Tafuta

Tamko la Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi lililotolewa tarehe 15 Septemba 2022 Tamko la Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi lililotolewa tarehe 15 Septemba 2022  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Kazakhstan: Tamko la Viongozi Wakuu wa Dini Kwa Mwaka 2022

Tamko la Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani lililotolewa tarehe 15 Septemba 2022 ni muhtasari wa mafundisho makuu ya dini. Tamko linakemea misimamo mikali ya kidini na kiimani; vitendo vya kigaidi; chuki na uhasama, ghasia na kwamba vita havina uhusiano wowote ule na misingi ya imani ya kweli na mambo haya yanapaswa kupingwa kwa nguvu zote! AMANI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi limeadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Hii ilikuwa ni hija ya 38 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa, lengo ni kuendelea kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Tamko la Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi lililotolewa tarehe 15 Septemba 2022 ni muhtasari wa mafundisho makuu ya dini mbalimbali duniani. Tamko linakemea kwa nguvu zote misimamo mikali ya kidini na kiimani; vitendo vya kigaidi; chuki na uhasama, ghasia na kwamba vita havina uhusiano wowote ule na misingi ya imani ya kweli na mambo haya yanapaswa kupingwa kwa nguvu zote. Mwenyezi Mungu aliwaumba watu wote kwa mfano na sura yake, katika usawa.

Viongozi wa kidini wanao wajibu na dhamana ya kudumisha amani
Viongozi wa kidini wanao wajibu na dhamana ya kudumisha amani

Viongozi wakuu wa dini duniani na dini za jadi wakiwa wanaongozwa na: Mshikamano, haki, usalama na ustawi wa wengi wanapenda kukazia tunu msingi za maisha ya kiroho zinazoratibiwa na kanuni maadili na utu wema, ili kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii yanayopania pamoja na mambo mengine: kuvunjilia mbali tabia ya kukosa maridhiano, hofu ya wageni, ubaguzi, kinzani na mipasuko ya kidini, kijamii, kikabila na kitamaduni. Viongozi wa kidini wanakazia amana na utajiri unaobubujika kutoka katika dini na tamaduni mbalimbali hata katika tofauti zao msingi kama sehemu ya ustaarabu wa mwanadamu, na sehemu ya ujenzi wa haki jamii na mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Elimu ya dini na elimu katika ujumla wake ni muhimu sana katika mustakabali wa maendeleo binafsi na kwa kuheshimu dini na tamaduni za watu. Wanatambua mchango na dhamana ya wanawake katika familia na jamii katika ujumla wake hasa katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya sanjari na maendeleo ya kijamii na kisiasa. Uchu wa mali na madaraka ni chanzo kikuu cha ukosefu wa usawa, kinzani, mipasuko ya kijamii pamoja na ukosefu wa maridhiano ndani ya jamii.

Kumbe, kuna haja ya kujidhatiti kikamilifu katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza Kimataifa kutokana na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Uhalifu wa Kimataifa na vitendo vya kigaidi; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; uhamiaji haramu, athari za mabadiliko ya tabianchi, umaskini na baa la njaa duniani. Viongozi wa kidini kwa nguvu zote wanalaani: Misimamo mikali ya kidini na vitendo vya kigaidi vinavyosigina: maisha ya binadamu, utu, heshima, haki msingi, amani na usalama wa raia na mali zao. Wanalaani wale wote wanaochochea machafuko na kinzani sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanahitaji kupatiwa ulinzi na usalama pamoja na misaada ya hali na mali. Viongozi wa dini wanapania kusaidia mchakato wa kuunda mazingira yatakayokoleza upatanisho na majadiliano katika ukweli na uwazi kwa pande zile zinazopingana na kwamba, kuna haja kwa viongozi wa kidini kusaidia mchakato wa upatanisho, kwa kukoleza majadiliano ya kidini, kitamaduni na kistaarabu katika ngazi mbalimbali ya maisha ya mwanadamu. Kumbe, kuna haja ya kujenga mahusiano na mafungamano baada ya changamoto zilizosababishwa na UVIKO-19. Viongozi wa kidini wanataka kuwa ni jukwaa la majadiliano linalowawakilisha waamini wa dini, madhehebu na imani mbalimbali duniani, ili kunogesha mafungamano ya kiimani, kidini na kitamaduni kwa njia ya majadiliano.

Mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa na Waathirika wa UVIKO-19
Mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa na Waathirika wa UVIKO-19

Viongozi wakuu wa dini duniani na dini za jadi kwa pamoja wanatamka kwamba, wataendelea kutekeleza wajibu wao ili kutafuta na kudumisha misingi ya amani na majadiliano baina ya dini, tamaduni na staarabu mbalimbali sanjari na kuendeleza misingi ya amani na ushirikiano kwa kukoleza tunu msingi za maisha ya kiroho na kimaadili. Magonjwa ya mlipuko ni hatari kwa Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, madhara yake ni makubwa, kumbe, kuna haja ya kushikamana na kusaidiana, ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza. Vita na kinzani sehemu mbalimbali za dunia zinaharibu mfumo wa mahusiano ya Kimataifa. Misimamo mikali ya kidini, vitendo vya kigaidi na vita ni mambo ambayo kamwe hayana uhusiano na dini ya kweli na kwamba, yanapaswa kupingwa kwa nguvu zote. Jumuiya ya Kimataifa isaidie jamii na jumuiya ambazo zimeathirika sana na vitendo vya kigaidi duniani, vita na machafuko. Huu ni wakati muafaka kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanasitisha vita, kinzani na mipasuko sehemu mbalimbali za dunia, kwa kujikita katika majadiliano, urafiki wa kijamii, mshikamano na maridhiano. Tofauti msingi kati ya watu hazina budi kuheshimiwa na kuthaminiwa, ili kujenga na kudumisha mafungamano na mahusiano ya kijamii, udugu wa kibinadamu; haki na mshikamano kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

Mshikamano wa udugu wa kibinadamu upewe msukumo wa pekee na Jumuiya ya Kimataifa. Viongozi wa kidini wanatambua na kuthamini “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu” kuwa ni mwongozo wa ujenzi wa amani na maridhiano; na msingi wa waamini kuheshimiana na kuthaminiana. Wanatambua na kukiri umuhimu wa Tamko la Makka lililopitishwa na Umoja wa Dini ya Kiislam Duniani, “Muslim World Leage” la Mwezi Mei 2019, huko Mecca, linalohimiza: Majadiliano ya kidini, maelewano, ushirikiano, ustawi na mafao ya wengi. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yazingatie pia tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Umaskini uvaliwe njuga ili kuboresha hali ya maisha ya watu, ili wasitumbukie katika misimamo mikali ya kidini na kiimani sanjari na kujikita katika mgawanyo sawa wa rasilimali za dunia; diplomasia ya Kimataifa, usawa, utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Vitendo vya kigaidi vinapaswa kulaaniwa na wote bila ya kupepesa pepesa macho. Usawa wa kijinsia ni muhimu katika kukuza haki msingi za binadamu; utu, heshima na usawa na kwamba, wanawake wanapaswa kuwezeshwa sanjari na maboresho ya maisha ya kifamilia na kijamii. Kuna haja pia kwa Jumuiya ya Kimataifa kuboresha mfumo wa maendeleo ya kidigitali, ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na maendeleo haya makubwa.

Watu wengi zaidi wanufaike na maendeleo ya sayansi na teknolojia
Watu wengi zaidi wanufaike na maendeleo ya sayansi na teknolojia

Tunu msingi za maisha ya kiroho, elimu ya dini, amani na maridhiano ya kidini ni muhimu sana kwa watu wote wa Mungu. Waamini wote wajitahidi kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, sanjari na kuwasaidia wale wote wanaoendelea kuathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Mshikamano wa udugu wa kibinadamu unapaswa kuoneshwa hasa kwa wale walioathirika zaidi na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ni matumaini ya viongozi wakuu wa dini duniani na dini za jadi kwamba, Tamko hili linakuwa ni Mwongozo kwa ajili ya kuragibisha utamaduni wa maridhiano; haki na amani na kwamba, unaweza kutumiwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Sekretarieti kuu imeagizwa kuibua dhana itakayofanyiwa kazi katika Jukwaa la majadiliano ya kidini katika kipindi cha miaka 10 yaani kuanzia mwaka 2023 -2032. Wanaipongeza sana Serikali ya Kazakhstan kwa kuonesha nguvu na utashi wa kuwa ni kituo cha Kimataifa cha mwingiliano wa tamaduni, majadiliano ya kidini na kiimani. Serikali imejitahidi sana kufanikisha Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi mjini Kaza, Nur Sultan, Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022, mchango mkubwa katika mchakato wa maendeleo, amani na utulivu. Kongamano la Nane la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi litaadhimishwa mwaka 2025 mjini Kaza, Nur Sultan, nchini Kazakhstan.

Tamko Viongozi wa Kidini
21 September 2022, 13:54