Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi. Baba Mtakatifu Francisko anashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Kazakhstan: Uhuru wa Kidini, Dhamiri, Haki na Amani

Hotuba imegusia: Mila, desturi na tamaduni; Hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini humo, mchango wa viongozi wa dini katika ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu; haki na wajibu; demokrasia na utamaduni wa kusikiliza, maridhiano, amani, majadiliano na kwamba, diplomasia inao wajibu wa kukuza na kudumisha majadiliano katika medani mbalimbali za Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi linaadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022. Kongamano hili linanogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Baba Mtakatifu, mara baada ya kuwasili, alilakiwa na wenyeji wake kwa heshima ya kitaifa, akapata nafasi ya kumtembelea na kuzungumza kwa faragha na Rais Kassym-Jomart Kemeluly Tokayev wa Kazakhstan ambaye amekuwepo madarakani kuanzia tarehe 12 Juni 2019.

Ziara ya Kitume nchini Kazakhstan
Ziara ya Kitume nchini Kazakhstan

Baadaye, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na viongozi wa asasi za kiraia katika Ukumbi wa “Qazaq Conert Hall.” Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia kuhusu: Mila, desturi na tamaduni njema; Hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini humo kunako mwaka 2001, mchango wa viongozi wa dini katika ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu; haki na wajibu; demokrasia na utamaduni wa kusikiliza kwa makini; maridhiano, amani, majadiliano katika ukweli na uwazi na kwamba, diplomasia inao wajibu wa kukuza na kudumisha majadiliano katika medani mbalimbali za Kimataifa na kwamba, silaha za nyuklia ni tishio kwa: haki, amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa.

Ziara ya Kitume nchini Kazakhstan
Ziara ya Kitume nchini Kazakhstan

Baba Mtakatifu amesema, yuko nchini Kazakhstan kama hujaji wa amani anayetafuta kunogesha majadiliano na umoja, kwa kukazia mila, desturi na tamaduni njema zinazowaunganisha watu wa Mataifa, tayari kuzirithisha kwa vizazi vijavyo! Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2001 alifanya hija ya kitume nchini Kazakhstan na kuielezea kuwa ni nchi ya wafiadini na mashuhuda wa imani, ni nchi ya mashujaa, watu wasomi na wasanii. Kazakhstan ni ambayo inakumbatia utukufu wa historia ya utamaduni, utu na mahangaiko ya watu, hasa kutokana na madhulumu dhidi ya Kanisa yaliyopelekea waamini wengi: kuuwawa, kuteswa na kufungwa magerezani na wengine, kupelekwa uhamishoni.

Ziara ya Kitume nchini Kazakhstan
Ziara ya Kitume nchini Kazakhstan

Hii ni historia ya utengano na ubaguzi, inayowachangamotisha watu wa Mungu nchini Kazakhstan sasa kusimama kidete na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu wote pasi na ubaguzi wa kijinsia, kikabila au imani ya mtu. Kazakhstan ni daraja linalounganisha Bara la Ulaya na Asia, changamoto ya kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja na mshimanano wa udugu wa kibinadamu. Itakumbukwa kwamba, Kazakhstan ina makabila 550 na wananchi wanaozungumza lugha 80, ushuhuda wa umoja katika utofauti, kiasi kwamba, nchi hii ni kielelezo cha daraja linalowakutanisha watu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, yuko nchini Kazakhstan ili katika maadhimisho ya Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi. Hii inaonesha kwamba, viongozi wa kidini wanao mchango mkubwa katika kukuza uhuru wa kuabudu na uhuru wa imani, kwa kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani; kwa kudumisha usawa kati ya raia, ili kuendeleza uzalendo, umoja na mshikamano wa kitaifa unaovuka ukabila, lugha na dini za watu. Dini mbalimbali ziwasaidie waamini kuwa ni mashuhuda wa imani na uhuru wa kidini, kama kielelezo makini cha ushirika na mafungamano ya kijamii. Kazakh, maana yake ni kutembea katika uhuru unaotambua haki na wajibu. Haya ni mambo msingi katika kukuza uhuru wa mawazo, dhamiri pamoja na uhuru wa mtu kujieleza. Kumbe, kila mtu anaweza kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ndani ya jamii.

Ziara ya Kitume nchini Kazakhstan
Ziara ya Kitume nchini Kazakhstan

Baba Mtakatifu amegusia umuhimu wa demokrasia na utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kwa kutambua kwamba, uongozi ni kwa ajili ya huduma kwa jamii. Ujenzi wa demokrasia makini ni mchakato wa muda mrefu unaohitaji subiri na uvumilivu. Demokrasia na ujenzi wa miji mipya inapaswa kusimikwa katika siasa safi, ushirika wa wananchi kwa ajili ya ustawi, maendeleo fungamani na mafao ya wengi. Hii ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa, ili kurekebisha mfumo tenge wa ugawaji wa rasilimali za nchi, kwa kuzingatia haki na wajibu; usawa na haki msingi za binadamu na kwamba, wananchi wote wanayo dhamana na wajibu wa kukuza na kuendeleza uchumi kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu badala ya kutafuta faida kubwa.

Baba Mtakatifu amekazia kuhusu: Maridhiano, amani, majadiliano katika ukweli na uwazi na kwamba, diplomasia inao wajibu wa kukuza na kudumisha majadiliano katika medani mbalimbali za Kimataifa. Baba Mtakatifu anafanya hija hii ya kitume wakati ambapo kuna vita kati ya Urussi na Ukraine vinaendelea kupamba moto na kwamba, yuko kati yao ili kupaaza kwa mara nyingine tena, kilio cha amani ambacho ni muhimu sana katika ujenzi wa maendeleo katika ulimwengu wa utandawazi. Diplomasia ya Kimataifa isaidie kukoleza mchakato wa majadiliano ili kuondkana na dhana ya uadui, na mafao ya watu binafsi. Jumuiya ya Kimataifa inahitaji viongozi watakaojifunga kibwewe kujenga na kudumisha misingi ya amani na utulivu kwa sasa na kwa kizazi kijacho, kwa kuzingatia misingi ya uelewa, uvumilivu na majadiliano na watu wote. Baba Mtakatifu anasema silaha za nyuklia ni tishio kwa: haki, amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Kumbe, kuna haja ya kujikita zaidi katika majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wakatoliki wataendeleza majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi nchini Kazakhstan.

Ziara ya Kitume nchini Kazakhstan
Ziara ya Kitume nchini Kazakhstan

Mwaka 2022, Vatican na Kazakhstan zinaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 30 ya Uhusiano wa Kidiplomasia. Kumbe, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko nchini humo ni fursa ya kusherehekea ukarimu na kuendelea kunogesha majadiliano ya kidugu na viongozi wakuu wa dini kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaombea watu wa Mungu nchini Kazakhstan amani, umoja, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Viongozi na wale wote wenye dhamana ya uongozi wahakikishe kwamba, wanasimamia mafao ya wengi, utulivu, amani na ustawi wa wote.

Hotuba ya Papa kwa viongozi wa kidiplomasia nchini Kazakhistan
13 September 2022, 16:16