Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Kazakhstan: Shukrani na Baraka
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume ya 38 Kimataifa, ilipania pamoja na mambo mengine: kuendelea kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu katika hija hii amekuwa ni hujaji wa majadiliano, amani na matumaini kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Kazakhstan. Ameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Kama sehemu ya desturi na utamaduni wake, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 16 Septemba, 2022 Kumbukumbu ya Watakatifu Cornelio na Cypriani, Mashahidi wa imani amekwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, Jimbo kuu la Roma, baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume ya 38 Kimataifa huko Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022.
Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea kutoka Nur Sultan, Kazakhstan amepitia katika anga Kazakhstan, Azerbaijan, Georgia, Bulgaria, Uturuki, Serbia/Montenegro, Bosnia-Erzegovina, Croatia, na hatimaye Italia, Baba Mtakatifu ametumia pia fursa hii kuwapatia na kuwatakia: furaha, neema na baraka; umoja, amani; ustawi, udugu maendeleo pamoja na kuwahakikishia sala zake katika maisha na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wakuu wa nchi na serikali zao. Amewashukuru watu wa Mungu nchini Kazakhstan kwa ukarimu na upendo waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini mwao.
Baba Mtakatifu katika salam na matashi mema kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia amemwambia kwamba, amekuwepo nchini Kazakhstan ili kushiriki katika Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022. Hili ni Kongamano ambalo limenogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumkirimia fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa dini pamoja na watu wa Mungu nchini Kazakhstan, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika amani. Anawashukuru watu wa Mungu nchini Italia na kuwatakia heri, baraka na fanaka katika maisha yao. Mwishoni amewapatia baraka zake za Kitume.