Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Vijana wa Medjugorje 2022: Amri Kuu ya Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Siku ya 33 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, nchini Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe 1 hadi 6 Agosto 2022, Sherehe ya Kung’ara Bwana, yananogeshwa na kauli mbiu: “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu. Lakini Kristo Yesu anawaalika watu wote akisema: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.” Mt 11:28-30. Mwaliko wa pekee kwa vijana ni kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu, anayewafahamu fika vijana wa kizazi kipya na yale mambo yanayosumbua nyoyo zao. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 33 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, uliosomwa tarehe 1 Agosti 2022 kwa niaba yake na Askofu mkuu Aldo Cavalli, Msimamizi Kitume wa Parokia ya Medjugorje, aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Novemba 2021. Katika ujumbe wake, Baba Mtakatifu anakazia Amri ya Upendo inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu, ili kufikiri, kuona na kutenda; mtindo wa maisha unaohitaji ujasiri wa kuwa karibu zaidi na Kristo Yesu.
Baba Mtakatifu anasema, hawa ni vijana ambao wanawaka tamaa ya mambo mengi, wanazongwa na majeraha mbalimbali; wanabeba mizigo mizito inayowashinda kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu na uhakika wa maisha; pamoja na wasi wasi mkubwa kwa leo na kesho iliyo bora. Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu anawaalika vijana wa kizazi kipya kumwendea na kujitia nira yake na kuanza kujifunza kutoka kwake. Hii ni changamoto ya kusimama na kuanza kutembea kifua mbele, ili kukabiliana na changamoto, fursa na matatizo yanayoibuka katika maisha ya ujana wao, badala ya kujifungia katika ubinafsi na undani wao! Vijana wanahimizwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu anayewapenda upeo. Vijana watambue ni mahali gani wanapotamani kwenda, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati, ili kutambua malengo sahihi ya maisha, ili wasitumbukie katika mambo ya kufikirika na udanganyifu, yanayowaacha wakielea kwenye “ombwe.” Ni muda wa kumjifunza Kristo Yesu, kutambua na kuthamini Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Nira anayozungumzia Kristo Yesu ni Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani akisema “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi.” Yn 15:12.
Upendo wa dhati ni dawa ya kweli inayoganga na kuponya majeraha ya mwanadamu, kwa kuendelea kumwilisha ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaopata chimbuko lake kutoka katika upendo wa Mungu. Kwa vijana kutembea na Kristo Yesu bega kwa bega, watamwiga na kuendelea kujifunza kutoka kwake, kwani Yeye ni Mwalimu mnyenyekevu, asiyewalazimisha wala kuwatisha mzigo kinyume cha uwezo wao. Kristo Yesu alijifanya maskini na kunyenyekea hadi kifo cha Msalaba. Jambo la msingi ni vijana kujinyenyekesha, kutambua udhaifu wao na kiburi kinacho “wavuruga” kiasi cha kudhani kwamba, wanaweza kufanya mambo yote kwa nguvu zao binafsi bila ya kumtegemea Mwenyezi Mungu. Vijana wajenge utamaduni wa kumsikiliza kwa makini Kristo Yesu, ambaye ni Mwalimu wa maisha, ili kujifunza moyo wake, upendo na njia yake ya kufikiri, kuona na kutenda; mambo ambayo kimsingi anasema Baba Mtakatifu yanahitaji ujasiri kwa kuwa karibu naye, ili kuweza kumuiga. Vijana wajifunze kupiga moyo konde na kumwendea Kristo Yesu, ili kumwelezea yale yote yanayofichama katika undani wa maisha yao, ili wapate raha na amani nafsini mwao.
Bikira Maria, Nyota ya Bahari, ni ishara ya matumaini juu ya bahari ya dunia iliyochafuka kwa mawimbi mazito mazito, atawasaidia na kuwaongoza kuelekea kwenye bandari salama, amani na utulivu wa ndani. Katika kipindi hiki cha likizo ya kiangazi, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kuwa karibu na Kristo Yesu katika: Sala, Neno, Sakramenti na kwa njia ya huduma makini kwa jirani, kwa kutambua kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu. Wajiweke karibu zaidi na Kristo Yesu, ili apate kuwapumzisha. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu amewakabidhi vijana wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili kwa maombezi yake, vijana waweze kujitwika nira ya upendo, upole na unyenyekevu wa Kristo Yesu na kuanza kumfuasa. Kwa kukutana na vijana wengine, wajitahidi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani. Itakumbukwa kwamba, Padre Slavko Barbarić (11 Machi 1946 – 24 Novemba 2000) ndiye muasisi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina.