Tafuta

Papa Francisko katika Sikukuu ya B. Maria Mama wa Mateso, amekutana na kuzungumza na Wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na wafanyakazi wa shughuli za kichungaji nchini Kazakhstan. Papa Francisko katika Sikukuu ya B. Maria Mama wa Mateso, amekutana na kuzungumza na Wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na wafanyakazi wa shughuli za kichungaji nchini Kazakhstan.  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Kazakhstan: Kumbukumbu!

Papa: Kumbukumbu inayochota amana yake katika Ekaristi Takatifu, nguvu inayowabidiisha kupenda. Watambue wamerithishwa imani kwa njia ya ushuhuda katika mwanga na tunu za Kiinjili. Hii ni imani inayopyaishwa kwa kujikita katika Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katika maisha na utume wao, watambue kwamba, wanamhitaji Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi limeadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022, na kunogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Itakumbukwa kwamba, hii ni hija ya 38 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa, lengo ni kuendelea kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 15 Septemba, 2022, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Msaada wa daima, Sikukuu ya Bikira Maria Mama wa Mateso, amekutana na kuzungumza na Wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na wafanyakazi wa shughuli za kichungaji nchini Kazakhstan. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia mambo yafuatayo: Kumbukumbu inayochota amana na utajiri wake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, nguvu inayowabidiisha kupenda. Watambue kwamba, wamerithishwa imani kwa njia ya ushuhuda wa maisha katika mwanga na tunu za Kiinjili.

Hii ni imani inayopaswa kupyaishwa daima kwa kujikita katika Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katika maisha na utume wao, watambue kwamba, wanamhitaji Mwenyezi Mungu. Waendelee kuimarisha udugu wa kibinadamu na kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa amani; warithi wa utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu amewahakikishia uwepo wake wa daima katika maisha na utume wao. Kanisa la Asia ya Kati lina utajiri mkubwa wa historia na Mapokeo na linaundwa na watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia na wote wanafanyika kuwa ni familia moja ya watu watakatifu wa Mungu na wala hakuna “mgeni”, “mtu wa kuja” wala “mnyamahanga.” Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake, amependa kuwafunulia wote hawa Fumbo la maisha yake. Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa anasema kwamba, yeye ni mwakilishi wa siri yake Kristo Yesu “ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.” Baba Mtakatifu Francisko amekita tafakari yake katika Kanisa linalo safari kati ya kumbukumbu na yale yajayo. Amewashukuru na kuwapongeza wamisionari wote wanaojisadaka hata baadhi yao wakayamimina maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia mwanga wa Injili ya Kristo Yesu.

Papa Francisko amepata nafasi ya kukutana na watu wa Mungu Kazakhstan
Papa Francisko amepata nafasi ya kukutana na watu wa Mungu Kazakhstan

Hapa ni mahali ambapo mchakato wa majadiliano ya kiekumene hauna budi kuendelezwa pamoja na kuendelea kuwakumbuka kwa dhati kabisa waliojisadaka kwa ajili ya Injili ya Kristo na kwa njia ya watu hawa, Mwenyezi Mungu ametenda mambo makuu katika historia ya maisha ya mwanadamu. Ni watu waliopitia magumu; walikuwa na karama lakini pia na mapungufu yao ya kibinadamu. Waamini wanapaswa kuyaangalia yaliyopita kwa moyo wa shukrani na hivyo kusonga mbele kwa moyo wa shukrani kwa yale ambayo Mwenyezi Mungu ametenda katika maisha yao na kila siku iwe ni siku ya neema, kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kama ilivyokuwa kwa wale wanawake watakatifu pamoja na wanafunzi wa Emau waliobahatika kuandamana na Kristo Yesu katika safari yao ya matumaini ya Kikristo bila kumtambua kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Lakini, wakamtambua Kristo Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza. Kwa kukutana na Kristo Mfufuka, wakapata nguvu ya kumtangaza na kumshuhudia kuwa kweli amefufuka. Ekaristi Takatifu ni nguvu ya upendo inayowabidiisha waamini kupenda kwa dhati na kuishi kikamilifu kumbukumbu ya imani, ibada na shughuli zao za kitume. Vinginevyo, bila kumbukumbu hai, mambo mengi yataweza kutoweka kama “ndoto ya mchana” na hivyo furaha na moyo wa shukrani kuanza kunyauka pole pole kama nyasi za kondeni.

Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu watambue ukuu na utakatifu wa Daraja Takatifu ya Upadre ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu. Waamini wajenge na kudumisha utamaduni wa shukrani kwa wale wote waliowarithisha imani. Hii ni imani inayorithishwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha katika mwanga wa Injili. Kamwe watu wa Mungu wasichoke kutangaza na kushuhudia imani yao, huku wakiendelea kuipyaisha na kukutana na Kristo Yesu. Watu wanataka kuona na kushuhudia upya wa Injili hai, inayowapatia matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Licha ya udhaifu na mapungufu ya waamini, lakini, daima Kristo yuko pamoja na kati ya wafuasi, ili kwa pamoja waweze kulijenga Kanisa. Kuna changamoto nyingi katika maisha ya imani mfano vijana na changamoto zao za ujana; sheria, kanuni na taratibu zinazodhibiti uhuru wa kidini. Lakini pamoja na yote haya, waendelee kujikita katika Heri za Mlimani ambazo ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu. “Heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Mt 5:3. Watu watakatifu wa Mungu wanapaswa kujinyenyekesha na kwamba, hii ni neema ya Mungu inayopaswa kuwawezesha kuzama zaidi katika huduma kwa jamii, wakati wa raha na shida. Waamini watambue kwamba, kamwe hawawezi kujitosheleza, kwani wanamhitaji Mwenyezi Mungu katika maisha na utume wao, ili kunogesha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Jumuiya ya waamini wa Kanisa Katoliki hata katika uchache wao inapaswa kuwa ni shuhuda wa imani na upendo kwa Mungu na jirani zao. Wajitahidi kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Wawe ni mashuhuda wa haki na ukweli; wasimame kidete kupinga rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma.

Papa Francisko anwataka waamini wawe ni mashuhuda wa haki na ukweli
Papa Francisko anwataka waamini wawe ni mashuhuda wa haki na ukweli

Jumuiya za Kikristo, Nyumba za Malezi na Seminari ziwe ni shule za: ukweli na uwazi na mahali pa kushirikishana tunu msingi za Kiinjili; kwa kutambua na kuthamini utu, heshima na usawa kwa wote. Huu ni usawa unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, hivyo kila mmoja wao azame na hatimaye, aweze kukumbatia Injili ya Kristo Yesu. Wakristo wajenge umoja unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Tunu msingi za Kiinjili ziwasaidie kuboresha maisha yao ili kuondokana na uchoyo na ubinafsi, tayari kujisadaka katika kupendo pasi na masharti. Wakristo wawe ni mashuhuda na vyombo vya ushirika na amani, tayari kusoma alama za nyakati ili kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Fumbo la Msalaba lilikuwa ni chemchemi ya nguvu, imani na matumaini kwa Wenyeheri: Padre Władysław Bukowiński, aliyefariki dunia tarehe 3 Desemba 1974 wakati wa madhulumu dhidi ya Kanisa. Mwenyeheri Alessio Zaryckyj (1912-1963), Mwenyeheri Askofu Mykyta Budka. Hawa ni mashuhuda wa imani walioadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ibada na uchaji; lakini chemchemi ya utakatifu wao ni huduma na ujirani mwema kwa watu wa Mungu na kwamba, hata waamini nao wanapaswa kutambua kwamba, ni wao pia ni warithi wa utakatifu wa maisha. Huu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu kuzingatia urithi wa imani na kuendelea kuutolea ushuhuda. Baba Mtakatifu ataendelea kuwasindikiza katika maisha na utume wao kwa njia ya sala na sadaka yake ya daima.

Imani inarithishwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha
Imani inarithishwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha

Askofu José Luis Mumbiela Sierra wa Jimbo la “Santissima Trinità in Almaty” nchini Kazakhstan, katika salam zake kwa Baba Mtakatifu Francisko, amemkaribisha ili kuzungumza na vyombo na mashuhuda wa amani na umoja, wanaojizatiti katika ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu hata katika changamoto za kiafya anazokabiliana nazo kwa sasa, kamwe asiache kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa watu wa Mataifa. Mama Kanisa anamshukuru na kumtukuza Mungu kwa zawadi ya mashuhuda na wafiadini walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu amesikiliza pia shuhuda kutoka kwa waamini walei, walioelezea kuhusu: changamoto, fursa na matatizo wanayokumbana nayo katika maisha ya familia na ndoa, hasa kwa zile familia ambazo wazazi wametengana na kusambaratika, malezi na makuzi ya watoto yanakuwa na mwelekeo tenge sana. Kishawishi kikubwa kwa watu wa ndoa na familiani: uchu wa fedha na mali; madaraka pamoja na tamaa za mwili. Changamoto hizi zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu na maisha adili.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa amani na umoja
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa amani na umoja

Watawa wanamshukuru Mungu kwa kuwakirimia zawadi ya maisha ya kuwekwa wakfu, sasa wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao; upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Watu watakatifu wa Mungu nchini Kazakhstan wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kujipambanua kama shuhuda na mjumbe wa amani, majadiliano, huruma na upendo wa Mungu. Uwepo wake kati yao ni ushuhuda wa nguvu na kamwe hautaweza kufutika katika sakafu ya nyoyo zao. Mapadre kwa namna ya pekee kabisa, wanaitwa na kutumwa kuwa kusali na kuwasindikiza watu wa Mungu; kuwaonesha huruma na mapendo; kuwasikiliza na kuwasaidia kadiri ya uwezo wao. Watu wa Mungu wanahitaji uwepo wa Mapadre kwa ajili ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Huduma ya upendo! Jambo la msingi ni kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na matumaini kwa watu wa Mungu nchini Kazakhstan.

Watu wa Mungu
15 September 2022, 15:01