Mwaka 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V: Msamaha, Huruma na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ilikuwa ni fursa adhimu kwa msamaha na huruma ya Mungu kuwa ni kiini cha tafakari ya maisha na utume wa Kanisa. Hii ni tafakari ambayo inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii inatokana na ukweli kwamba, msamaha na huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na njia muafaka ya uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Imekuwa ni nafasi kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha utandawazi wa ushirika na mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika maisha ya kiroho na kimwili, dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayotenga, nyanyasa na kuwabagua maskini. Kwa sasa tofauti msingi kati ya watu, kimekuwa ni chanzo cha kinzani, migogoro na uhasama. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, kwa kuthamini, utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma kama ulivyofunuliwa na Kristo Yesu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wawe ni wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema, wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa: unyenyekevu, ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu, umoja na mshikamano wa binadamu. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 28 Agosti 2022 anazindua rasmi maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Huruma ya Papa Celestin V, kwa kufungua lango la Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio” Jimbo kuu la Aquila, nchini Italia. Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Dominika ya 22 ya Mwaka C wa Kanisa na baadaye, ataongoza Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio.” Papa Francisko anataka kukazia umuhimu wa Mama Kanisa kuendelea kuwa shuhuda na chombo cha huruma na matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo, ili waonje tena upendo wa Baba wa milele.
Maadhimisho haya yalizinduliwa tarehe 23 na kilele chake ni tarehe 30 Agosti 2022. Kilele cha Mwaka wa 728 wa Huruma ya Papa Celestin V kimekuwa kikiadhimishwa kila mwaka tarehe 28 Agosti, kwa kuwakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuchuchimilia na kuambata amani, kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu. Maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Huruma ya Papa Celestine V, yamepitia katika vitongoji mbalimbali: “Eremo del Morrone, Sulmona na hatimaye Kanisa kuu la L’Aquila. Mada ambazo zimekuwa zikijadiliwa ni pamoja na: Dhana ya Msamaha katika maisha ya mwamini; Dhana ya Kanisa kama chombo cha huruma na matumaini kuanzia kwa Papa Celestine V hadi Baba Mtakatifu Francisko; Uhuru wa watu wa Mungu kukutana katika ukweli na haki na hatimaye ni tema kuhusu Papa Celestin V. Maadhimisho haya yanatoa pia mkazo kwa majadiliano ya kiekumene, haki, amani na msamaha.
Hii ni amani inayopaswa kupata chimbukio lake katika akili na nyoyo za watu. Huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba: vita, chuki, uhasama na ubaya wa moyo ni mambo ambayo hayana msingi kabisa na kwamba, waathirika wakuu ni wale watu wanaofungwa katika hali kama hizi, kwani ni mambo yanayowapokonya utu wao, heshima na haki zao msingi. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Huruma ya Mungu anaendelea kusema Baba Mtakatifu Francisko inawasha moto wa upendo mioyoni mwa watu, kwa kuguswa na mahitaji yao pamoja na kuwashirikisha. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuishi kwa furaha tunu hizi msingi za maisha ya Kikristo.