Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Jumatano, tarehe 14 Septemba 2022 amepata fursa ya kutoa hotuba ya ufunguzi wa Kongamano hili Baba Mtakatifu Francisko Jumatano, tarehe 14 Septemba 2022 amepata fursa ya kutoa hotuba ya ufunguzi wa Kongamano hili  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Kazakhstan: UVIKO-19, Amani, Udugu na Mazingira

Papa Francisko, tarehe 14 Septemba 2022 amepata fursa ya kutoa hotuba ya ufunguzi wa Kongamano hili lililofunguliwa kwa sala ya ukimya na Baba Mtakatifu amekazia kuhusu: Thamani ya uhai, athari za misimamo mikali ya kidini, Uhuru wa kidini pamoja na changamoto za Kimataifa:UVIKO-19, Amani, Udugu wa Kibinadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi linaadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022, linanogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Hii ni hija ya 38 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa, lengo ni kuendelea kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Jumatano, tarehe 14 Septemba 2022 amepata fursa ya kutoa hotuba ya ufunguzi wa Kongamano hili lililofunguliwa kwa sala ya ukimya na Baba Mtakatifu amekazia kuhusu: Utambulisho na thamani ya uhai wa mwanadamu; athari za misimamo mikali ya kidini na kiimani; Uhuru wa kidini na changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa: UVIKO-19, Amani, Udugu wa Kibinadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wote waliohudhuria mkutano huu na kwamba, wote wanaunganishwa na kifungo cha udugu wa kibinadamu unaopaswa kusimikwa katika misingi ya: kuheshimiana, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kuendelea kushikamana kama ndugu wamoja.

Umoja na mshikamano ni muhimu katika kukabiliana na changamoto mamboleo.
Umoja na mshikamano ni muhimu katika kukabiliana na changamoto mamboleo.

Hii ndiyo kazi kubwa ambayo nchi ya Kazakhastan imekuwa ikitekeleza. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha uhai wa binadamu, kwa kutambua na kuthamini uzuri wake na kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kumbe, wanao wajibu wa kuzama katika undani wa maisha, daima wakitambua kwamba, hapa duniani ni wasafiri, hivyo wanapaswa kuyainua macho yao mbinguni, ili kuziwezesha roho na akili kuendelea kuwa hai. Misimamo mikali ya kidini na kiimani inahatarisha uhuru wa kuabudu na kumtukuza Mungu na wala wongofu wa shuruti hauna mvuto wala mashiko. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba, binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine.

Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuheshimiana, kwa kuishi kwa amani na utulivu, bila kuathiriwa na tofauti za kikabila na kidini, ili kuheshimu umoja unaofumbatwa na unaosimikwa katika tofauti. Ni kwa njia hii, watu wataweza kutambua umuhimu wa dini katika ulimwengu wa kisasa. Viongozi wa kidini wanao mchango mkubwa katika maisha ya kijamii, ustawi na maendeleo ya wengi baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Gonjwa hili ni kati ya changamoto kubwa zinazoiandama Jumuiya Kimataifa na kwamba, inaweza kushughulikiwa kikamilifu ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itakuwa imeungana, kwani binadamu wote wamepanda mtumbwi mmoja kwa sasa, watu wote wanahitajiana na kukamilishana na wala hakuna mtu anayeweza kujigamba kwamba, anaweza kujitosheleza. Jambo la msingi ni kukuza na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kwamba, dini zinapaswa kuwa ni kikolezo cha umoja ili kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kumwandama mwanadamu.

Changamoto za Jumuiya ya Kimataifa: UVIKO-19, Udugu, Amani na Mazingira
Changamoto za Jumuiya ya Kimataifa: UVIKO-19, Udugu, Amani na Mazingira

Walimwengu wakumbuke kwamba, haitoshi kuwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi na sayansi; wala kishawishi cha kutaka kupata faida kubwa kwa mateso ya maskini na wanyonge, changamoto na uzoefu uliojitokeza wakati wa maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 uwasaidie walimwengu kuwa wanyenyekevu, kwa kusaidiana, ili kujenga umoja na udugu wa kibinadamu unaovuka mipaka ya ukabila, utaifa na udini. Viongozi wa kidini wasaidie kuunda dhamiri nyofu; kwa kuonesha mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, mshikamano wa kidugu ni dawa inayoponya majeraha ya kijamii. UVIKO-19 umewatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato na hivyo kusababisha ukosefu wa haki jamii, hali inayochochewa pia na vitendo vya kigaidi; chuki na uhasama. Baba Mtakatifu Francisko anasema, amani ni kati ya changamoto pevu kwa waamini wa dini mbalimbali duniani. Kumbe, kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kidini yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu Muumbaji na hivyo kuanza kujibidiisha katika kulinda uhai wa binadamu na kuondokana na tabia za chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani, ambayo imekuwa ni chanzo cha maafa katika maisha ya binadamu.

Papa Francisko amekutana na kuzungumza na viongozi wa kidini
Papa Francisko amekutana na kuzungumza na viongozi wa kidini

Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya uhai na haki. Kamwe mambo matakatifu yasitumike kwa ajili ya baadhi ya watu kutaka kutawala kwa nguvu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni amani ya watu wake. Ni katika muktadha huu, kuna haja kwa waamini wa dini mbalimbali kujenga utamaduni wa kukutana, kujadiliana katika ukweli, uwazi na uvumilivu, kwa matumaini ya amani kuweza kuchipua na hatimaye kutamalaki. Watu wajitahidi kufahamiana, ili waweze kuthaminiana zaidi. Baba Mtakatifu anasema, changamoto ya tatu ni udugu wa kibinadamu, unaowawezesha watu wote kutambua na kuthamini utakatifu wa maisha ya kila mwanadamu, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni mchango mkubwa unaopaswa kutolewa na dini mbalimbali duniani, ili kuwakumbusha walimwengu kwamba, wote ni ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi. Leo hii kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linalosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, umaskini pamoja na watu kutafuta fursa za kuboresha maisha yao kutoka katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Hawa ni watu wanaokumbana na changamoto kubwa njiani, lakini kwa bahati mbaya si sehemu ya habari, na wakati mwingine, wamekuwa wakitendewa kinyume cha haki msingi za binadamu. Binadamu wakumbuke hapa duniani ni wapita njia na wala hawana makazi ya kudumu, kumbe, wanapaswa kusumbukiana kama kielelezo cha utu wema.

Utunzaji wa mazingira ni sehemu ya haki jamii kwa walimwengu
Utunzaji wa mazingira ni sehemu ya haki jamii kwa walimwengu

Changamoto ya nne Kimataifa ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili kudhibiti athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi; kwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote ambayo kimsingi ni sehemu ya Kazi ya Uumbaji. Uchafuzi na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wataalam wanasema, kuna uhusiano na mwingiliano mkubwa kati ya uharibifu na uchafuzi wa mazingira pamoja na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kumbe, kuna haja ya kujifunga kibwebwe kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Watu wafikiri na kutenda katika ukweli na haki, ili kuondoa tabia ya kudhaniana vibaya; ili hatimaye, kujenga urafiki wa kijamii, unaowawezesha watu kujenga utamaduni wa kuwakutanisha watu, mng’ao wa Mwanga wa Mungu wetu. Baada ya ufunguzi wa Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi, Baba Mtakatifu Francisko amepata bahati ya kukutana na kuzungumza na wajumbe kutoka nchini Kazakhstan; Misri, Israeli, Wajumbe wa Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, “The Lutheran World Federation” (LWF). Wajumbe kutoka Urussi, Yerusalemu pamoja na Mheshimiwa Miguel Moratinos, Mwakilishi mkuu wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, UN.

Kongamano Ufunguzi

 

14 September 2022, 15:41