Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Kazakhstan: Mahojiano Maalum Na Wanahabari
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi limekuwa likiadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Hii ni hija ya 38 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa, lengo ni kuendelea kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Jumatano, tarehe 14 Septemba 2022 alipata fursa ya kutoa hotuba ya ufunguzi wa Kongamano hili lililofunguliwa kwa sala ya ukimya na kukazia kuhusu: Utambulisho na thamani ya uhai wa mwanadamu; athari za misimamo mikali ya kidini na kiimani; Uhuru wa kidini na changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa: UVIKO-19, Amani, Udugu wa Kibinadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 15 Septemba 2022 amepata fursa tena ya kutoa hotuba ya kufunga Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi. Katika hotuba yake alijikita katika mambo makuu yanayofungamanishwa na amani na umoja; Tamko la Kongamano linalobeba muhtasari wa mafundisho makuu ya dini duniani; uhuru wa kidini; utu, heshima na haki msingi za binadamu; Ujenzi wa udugu wa kibinadamu; amani, wanawake na kwamba, vijana ni mashuhuda na vyombo vya amani na umoja.
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 15 Septemba 2022 akiwa njiani kurejea mjini Vatican alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kuwenye msafara wake nchini Kazakhstan. Amezungumzia kuhusu vita kati ya Urussi na Ukraine; haki ya kujilinda dhidi ya maadui, biashara haramu ya silaha na madhara yake duniani; Siasa na sera za Bara la Ulaya zinavyotishia tunu msingi za maisha ya kijamii na kiutu na hivyo kuibua viongozi wanaojitafutia umaarufu wa kisiasa ili kujimwambafai mbele ya Jumuiya ya Kimataifa. Kanisa linahitahi wachungaji wema na watakatifu na wala si tu mikakati ya shughuli za kichungaji. Baba Mtakatifu bado ametia nia ya kutembelea Sudan ya Kusini na DRC, Mwezi Februari 2023 panapo majaliwa. Baba Mtakatifu ameshangazwa sana na maendeleo makubwa yaliyopatikana nchini Kazakhstan katika kipindi cha miaka thelathini tangu ilipojipatia uhuru wake. Ni nchi yenye watu milioni 19; watu wenye nidhamu na ustaarabu wa hali ya juu kabisa. Kuna maendeleo makubwa ya viwanda, uchumi fungamani pamoja na utajiri mkubwa wa utamaduni, mila na desturi njema. Baba Mtakatifu ameguswa sana kwa kushiriki katika Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi lililoadhmishwa mjini Kaza, Nur Sultan, Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Amepata nafasi ya kusisikiliza maoni, changamoto na fursa katika mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kudumisha amani duniani, anasema, Mungu akipenda, angetamani kurudi tena nchini Kazakhstan, lakini zaidi kwa ajili ya kushiriki katika Kongamano la 8 la Kimataifa.
Baba Mtakatifu anasema amani ni tunda la haki na mapendo na kushindwa kwa amani matokeo yake ni vita. Mababa wa Kanisa wanasema, vita ya uchokozi kwa asili ni mbaya, ni kinyume cha kanuni maadili na utu wema. Kunapozuka vita katika nchi fulani, viongozi wa nchi hiyo iliyoshambuliwa wana wajibu na haki ya kujihami hata kwa kutumia silaha. Kwa mujibu wa sheria inayokubalika kihalali, matumizi ya nguvu lazima yazingatie masharti fulani: Madhara yaliyosababishwa na uchokozi huo kwa Taifa au Jumuiya ya Kimataifa yawe ya kudumu, mazito na yaliyothibitika kuwa ni ya kweli. Njia nyingine zote zilizojaribiwa kuuzima uchokozi huo ziwe zimeonekana kutofaa na kuwe na matumaini makubwa ya kufanikiwa. Matumizi ya silaha yasisababishe madhara na fujo kubwa zaidi kuliko madhara na fujo zilizokusudiwa kukomeshwa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kimsingi hakuna vita halali, hii ni dhana ambayo imepitwa na wakati kwa sababu vita ni kati ya vyanzo vikuu vya maafa na umaskini kama inavyoonekana katika vita kati ya Urussi na Ukraine; Azerbaijan na Armenia. Myanmar, Pwani ya Pembe ya Afrika kunawaka moto, Msumbiji, Eritrea na Ethiopia choko choko zinaendelea. Watu wa Mungu walidhani kwamba, Vita Kuu ya Pili ya Dunia kunako mwaka 1945 ingekuwa vita ya mwisho kwenye uso wa dunia. Watu wanaendelea kuteseka kutokana na vita inayorindima sehemu mbalimbali za dunia.
Watu wa kiu ya haki na amani duniani; wana kiu ya elimu makini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wao. Lakini kwa bahati mbaya, biashara ya silaha duniani, inaendelea kushamiri kama uyoga. Kuna haja ya kuwa na ujasiri wa kutoshirikiana na wafanyabiashara wa silaha duniani. Wahusika wa Vita wanapaswa kutubu na kumwongekea Mungu pamoja na kuwafidia waathirika wa Vita hivyo. Vita katika ukweli ni kosa na kwamba, watu wanaweza kujihami, pale inapowabidi. Baba Mtakatifu Francisko anasema. Vita ina madhara makubwa kwa watu na mali zao; inadhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Vita inazalisha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuwatumbukiza watu katika umaskini wa hali na kipato. Majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu sana, ingawa wakati mwingine ni vigumu kufanya majadiliano na wale ambao wameanzisha vita, ili kupata suluhu na hatimaye kukomesha vita. Baba Mtakatifu anasema, mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na waasisi wa Umoja wa Ulaya hapo tarehe 25 Machi 1957, ni kujiwekea sera na mikakati ya kukabiliana na changamoto mamboleo katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni, lakini hasa kwa kuwekeza katika ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu.
Walitaka kulinda na kudumisha uhai, udugu na haki, kama chachu muhimu sana ya mabadiliko Barani Ulaya, baada ya patashika nguo kuchanika wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Waasisi wa Umoja wa Ulaya walikazia kwa namna ya pekee kuhusu: Zawadi ya maisha ya binadamu na haki zake msingi sanjari na umuhimu wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano unaosimikwa katika: ukweli na haki; msingi wa sera za kisiasa, kisheria na kijamii Barani Ulaya. Jumuiya ya Ulaya itaweza kudumu na kushamiri, ikiwa kama itaendelea kujikita katika uaminifu kwa mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Ulaya. Hii ilikuwa ni changamoto ya kuvunjilia mbali kuta za utengenano, ili kuokoa maisha ya familia zilizokuwa zinaogelea katika dimbwi la umaskini, vita na mipasuko ya kijamii, inayoendelea kushuhudiwa hata leo hii. Matatizo na changamoto za uongozi ndani ya Jumuiya ya Ulaya yanapaswa kupewa ufumbuzi wa kudumu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, nchi nyingi Barani Ulaya zimeanza kupoteza tunu ya ukarimu na matokeo yake, Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi.
Kumbe, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi dhidi ya utamaduni wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Wakimbizi na wahamiaji ni amana na utajiri wa Kanisa mahalia. Kuna waasisi wakuu wa Umoja wa Ulaya akina Robert Schuman, Adenauer, De Gasper na wenzake waliosimamisha tunu msingi za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Leo hii kuna viongozi wanaoibuka kutafuta umaarufu usiokuwa na tija wala mvuto kwa kutaka kujimwambafai tu! Utamaduni wa Kifo: Sera za utoaji mimba na Kifo laini: Baba Mtakatifu anaendelea kuwakumbusha waamini kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kama waamini wanaitwa na kuhamasishwa kulinda, kuitunza na kuidumisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu, hata pale watu wanapokumbana na magonjwa pamoja na mahangaiko mbalimbali ya maisha. Hakuna mwenye haki ya “kufyekelea mbali zawadi ya maisha ya binadamu”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, uhai wa binadamu unaheshimiwa na kuthaminiwa na kwa njia hii, kuweza kutangaza na kushuhudi tunu msingi za maisha ya Kikristo katika mazingira ya kifamilia. Kila huduma ya matibabu inayotolewa kwa mgonjwa iwe ni chemchemi ya huruma na upendo kwa wagonjwa wanaoteseka. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya afya ya mwanadamu yanapaswa kuwa kweli ni chombo cha huduma kwa wagonjwa na wala si vinginevyo. Kamwe mgonjwa asionekane kuwa ni mzigo mzito, kiasi cha kuanza kuhalalisha kisheria mchakato wa kifolaini.
Kwa haraka haraka anasema Baba Mtakatifu, jambo hili linaweza kuonekana kuwa kama sehemu ya uhuru wa mtu binafsi; lakini ndani mwake, uhuru huu unafumbata ubinafsi unao thubutu kupima: haki, heshima na utu wa mtu kutokana na umuhimu wake. Kifolaini hakimsaidii mtu kumpunguzia maumivu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, umefika wakati wa kusimama kidete kupinga utamaduni na utandawazi usiojali utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini, ni hatari kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee hata nchini Hispania badala ya sera na mikakati inayopania kuwagawa watu. Siasa ni wito wa huduma miongoni mwa waamini walei ili kudumisha urafiki wa kijamii, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Ni kwa njia hii, siasa inawawezesha watu kuwa ni sehemu ya wadau katika mchakato wa maendeleo yao wenyewe, bila kuwahusisha watu mahalia, hapo hakuna siasa ya kweli! Siasa inafumbata mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika ulimwengu mamboleo! Siasa inasimikwa katika umoja na mshikamano katika utekelezaji wa mpango mkakati kadiri ya mwanga wa tunu msingi za Kikristo. Baba Mtakatifu anakiri kwamba hazifahamu sana siasa za Italia.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu pamoja na wajibu wa kimaadili. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba: wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondosheka na katika sheria za muundo wa jamii. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufunda dhamiri za watu, ili kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. DH.1.
Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Baba Mtakatifu kuhusiana na uhuru wa kidini na kuabudu mintarafu China anasema, hawa ni watu wenye uvumilivu, uzoefu na mang’amuzi makubwa kutoka kwa wanasayansi na wamisionari. Wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa jinsi walivyo. Itakumbukwa kwamba, tarehe 22 Septemba 2018 Vatican na China zilitiliana saini makubaliano ya mpito kuhusu dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kuteuwa Maaskofu Katoliki, makubaliano haya ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini China. Haya ni matunda ya majadiliano, maridhiano na uvumilivu, ili kuganga na kuponya madonda ya kinzani na kutoelewana kati ya nchini hizi mbili. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoka kipaumbele cha pekee kwa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili familia ya Mungu nchini China iweze: kuamini, kutumaini na kupenda na hatimaye, kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao! Kuna baadhi ya waamini na viongozi wa Kanisa nchini China wamekwaza na makubaliano haya ya mpito, lakini hii ni sehemu ya ukweli wa kibinadamu unaofumbatwa pia katika tunu msingi za maisha ya Kikristo.
Hii ni sehemu ya mchakato wa majadiliano yanayolenga kwenye maboresho ya shughuli za kichungaji nchini China; kwa kuheshimu na kuthamini amana na utajiri unaofumbatwa katika mapokeo ya China! Matunda na makubaliano haya ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni wa majadiliano: kwa kusikilizana, ili hatimaye, kupata suluhu ya kudumu katika changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza ili hatimaye, kujenga mshikamano wa udugu wa binadamu. Waamini wa Kanisa Katoliki nchini China wanaomba ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu. Utamadunisho wa Injili ni mbereko ya uinjilishaji na ushuhuda wa imani katika matendo. Baba Mtakatifu Francisko anasema dhamana na wajibu wa majadiliano kati ya Kanisa na China yanaratibiwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Majadiliano hayana budi kupewa kipaumbele cha kwanza. Rais Kassym-Jomart Tokayev wa Kazakhstan, tarehe 14 Septemba 2022 alipokea ugeni mzito kutoka China uliokuwa unaongozwa na Rais Xi Jinping wa China. Kati ya mambo waliyojadiliana ni mahusiano ya kidiplomasia katika kipindi cha miaka 30; ushirikiano wa kiuchumi, ulinzi na usalama. Lakini Rais Jinping hakuweza kuonana na Baba Mtakatifu. Kanisa daima litaendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano, yanayohitaji uwajibikaji unaomwilishwa katika matendo kwa kuheshimu uhuru wa watu, lakini zaidi kwa kuheshimu maisha ya watu wa Mungu nchini Nikaragua. Baba Mtakatifu anasema, bado anakabiliana na changamoto za kiafya lakini bado ametia nia kutembelea Sudan ya Kusini. Hii itakuwa ni hija ya kiekumene na kwamba, panapo majaliwa watakwenda pia nchini DRC.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawahimiza Wakristo kwa busara na mapendo, kwa njia ya majadiliano ya kidini, umoja na ushirikiano na waamini wa dini nyingine, kutoa ushuhuda wa imani na wa maisha yao. Waamini watambue, wahifadhi na kukuza mema ya kiroho, kimaadili, pamoja na tunu msingi za kijamii na za kitamaduni ambazo zinapatikana kutoka kwa waamini wa dini nyingine. Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali ni nyenzo msingi ya kupambana na tabia ya ubinafsi, misimamo mikali ya kidini na kiimani ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na maridhiano kati ya watu, kila mtu akipewa nafasi ya kushuhudia imani yake! Kumbe, katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Wakristo wanapaswa kumuungama Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chanzo cha imani, furaha na matumaini kwa waja wake. Mwenyezi Mungu ni kiini cha majadiliano na watu wake na kamwe hajaacha kuzungumza na wanawadamu katika safari ya maisha yao hapa duniani, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale hata leo hii, Mwenyezi Mungu anazungumza na binadamu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele, aliyetumwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika mchakato wa majadiliano ya kidini nchini Kazakhstan na Moroco.
Baba Mtakatifu katika barua yake kwa familia ya Mungu nchini Ujerumani, anawasihi Maaskofu kushikamana na kutembea kwa pamoja kama ndugu na kamwe asiwepo mtu anayetembea pweke pweke, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Roho Mtakatifu, aweze kupyaisha maisha na utume wa Kanisa nchini Ujerumani. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hiki ni kipindi cha mabadiliko makubwa yanayoibua matatizo na changamoto mpya na zile za zamani, mwaliko kwa familia ya Mungu kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu anatambua hali ngumu ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Ujerumani, ndiyo maana ameamua kuwaandikia ujumbe huu, ili kuunga mkono jitihada zinazoendelea kufanyika hadi wakati huu! Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kama ambavyo imeshuhudiwa wakati wa mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani uliofanyika mwezi Machi 2019. Mkutano huu uliwajumuisha: Maaskofu, wakleri, watawa, wajumbe kutoka kwa waamini walei, wataalam na mabingwa wa mambo mbalimbali katika maisha na utume wa Kanisa. Wote hawa kwa pamoja walijadili na hatimaye kupitisha mbinu mkakati wa kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo nchini Ujerumani. Umuhimu wa utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa nchini Ujerumani ni matunda ya utafiti na upembuzi yakinifu uliofanywa na Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, DBK, inayowahusisha wawakilishi wa makundi mbali mbali ya familia ya Mungu nchini Ujerumani.
Tume hii pamoja na mambo mengine, ili dadavua kwa kina na mapana kuhusu uwepo wa idadi kubwa ya waamini wenye umri mkubwa ndani ya Kanisa Katoliki, ikilinganishwa na idadi ya vijana wanaobatizwa kila mwaka. Tume hii ilipembua pia kuhusu kupungua kwa idadi ya miito ya kitawa na kipadre nchini Ujerumani, mafundisho tenge kuhusu tendo la kujamiiana au kama wanavyofahamu wengi, tendo la ndoa. Tume iligusia pia hali na mtindo wa maisha na utume wa Mapadre nchini Ujerumani. Baba Mtakatifu anasema, hana sababu msingi ya kuzama tena katika tafiti hizi, bali anapenda kujielekeza zaidi kwa kuchangia hoja zake katika maisha ya kiroho zaidi, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya. Kumbe, kipaumbele cha kwanza katika majadiliano haya yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kilenge kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa nchini Ujerumani. Familia ya Mungu nchini Ujerumani iendelee kujiweka chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu kwani historia inafundisha kwamba, pale ambapo Jumuiya ya waamini ilijiangalia yenyewe na kutaka kutatua matatizo na changamoto zake kwa kutumia nguvu zake yenyewe; mbinu na akili zake, imejikuta ikikuza na kuendeleza matatizo yaliyokuwa yanapaswa kupewa ufumbuzi wa kudumu.
Baba Mtakatifu anaikumbusha familia ya Mungu nchini Ujerumani kwamba, inafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika umoja na utofauti; hii ni familia yenye ukarimu, inayojituma na kuwajibika barabara. Jambo la msingi ni kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Kuna hatari kubwa kwa waamini wengi kuendelea kukengeuka kutokana na kutopea kwa imani pamoja na kumong’onyoka kwa kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu; mambo ambayo athari zake zimeanza kutikisa misingi ya maisha ya kijamii na kitamaduni; changamoto ambayo haina majibu ya mkato! Baba Mtakatifu anakazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa nchini Ujerumani kwa kuwashirikisha watu wa Mungu katika ngazi mbali mbali na baada ya sala, tafakari na majadiliano ya kina, matunda ya Sinodi yanarejeshwa tena miongoni mwa familia ya Mungu kwa utekelezaji unaowawajibisha wote; ili kuweza kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Kanisa nchini Ujerumani liendelee kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari kama sehemu ya mbinu mkakati wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ndani na nje ya Ujerumani. Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili uendelee kuimarishwa, ili kutoa utambulisho kwa waamini kwamba, wao ni sehemu ya watu wa Mungu wanaendeleza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kuukumbatia utakatifu wa maisha!
Mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa hauna budi kufumbata chachu na tunu msingi za Kiinjili, kiutu na kimaadili; kwa kutambua kwamba, wao ni waamini wa Kanisa Katoliki. Hapa kuna hja ya kuzama katika wongofu wa shughuli za kichungaji, kama dira na mwongozo wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa watu wa Mungu. Roho Mtakatifu awalinde na kuwaongoza watu wa Mungu nchini Ujerumani katika majadiliano yao ili kuwa na mwelekeo sahihi wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, vinginevyo, Sinodi pia inaweza kutumiwa vibaya na kuweza kusababisha kinzani na mipasuko miongoni mwa watu wa Mungu nchini humo. Kanisa linapaswa kuendeleza utume wake wa kinabii nchini Ujerumani, kwa kusaidia kuinjilisha na kutamadunisha maisha ya watu wa Mungu, ili hatimaye, waweze kupata maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu anakaza kusema, upyaisho wa kweli wa maisha na utume wa Kanisa unafumbatwa katika ujenzi wa utamaduni wa kukutana na wengine katika huduma hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni wakati wa kukuza na kudumisha Injili ya uhai, upendo na mshikamano dhidi ya utamaduni wa kifo na utandawazi usioguswa na mahangaiko ya watu wengine! Ni vyema ikiwa kama familia ya Mungu nchini Ujerumani itaondokana kabisa na tabia ya maamuzi mbele na chuki dhidi ya wageni na wahamiaji nchini humo!
Baba Mtakatifu anaendelea kukazia umuhimu wa utambuzi wa Kikanisa “Sensus Ecclesiae” katika utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, ili wote waweze kutembea kwa pamoja na katika umoja. Changamoto changamani ni pevu sana. Kuna maswali yanayoibuliwa na kamwe hayawezi kufumbiwa macho, bali kushughulikiwa, kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa ukweli wa mambo nchini Ujerumani. Kanisa lijenge na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza hasa maskini, wadogo na wanyonge ndani ya jamii. Katika hija hii ya Kanisa kama sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, hata katika tofauti zao, waamini wajiweke chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Kristo Yesu anawaonesha njia ya Heri za Mlimani kama dira na mwongozo wa maisha mapya. Kimsingi, watu wa Mungu nchini Ujerumani wanawahitaji wachungaji wema na watakatifu, watakaokuwa karibu zaidi na waamini wao. Kamwe Kanisa lisiongozwe kama taasisi ya Kisiasa. Viongozi wa Kanisa wajenge na kuimarisha ujirani mwema na waamini wao. Mchakato wa kutaka kupyaisha Kanisa Katoliki nchini Ujerumani, hazina budi kusimikwa katika toba na wongofu wa ndani, kwa kujenga na kuimarisha ujirani mwema kati ya waamini na viongozi wao wa Kanisa.