Tetemeko la Ardhi L'Aquila 2009: Mashuhuda wa Imani na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 28 Agosti 2022 baada ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V, kwa kufungua lango la Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio” Jimbo kuu la L’Aquila, nchini Italia. Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ameonesha matumaini makubwa kwamba, mji wa L’Aquila utaweza kugeuka na kuwa ni mji mkuu wa: msamaha, amani na maridhiano. Baadaye, ameongoza Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio.” Baba Mtakatifu amekutana na kusalimiana na: viongozi wa Serikali na Asasi za kiraia, ndugu, jamaa na marafiki wa wahanga wa tetemeko la ardhi tarehe 6 Aprili 2009 mji wa L’Aquila ulipokumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha watu 309 kupoteza maisha, watu wengine 1,600 kujeruhiwa vibaya na watu 80, 000 wakabaki bila makazi maalum baada ya nyumba zao kubomolewa na kutofaa tena kwa matumizi ya binadamu. Baba Mtakatifu anawapongeza pamoja na kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wote wa Mungu na kwa jinsi walivyosimama kidete, kwa ari na moyo mkuu kushughulikia janga hili la asili ambalo limeacha madonda makubwa katika akili na nyoyo za watu.
Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kuwa ni mashuhuda wa imani: katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala, kwa kutambua kwamba, hapa duniani mwanadamu ni mpita njia. Waswahili wanasema, “Kanyaga pole pole” kumbe, kama waamini wanapaswa kuyaelekeza macho yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, na kwa njia hii, amewakomboa katika dhambi na mauti. Wale wote waliotangulia mbele za haki, wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele kwa sasa wako mbele ya Kristo Yesu, Hakimu mwenye huruma. Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, katika sakafu ya moyo wake, majina ya ndugu, jamaa na marafiki zao waliopoteza maisha kutokana na tetemeko la ardhi la tarehe 6 Aprili 2009 yameandikwa kwa “karamu ya huruma na upendo.” Kifo hakiwezi kufuta kabisa upendo wa Mungu kwa waja wake, ndiyo maana Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake akisali na kusema “Ee Bwana, uzima wa waamini wako hauondolewi ila unageuzwa tu. Nayo makao ya hapa duniani yakisha bomolewa, unawakirimia makao ya milele mbinguni.” Rej. Utangulizi wa wafu.
Katika machungu ya moyo, mambo msingi yanayotakiwa kupewa uzito wa upekee ni: Ushuhuda wa ujirani mwema, urafiki, ili kutembeana na kusaidiana kama ndugu wamoja katika mchakato wa kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazoibuka katika maisha. Baba Mtakatifu anawapongeza watu wa Mungu Jimbo kuu la L’Aquila kwa kujenga na kutunza Kikanisa cha Kumbukumbu kwa unadhifu wa hali ya juu, kwani kumbukumbu ni nguvu ya watu wa Mungu na ikiwa kama nguvu hii inapata mwanga wa imani, inakua ni chombo cha kuwasongesha mbele kwa imani, matumaini na mapendo ya kweli, huku wakiwa wanabeba ndani mwao: historia, amana na mang’amuzi yao ya kale. Mapokeo ya Kikristo na Kitamaduni yamewawezesha kukabiliana na athari za tetemeko la ardhi la mwaka 2009 kwa ujasiri na uvumilivu mkuu, kiasi cha kuweza kusonga mbele hadi wakati huu. Tetemeko la ardhi limeacha athari kubwa katika maisha na vipaumbele vya watu. Kuna ujenzi na ukarabati mkubwa wa makazi ya watu, shule na Makanisa, lakini kipaumbele cha kwanza kiwe ni ujenzi wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kitamaduni, kijamii na Kikanisa; yote yafanyike kwa ari na moyo mkuu unaofumbatwa katika ushirika, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Ujenzi na ukarabati wa mji wa L’Aquila uwe na malengo ya muda mfupi na mrefu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni amana na utajiri wa jamii na kiimani, chachu ya: maisha, imani na matumaini ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kutoa salam maalum kwa wawakilishi wa wafungwa kutoka Abruzzo, kama alama ya matumaini katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu.