Papa Francisko asikitishwa sana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Iraq na kuwataka viongozi wakuu kujikita katika majadiliano kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi Papa Francisko asikitishwa sana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Iraq na kuwataka viongozi wakuu kujikita katika majadiliano kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi 

Wito wa Papa Francisko Kwa Iraq: Majadiliano Katika Ukweli na Uwazi

Baba Mtakatifu bado ana kumbukumbu hai ya hija yake ya Kitume nchini Iraq. Alishuhudia amani na utulivu kati ya waamini wa dini na madhehebu mbalimbali nchini Iraq. Anasema, majadiliano katika ukweli, uwazi, na udugu wa kibinadamu ndiyo njia muafaka ya kuweza kufikia malengo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hija yake ya kitume ya 33 kimataifa nchini Iraq ni kati ya hija ambazo zilikuwa hatari sana katika maisha na utume wake. Alitumia muda mrefu kusali na kutafakari. Akapima madhara na faida yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Iraq. Akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuomba ulinzi na usalama kutoka kwa Bikira Maria, Afya ya Warumi, akapiga moyo konde na kuamua kwamba, kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021 angefanya hija ya kitume nchini Iraq kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Baba Mtakatifu akawa ni hujaji wa toba, ili kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha, tayari kuanza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa.

Machafuko ya kidini na kisiasa ni hatari sana nchini Iraq kwa sasa.
Machafuko ya kidini na kisiasa ni hatari sana nchini Iraq kwa sasa.

Baba Mtakatifu akawepo nchini Iraq kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Akapata nafasi ya kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini. Hii ilikuwa ni hija ya kwanza ya kihistoria kuandikwa na Baba Mtakatifu Francisko, kama Khalifa wa kwanza wa Mtakatifu Petro kutembelea Iraq, licha ya changamoto pevu zilizokuwa mbele yake. Huduma ya huruma na upendo kwa watu wa Mungu sanjari na mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu ni mambo msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi anasema Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na wanatasnia ya mawasiliano ya jamii, waliokuwemo kwenye msafara wake kutoka Iraq. Aligusia jinsi alivyokosa maneno kwa kupigwa na bumbuwazi, alipoona na kushuhudia kwa macho yake, jinsi Makanisa yaliyokuwa mazuri ambayo kwa sasa yamebaki kuwa magofu na wala hayafai tena kwa matumizi kama nyumba za Ibada.

Papa Francisko bado anakumbuka hija yake ya kitume nchini Iraq mwaka 2021
Papa Francisko bado anakumbuka hija yake ya kitume nchini Iraq mwaka 2021

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi, Jumatano tarehe 31 Agosti 2022 amesema kwamba, anafuatilia kwa wasi wasi mkubwa matukio ya vurugu, kinzani na uhasama ambayo yamejitokeza nchini Iraq hivi karibuni. Anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia amani wananchi wa Iraq. Baba Mtakatifu, anasema, bado ana kumbukumbu hai ya hija yake ya Kitume nchini Iraq kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2022. Alishuhudia amani na utulivu kati ya waamini wa dini na madhehebu mbalimbali nchini Iraq. Anasema, majadiliano katika ukweli, uwazi, na udugu wa kibinadamu ndiyo njia muafaka ya kuweza kufikia malengo yanayokusudiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Iraq katika ujumla wao.

Wito Iraq
31 August 2022, 15:10