Hija ya Kitume ya Papa Francisko Kazakhstan: Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba! Ushuhuda
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu umefunuliwa kwa njia ya Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Ni katika muktadha huu, Msalaba unakuwa ni kitabu cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Katika maisha na utume wa Kanisa, Wakristo wa nyakati mbalimbali wamesoma na kulitafakari Fumbo la Msalaba na hapo wakapata chemchemi ya majibu yaliyozima kiu ya maisha yao ya ndani! Kwa njia ya Roho Mtakatifu, wameweza kutambua msingi wa sayansi ya huruma na upendo wa Mungu, chemchemi ya hekima na busara ya Kikristo, yaani mwanga wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuishi katika mwanga wa Mungu kwa kutambua kwamba, utukufu wa Mungu umetundikwa Msalabani! Kwa Mtakatifu Petro, wanafunzi wengine na hata kwa Wakristo katika ulimwengu mamboleo bado Msalaba unaonekana kuwa ni kashfa ya mwaka. Lakini, kwa Kristo Yesu, kashfa inakuja pale Mkristo anapoukimbia Msalaba, yaani kukimbia na kutofanya mapenzi ya Mungu, utume na kazi ya ukombozi ambayo alitumwa na Baba yake wa mbinguni kuja kuutekeleza.
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba, anaadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba “Exaltatio Sanctae Crucis” kwa lugha ya Kilatini. Fumbo la Msalaba linayagusa maisha ya mwamini kwa namna ya pekee. Msalaba katika mapokeo ya kale, ilikuwa ni alama ya uovu wa kutisha na hali ya kukatisha tamaa, lakini, kwa njia ya Kristo Yesu Mkombozi wa dunia, Msalaba umepata maana mpya katika maisha ya mwanadamu. Msalaba sasa ni kielelezo cha ushujaa wa Kristo Yesu na mashuhuda wa imani, wanaoendelea kuteseka pamoja na kuyamimina maisha yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake sehemu mbalimbali za dunia. Maadhimisho ya Sikukuuu ya Kutukuka kwa Msalaba kwa Mwaka 2022 yanapata uzito wa pekee kwa watu wa Mungu nchini Kazakhstan, kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Fumbo la Msalaba lilikuwa ni chemchemi ya nguvu, imani na matumaini kwa Wenyeheri: Padre Władysław Bukowiński, aliyefariki dunia tarehe 3 Desemba 1974 wakati wa madhulumu dhidi ya Kanisa. Mwenyeheri Alessio Zaryckyj (1912-1963), Mwenyeheri Askofu Mykyta Budka.
Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi linaadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022. Kongamano hili linanogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Jumatano tarehe 14 Septemba 2022, Baba Mtakatifu anashiriki katika ufunguzi wa mkutano huu kwa kutoa hotuba, atapata muda wa kukaa kimya na hatimaye, kukutana kwa faragha na baadhi ya viongozi wa dini. Jioni, Baba Mtakatifu anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 70% ya wananchi wa Kazakhstan ni waamini wa dini ya Kiislam, asilimia 25% ni Wakristo na kati yao waamini wa Kanisa Katoliki ni walau kiasi cha 1% ya wananchi wote wa Kazakhstan. Ni katika muktadha huu, Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba inachukua uzito wa pekee kwa watu wa Mungu nchini Kazakhstan. Maaskofu wa Kazakhstan wanasema, hii ni Sherehe ya shukrani inayofumbatwa katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, licha ya matatizo na magumu ya maisha. Huu ni mwanzo wa kutembea katika njia ya haki, amani na ukweli, kwani Baba Mtakatifu Francisko anawatembelea kama hujaji wa umoja na amani.
Sikukuu ya Kutuka kwa Msalaba inapata chimbuko lake kunako mwaka 335 Mfalme Costantino alipojenga Makanisa makuu mawili na kwa mara ya kwanza, akawaonesha watu Masalia ya Msalaba Mtakatifu. Hata hivyo, hii ni Sikukuu yenye ukuu na maana yake kwani inadhihirisha kuwa Msalaba wa Kristo ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu; ni siku ambayo Msalaba wa Kristo unang’ara duniani! Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuutangaza utukufu na kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele. Changamoto kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kuuangalia, kuutafakari, kuushangaaa, kuusikiliza, kuuheshimu, kuutukuza na kuuabudu kwa imani, matumaini na mapendo, kwani ni kielelezo ambacho wokovu wa dunia umetundikwa juu yake! Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye!
Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo. Waamini watambue ukuu wa Msalaba na wala si tu kama kito cha thamani wanachovaa shingoni au kupamba majumbani mwao, bali ni dira na mwaliko wa kuutafakari upendo wa Yesu aliyejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba iwasaidie waamini kutambua na kuthamini ukuu wa Msalaba, madhara ya dhambi na thamani ya mateso ya Kristo Yesu Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa watu wote. Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na kifo. Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya ukimya mkubwa.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Msalaba unatisha, kama ilivyojionesha hata kwa Mitume wa Yesu, waliotaka kukimbia madhulumu ya Nero; Mtume Petro kwa mshangao mkubwa akakutana na Kristo Yesu njiani akielekea mjini Roma ili aweze kusulubishwa mara ya pili; hapo ndipo Mtume Petro alipoishiwa nguvu, akapiga moyo konde na kufuata nyayo za Kristo Yesu, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake juu ya Msalaba miguu juu, kichwa chini, kwa kutambua kwamba, Yesu alikuwa amempenda upeo! Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya Msalaba, Yesu anajiunga na wale wote wanaodhulumiwa na kuteswa; watu ambao hawana tena nguvu ya kupiga kelele; hasa watu wasiokuwa na hatia wala ulinzi madhubuti; familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha; wale wanaolia na kuomboleza kwa kuondokewa na wapendwa wao katika maisha; wanaowalilia watoto wao waliotumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu anaungana na mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani wakati ambapo kuna sehemu nyingine za dunia wanakula na kusaza! Anajiunga na wale wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani, mawazo na rangi ya ngozi yao.
Kristo Yesu anaendelea kujiunga na umati mkubwa wa vijana uliopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya maisha kutokana na wanasiasa wanaowaongoza kuelemewa mno na: Uchoyo, ubinafsi rushwa na ufisadi. Yesu anaendelea kuungana kwa njia ya Fumbo la Msalaba na waamini ambao wamepoteza imani yao kwa Mungu na Kanisa kutokana na kashfa na utepetevu wa imani ulioneshwa na watumishi wa Injili. Yesu anayapokea yote haya kwa mikono miwili na kujitwika mabegani mwake pamoja na Misalaba ya wafuasi wake, tayari kuwaambia, jipeni moyo kwani yuko pamoja nao na kwamba, ameshinda dhambi na mauti na yuko kati yao ili kuweza kuwakirimia matumaini na maisha tele! Fumbo la Msalaba ni mwaliko kwa kila mwamini kuwa kama Simoni wa Kirene, aliyemsaidia Kristo Yesu kubeba Msalaba, Mtakatifu Veronica aliyeupangusa Uso wa Yesu, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na kwa wanawake wengine watakatifu, waliopiga moyo konde, wakaifuata ile Njia ya Msalaba; “Via Crucis”; Njia ya uchungu “Via Dolorosa” wakiwa wamesheheni upendo na huruma hadi chini ya Msalaba, wakiwa wamesheheni matumaini kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.
Ni kutokana na mazingira haya, Kristo Yesu, akageuka na kumwambia Petro “Nenda nyuma yangu, Shetani! U kikwazo kwangu, maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu” Rej. Mt. 16: 23. Msalaba ni alama takatifu ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni Sadaka ya Kristo Yesu na kamwe, Msalaba usigeuzwe kuwa ni alama ya mapambo shingoni au kuhusianishwa na imani za kishirikina. Kila mara mwamini anapomtaza Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, amwone kuwa ni Mtumishi mwaminifu wa Mungu, aliyetekeleza dhamana na utume wake, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake unaoleta wokovu, kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za binadamu. Matokeo yake, kama kweli waamini wanataka kuwa wafuasi wake, wanapaswa kufuata nyayo zake, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani.