilishwa kutoka katika mizizi na kutoa matunda. "Ni kwa njia hiyo tu itawezakana kutoa maisha katika ulimwengu bora, kwa kutumia ubunifu bila kuchoka kamwe na kuongozwa na moyo mkubwa usio na mipaka", amesisitiza Baba Mtakatifu katika mahojiano hayo.