Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 15 Septemba 2022 amepata fursa tena ya kutoa hotuba ya kufunga Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 15 Septemba 2022 amepata fursa tena ya kutoa hotuba ya kufunga Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Kazakhstan: Hotuba ya Kufunga Kongamano! Amani

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amejikita katika mambo makuu yanayofungamanishwa na amani na umoja; Tamko la Kongamano linalobeba muhtasari wa mafundisho makuu ya dini duniani; uhuru wa kidini; utu, heshima na haki msingi za binadamu; Ujenzi wa udugu wa kibinadamu; amani, wanawake na kwamba, vijana ni mashuhuda na vyombo vya amani na umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi limekuwa likiadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Hii ni hija ya 38 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa, lengo ni kuendelea kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Jumatano, tarehe 14 Septemba 2022 alipata fursa ya kutoa hotuba ya ufunguzi wa Kongamano hili lililofunguliwa kwa sala ya ukimya na kukazia kuhusu: Utambulisho na thamani ya uhai wa mwanadamu; athari za misimamo mikali ya kidini na kiimani; Uhuru wa kidini na changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa: UVIKO-19, Amani, Udugu wa Kibinadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 15 Septemba 2022 amepata fursa tena ya kutoa hotuba ya kufunga Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi. Katika hotuba yake amejikita katika mambo makuu yanayofungamanishwa na amani na umoja; Tamko la Kongamano linalobeba muhtasari wa mafundisho makuu ya dini duniani; uhuru wa kidini; utu, heshima na haki msingi za binadamu; Ujenzi wa udugu wa kibinadamu; amani, wanawake na kwamba, vijana ni mashuhuda na vyombo vya amani na umoja. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza viongozi wa dini mbalimbali duniani katika mchakato wa ujenzi wa amani na umoja. Itakumbukwa kwamba, Kongamano la Kwanza la Viongozi wa Dini Duniani liliadhimishwa kunako Januari 2002 mjini Assisi, Italia, kwa mwaliko wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Lengo lilikuwa ni kuendelea kuimarisha mchango wa dini mbalimbali katika kukuza: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa njia ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Hii ni kutokana na kinzani kubwa zilizoibuka miongoni mwa waamini wa dini mbalimbali duniani, baada ya shambulizi la kigaidi lililofanyika nchini Marekani tarehe 11 Septemba 2001.

Vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa amani na umoja
Vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa amani na umoja

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kulikuwa na hofu ya kugeuza dini kuwa ni vitalu vya kukuzia misimamo mikali ya kidini na kiimani, udini na ukabila. Lakini Kongamano hili limeonesha kiini cha dini mbalimbali duniani kwa kuwakutanisha viongozi wa dini mbalimbali nchini Kazakhstan. Tamko la Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi lililotolewa tarehe 15 Septemba 2022 ni muhtasari wa mafundisho makuu ya dini mbalimbali duniani. Tamko linakemea kwa nguvu zote misimamo mikali ya kidini na kiimani; vitendo vya kigaidi; chuki na uhasama, ghasia na kwamba vita havina uhusiano wowote ule na misingi ya imani ya kweli na mambo haya yanapaswa kupingwa kwa nguvu zote. Mwenyezi Mungu aliwaumba watu wote kwa mfano na sura yake, katika usawa. Kumbe, imani, kabila, mahali anapotoka mtu ni mambo yanayopaswa kuheshimiwa na kuwa ni sehemu muhimu sana ya mafundisho ya kidini. Hivyo basi, kuna haja kutofautisha kati ya masuala ya Serikali na Kidini; lakini kwa kutambua kuwa, haya pia ni mambo yanayoingiliana. Watu wasibaguliwe na kutweza kwa sababu ya imani yao. Hapa kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu; mambo ambayo yamekuwa ni sababu msingi ya vita na mashambulizi ya kigaidi.

Viongozi wa dini duniani wanasema, wanataka kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini katika matumaini ya uzuri wa mbinguni. Mama Kanisa anatangaza na kushuhudia kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; anakiri katika dhana ya umoja wa Familia ya watu wa Mungu duniani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema, “Maana, watu wote ni jumuiya moja tu. Wenyewe, asili yao ni moja, kwa sababu Mungu aliwaweka wote wakae juu ya uso nchi yote; tena wao wanacho kikomo kimoja tu, yaani Mungu, ambaye maongozi yake, ushuhuda wa wema wake, na azimio lake la wokovu yawaelekea watu wote.” Nostra aetate, 1. Ni katika muktadha huu, Vatican imeendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kwa ajili ya kutafuta na kudumisha amani duniani. Majadiliano ya kidini ni chombo muhimu sana cha huuduma kwa binadamu katika muktadha wa kushukuru na kumtukuza Mungu kwa utukufu wake wote.

Tamko la Viongozi wa Kidini ni Muhtasari wa Mafundisho makuu ya kidini.
Tamko la Viongozi wa Kidini ni Muhtasari wa Mafundisho makuu ya kidini.

Miaka 21 iliyopita, Mtakatifu Yohane Paulo II katika hija yake ya Kitume nchini Kazakhstan alikazia umuhimu wa Kanisa kumwongoza mwanadamu na kwamba, hii pia ndiyo njia kwa dini mbalimbali duniani. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hayana budi kupewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, maamuzi yazingatie kikamilifu katika misingi hii. Binadamu na familia katika ujumla wake ni kiota cha upendo kinachopaswa kulindwa na kuendelezwa. Mapokeo, amana na utajiri mkubwa wa dini mbalimbali duniani unajikita katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na ujirani mwema. Uaminifu kwa Mwenyezi Mungu unakwenda sanjari na upendo kwa viumbe walioumbwa kwa sura na mfano wake. Katika hitimisho la hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu wa kutafuta, kuilindia na kutunza amani, dhidi ya vita na tabia ya kutaka kupimana nguvu. Amani ya kweli ni matunda ya udugu wa kibinadamu.

Papa Francisko Mjumbe wa amani na umoja
Papa Francisko Mjumbe wa amani na umoja

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, amani si kutokuwepo kwa vita, wala haiwezi kupunguzwa kuwa ni tendo la kudumisha uwiano kati ya nguvu zinazopingana. Tena amani si tu matokeo ya utawala wa mabavu, bali inaitwa kwa usahihi kamili “Kazi ya Haki.” Gaudium spes, 78. Amani ni chemchemi ya udugu wa kibinadamu, haki, usawa na maridhiano. Hii ni changamoto kwa walimwengu kusimama kidete kutafuta, kulinda na kujenga amani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si kuwasababishia binadamu maafa na majanga katika maisha. Wajenzi wa amani watakumbukwa daima katika historia ya mwanadamu. Wanawake wajengewe uwezo wa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani duniani; kwa kudumisha usawa, kwa kupewa madaraka na kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa kutoa maamuzi. Viongozi wa kidini wanadhamiria kusimama kidete kuona kwamba, wanawake wanaheshimiwa, wanatambuliwa na kuhusishwa kikamilifu. Vijana ni vyombo na mashuhuda wa amani na wanahamasishwa kuwa ni walinzi na watunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Vijana wapewe elimu makini kuhusu amani; wapewe fursa ya kusoma na wala si kubebeshwa silaha na kupelekwa mstari wa mbele. Vijana waheshimiwe na kusikilizwa kwa makini na kwamba mchakato wa ujenzi wa ulimwengu mamboleo uwahusishe vijana wa kizazi kipya.

Papa Hotuba ya Kufunga
15 September 2022, 15:53