Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Kazakhstan: Kiu ya Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Alhamisi tarehe 15 Septemba 2022 Baba Mtakatifu Francisko anakutana na kuzungumza kwa faragha na Wayesuit wanaoishi na kufanya utume wao nchini Kazakhstan. Anatarajia kukutana na kuzungumza na watu wa Mungu nchini humo kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Msaada wa Daima. Alasiri, anashiriki na kutoa hotuba ya mwisho wakati Wajumbe watakapokuwa wanatoa Tamko la Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi mjini Kaza, Nur Sultan. Baadaye ataondoka na kurejea mjini Roma majira ya saa 2: 15 Usiku. Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Sikukuu ya Kutukuzwa kwa Msalaba, iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Milicia, amewashukuru watu wote wa Mungu nchini Kazakhstan, kwa kushiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu pamoja na maandalizi yote hadi wakati huo anapohitimisha siku kwa Ibada ya Misa Takatifu.
Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea waamini waliotoka nchi mbalimbali ili kuhudhuria maadhimisho haya. Amewakumbuka na kuwabariki wagonjwa, wazee, watoto na vijana. Katika Sikukuu ya Kutukuzwa kwa Msalaba amesema, waamini wote wameungana kiroho na wale waliokuwa wanasali kwenye Madhabahu ya Bikira Maria, Malkia wa Amani huko Oziornoje. Msalaba ni shukrani ya watu wa Mungu kutoka Kazakhstan. Baba Mtakatifu amewashukuru watu wa Mungu nchini Kazakhstan kwa kujikita kuendeleza mchakato wa majadiliano na amani ambayo ulimwengu unaonesha kiu kubwa Baba Mtakatifu amewakumbuka watu wanaoteseka kutokana na vita sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee Ukraine. Kamwe vita isizoeleke miongoni mwa watu wa Jumuiya ya Kimataifa.
Waathirika wapewe msaada na jitihada zaidi ziwekwe ili kuendeleza amani. Majadiliano katika ukweli na uwazi ni njia ya pekee kuweza kufikia amani. Watu waendelee kujifunza namna ya kutafuta amani na kamwe wasikimbilie na kujikita katika mashindano ya kutenegeneza na kulimbikiza silaha. Wawe na ujasiri wa kutumia rasilimali inayotumika katika vita kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, ili kunogesha umoja na amani. Wakati huo huo, Askofu mkuu Tomash Bernard Peta wa Jimbo kuu la “Maria Santissima in Astana,” Kazakhstan, kwa niaba ya watu wa Mungu Kazakhstan na Asia ya Kati, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu na mahubiri, amemwomba aibariki nchi yao na walimwengu wote ili waweze kuishi kwa amani na umoja. Baraka zake ziwasaidie watu wa Mungu kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani na umoja.