Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Kazakhstan: Misa: Kutukuzwa Kwa Msalaba
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba, anaadhimisha Sikukuu ya Kutukuzwa kwa Msalaba “Exaltatio Sanctae Crucis” kwa lugha ya Kilatini. Fumbo la Msalaba linayagusa maisha ya mwamini kwa namna ya pekee. Msalaba katika mapokeo ya kale, ilikuwa ni alama ya uovu wa kutisha na hali ya kukatisha tamaa, lakini, kwa njia ya Kristo Yesu Mkombozi wa dunia, Msalaba umepata maana mpya katika maisha ya mwanadamu. Msalaba sasa ni kielelezo cha ushujaa wa Kristo Yesu na mashuhuda wa imani, wanaoendelea kuteseka pamoja na kuyamimina maisha yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake sehemu mbalimbali za dunia. Maadhimisho ya Sikukuuu ya Kutukuka kwa Msalaba kwa Mwaka 2022 yanapata uzito wa pekee kwa watu wa Mungu nchini Kazakhstan, kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Fumbo la Msalaba lilikuwa ni chemchemi ya nguvu, imani na matumaini kwa Wenyeheri: Padre Władysław Bukowiński, aliyefariki dunia tarehe 3 Desemba 1974 wakati wa madhulumu dhidi ya Kanisa. Mwenyeheri Alessio Zaryckyj (1912-1963), Mwenyeheri Askofu Mykyta Budka. Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba iwasaidie waamini kutambua na kuthamini ukuu wa Msalaba, madhara ya dhambi na thamani ya mateso ya Kristo Yesu Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa watu wote.
Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na kifo. Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya ukimya mkubwa. Juu ya Msalaba umetundikwa wokovu wa binadamu na kwamba, Msalaba ni nguvu ya Mungu, utambulisho wa Mkristo na chemchemi ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 14 Septemba 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Sikukuu ya Kutukuzwa kwa Msalaba, kwa kujikita katika Liturujia ya Neno la Mungu, Sikukuu ya Kutukuzwa kwa Msalaba. Hes 21: 4-9, Flp 2: 6-11; Yn 3: 13-17. Baba Mtakatifu katika tafakari yake amezungumzia kuhusu nyoka wa moto waliotumwa na Mungu, wakawauma na watu wengi wakafa, nyoka ya shaba inayookoa maisha na nyoka wanaoendelea kuhatarisha maisha ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. “Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.” Hes 21:5.
Katika safari ya kuelekea nchi ya ahadi, Waisraeli, walivunjika moyo, wakakata tamaa, kiasi hata cha kutaka kusahau nchi ya ahadi na kushindwa kutambua kwamba, Mungu alikuwa kati pamoja nao huku akiwaongoza. Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, Shetani, Ibilisi kwa mfano wa nyoka ndiye aliyewashawishi Adamu na Hawa kiasi cha kutia shaka uwepo wa Mungu, wivu wa Mungu na jinsi alivyokuwa anawanyima uhuru na furaha. Waisraeli wakiwa jangwani, nyoka za moto zinarejea tena, yaani dhambi ya asili inaibuka kwa mara nyingine tena, kiasi cha Waisraeli kuhoji uwepo wa Mung una hivyo kushindwa kumwamini, wakamlalamikia na kumwasi Mungu asili ya maisha na matokeo yake wakakumbana uso kwa uso na kifo na huo ukawa ni mwisho mwa moyo usikuwa na imani. Hii ni fursa kwa waamini kuchunguza dhamiri zao na kuangalia ni wepi ambapo katika maisha ya mwamini mmoja mmoja au jumuiya ya waamini walishindwa kumwamini Mungu, huyu ndiye nyoka wa ukosefu wa uaminifu anayeweza kuwang’ata wote, kwa kuwatumbukiza katika ombwe na hali ya kuvunjika, kupondeka na kufa moyo, kiasi hata cha kukosa ari na mwelekeo wa sahihi wa maisha.
Baba Mtakatifu anasema, Kazakhstan ni nchi ambayo katika historia yake, imeng’atwa na vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Kanisa; uhuru, utu, heshima na haki msingi za binadamu zikawekwa rehani. Hizi ni kumbukumbu za kihistoria ambazo zinaendelea kuishi, changamoto na mwaliko wa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha msingi wa amani, hatua kwa hatua. Kama yalivyo maendeleo fungamani ya binadamu, haki jamii, na utulivu miongoni mwa waamini wa dini mbalimbali nchini Kazakhstan. Ni wajibu wa watu wote kujikita mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kufahamiana, ili hatimaye kujenga madaraja ya ushirikiano na mshikamano na watu wa kila taifa na tamaduni. Yote haya yanogeshwe na imani kwa Kristo Yesu, kwa kumwangalia na kujifunza kutoka kwake, ili kuonja upendo wake wa ujumla; upendo unaoteseka. Baada ya watu kung’atwa na kufa sana, wakatubu na kumwongokea “Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi.” Hes 21:8. Hii inaonesha mpango wa Mungu kushuhulikia dhambi, mdhambi na wale wasiomwamini wala kumtegemea. Hiki ni kielelezo cha mapambano ya maisha ya kiroho. Kristo Yesu aliyeteswa, akatundikwa Msalabani na hatimaye, akafa na kuzikwa, ni chemchemi ya maisha mapya. Ni mshindi dhidi ya dhambi na mauti.
Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu alivyoishinda dhambi na mauti. Kwa wale wote waliotenda dhambi, wanapata msamaha na huruma ya Mungu kwa kumkimbilia Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuikimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Kristo Yesu ni njia ya wokovu, maisha mapya na ufufuko. Huyu ndiye aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na hivyo kutoa mwelekeo mpya wa Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwanadamu. Kutoka katika Msalaba wa Kristo Yesu, waamini wanajifunza: Upendo, dhidi ya chuki; Huruma dhidi ya tabia ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; msamaha dhidi ya tabia ya kutaka kulipiza kisasi. Kristo Yesu amenyoosha mikono yake Msalabani, kielelezo cha Mwenyezi Mungu anayewakumbatia watoto wake; anawaonesha ule upendo wa kidugu unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, na utambulisho wa Kikristo. Msalaba ni kielelezo cha unyenyekevu, sadaka na upendo kwa wote bila masharti. Msalaba wa Kristo Yesu umeondoa sumu ya kifo na kufyekelea mbali tabia ya watu kung’atana, imeondoa litania ya malalamiko, kuseng’enyana; tabia ya kupandikiza maovu ndani ya jamii; kwa kuharibu na kuchafua mazingira nyumba ya wote kwa dhambi na tabia ya kutokuaminiana.
Kwa kuchomwa kwake na mkuki ubavuni waamini wamekirimiwa maisha mapya. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini wote watajitahidi kuwa huru dhidi ya sumu ya kifo. Kwa njia ya neema ya Mungu, wanaweza kuwa Wakristo wakamilifu na mashuhuda wa furaha, maisha mapya, upendo na amani. Baba Mtakatifu Francisko yuko nchini Kazakhstan ili kushiriki katika Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi linaloadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan, nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022. Kongamano linanogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Na hii ni hija ya Baba Mtakatifu Francisko ya 38 Kimataifa.