Papa Francisko: Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni mwaliko kwa watoto wa Kanisa kulitafakari Fumbo hili la imani. Papa Francisko: Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni mwaliko kwa watoto wa Kanisa kulitafakari Fumbo hili la imani. 

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho: Tafakari ya Fumbo la Imani ya Kanisa

Tarehe Mosi, Novemba 1950, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa Kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 10 Agosti 2022, anawaalika waamini kumtafakari Bikira Maria aliyefuatana na Kristo Yesu katika maisha na utume wake, akateseka sana, kiasi cha kudiriki kusimama chini ya Msalaba wa Kristo Yesu na hatimaye, akamfuata kwa kupalizwa mbinguni kwenye utukufu. Huko mbinguni, Bikira Maria anawatazama watoto wake wote kwa upendo wa kimama, mwaliko kwa waamini kumwinulia macho yao Bikira Maria ili aweze kuwaongoza kwenda mbinguni. Kwa mwanga na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, akiwa ameungana na Maaskofu wenzake kutoka sehemu mbalimbali za dunia, Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili ni sehemu ya Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki. Bikira Maria tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili.

Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa Kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos.” Bikira Maria ni Mama yake Kristo Yesu, ambaye ni Mwana wa Baba wa milele, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kweli kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Kanisa linamwita kuwa ni Eva mpya kutokana na utii wake kwa Mwenyezi Mungu. Bikira Maria ni kielelezo cha imani na ishara na utimilifu kamili wa Kanisa. Kumbe, kwa njia ya imani na utii wake thabiti, Bikira Maria akapewa upendeleo wa pekee kuweza kushiriki katika kazi ya ukombozi kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kwa utii wake amekuwa Eva mpya, Mama wa walio hai.

Sherehe ya Kupalizwa Bikira Maria Mbinguni ni mwaliko wa kutafakari fumbo la imani
Sherehe ya Kupalizwa Bikira Maria Mbinguni ni mwaliko wa kutafakari fumbo la imani

Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho kama kielelezo cha kulala usingizi wa amani “Dormitio” na wataalam wengine wakaongeza kusema, “Somnum Mariae”. Mwili wa Bikira Maria uliokuwa umekingwa na dhambi ya asili, ukapalizwa mbinguni. Hiki ni kielelezo makini cha imani ya watu wa Mungu kama alivyokiri Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa, kielelezo makini cha imani ya watu wa Mungu. Utenzi wa Bikira Maria ni kielelezo cha mtazamo mpya kuhusu Mwenyezi Mungu, ni shule ya uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika huruma na upendo wa Mungu. Ni muhtasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni mwaliko kwa watoto wa Kanisa kulitafakari Fumbo hili la imani kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kumwokoa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kristo Yesu aliyezaliwa, akateswa, akafa, akafufuka amepaa na mwili wake wa utukufu, hatima ya maisha ya waamini wote. Kumbe hapa duniani, watu wa Mungu wajibidiishe kumtumikia Mungu: kiroho na kimwili. Ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu alipaa mbinguni kutokana na nguvu za Kimungu zilizokuwa zikitenda kazi ndani mwake. Bikira Maria amepalizwa mbinguni kwa mastahili ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Mama Kanisa anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika watoto wake wote waliotawanyika sehemu mbalimbali za dunia kuimarisha imani yao kwa nguvu ya upendo wa Mungu pamoja na kutambua kwamba, miili yao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Waamini watambue kwamba miili yao ni Mahekalu ya Roho Mtakatifu.
Waamini watambue kwamba miili yao ni Mahekalu ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anatukumbusha kwamba, maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria yanakwenda sanjari na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Bikira Maria, Mama wa Mungu kwa upendeleo na neema ya Mungu akabahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na hivyo kushirikishwa kwa namna ya pekee kabisa katika Fumbo la Pasaka na utukufu wa Kristo Yesu. Hili ni Fumbo linaloonesha historia ya ubinadamu, matumaini ya watu wa Mungu na Kanisa katika ujumla wake. Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho, anaendelea kuliombea Kanisa ambalo bado liko safarini, ili liweze kupata neema ya uzima wa milele. Bikira Maria kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama anaendelea kuwasindikiza watoto wa Kanisa ambao wako bondeni huku kwenye machozi, ili siku moja, waweze kufika mbinguni na kufurahia maisha na uzima wa milele. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni inakita mizizi yake katika imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kielelezo cha ushindi wa nguvu ya upendo wa Mungu kwa waja wake.

Utenzi wa Bikira Maria, “Magnificat” ni mtazamo mpya kuhusu Mwenyezi Mungu na ulimwengu katika ujumla wake. Hii ni shule ya uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani unaowahimiza waamini kujenga na kudumisha utamaduni unaomwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Utenzi huu unatoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu, ambaye ni: Bwana na Mkuu: ni mwingi wa huruma na mapendo; ni mtakatifu na enzi zote ni zake na kwamba, huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi. Huruma yake ni sawa na mto unaoendelea “kurutubisha” historia ya mwanadamu. Ni Mungu ambaye ameutazama unyonge wa mjakazi wake, kiasi cha kumkirimia neema na baraka, mambo ambayo ameyapokea kwa moyo wa unyenyekevu. Ndiyo maana roho yake inamfurahia Mungu mwokozi wake kwa sababu amemuumba, akampenda na kumkomboa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Na kwa njia ya utenzi huu, anataka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo, uzuri na umilele kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni kilele cha furaha yote ya mwanadamu.

Bikira Maria amekingiwa dhambi ya asili na hatimaye kupalizwa mbinguni
Bikira Maria amekingiwa dhambi ya asili na hatimaye kupalizwa mbinguni

Kanisa linapaswa kuunganisha nguvu zake na kushirikiana na watu wenye mapenzi mema ili kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kanisa linapaswa kuwa kweli ni sauti ya kinabii ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Linapaswa kutangaza na kusimamia ukweli, maadili na utu wema, dhidi ya utamaduni wa kifo! Bikira Maria ni shuhuda wa utajiri unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kuwa kweli ni sauti ya kinabii. Kwa hakika, Bikira Maria ni nyota ya uinjilishaji. Kimsingi, “Magnificat” ni muhtasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, chachu makini ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Kanisa halina budi kuwa na ujasiri wa kinabii ili kusimama kidete kulinda, kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Rasilimali na utajiri wa dunia hii vinapaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu katika ujumla wake.

UTENZI WA MAMA BIKIRA MARIA: “Magnificat”: Moyo wangu wamtukuza Bwana, Roho yangu inafurahi* Kwa sababu ya Mungu mwokozi wangu. Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma, Mtumishi wake mdogo, * Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, * Jina lake ni takatifu. Huruma yake kwa watu wanaomcha* Hudumu kizazi hata kizazi. Amefanya mambo makuu kwa mkono wake* Amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi, *Akawakweza wanyenyekevu. Wenye njaa amewashibisha mema, * Matajiri amewaacha waende mikono mitupu. Amempokea Israel mtumishi wake, * Akikumbuka huruma yake, Kama alivyowaahidia wazee wetu, * Abrahamu na uzao wake hata milele. Lk 1:46-55.

Bikira Maria
12 August 2022, 17:06