Tafuta

Kristo Yesu ni kiini cha upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa tayari kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kiekaristi. Kristo Yesu ni kiini cha upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa tayari kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kiekaristi. 

Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa: Yesu kiini Cha Upyaisho wa Maisha na Matumaini

Mambo msingi: Umuhimu wa Ekaristi Takatifu unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu na utu wa ndani dhidi ya dini inayojimwambafai kwa mwonekano wa nje. Ni mwaliko wa kudumisha upendo, kujenga udugu wa kibinadamu kama kielelezo makini cha Kanisa la Kisinodi ili kupambana na upweke hasi na umaskini. Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya matumaini mapya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia kuanzia tarehe 22-25 Septemba 2022, imekuwa ni fursa adhimu ya kutafakari umuhimu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, hii ni Sakramenti pacha na Sakramenti ya Upatanisho inayowawezesha waamini kujichotea neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho haya. Waamini wameshiriki “Njia ya Nuru ya Ekaristi Takatifu”: “Via Lucis Eucaristica.” Waamini wamepata nafasi ya: Kutafakari, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kuabudu Ekaristi pamoja na kutolea Ushuhuda wa maisha yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Umoja na ushiriki katika maisha na utume wa Kanisa umejidhihirisha wazi kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Baba Mtakatifu Francisko domenika tarehe 25 Septemba 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu na kufunga rasmi maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia huko Jimbo kuu la Matera-Irsina kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Torniamo al gusto del pane. Per una Chiesa Eucaristica e Sinodale” "Turudi Kwenye Ladha ya Mkate kwa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi." Ibada hii imehudhuriwa na waamini kutoka sehemu mbalimbali za Italia. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa Ekaristi Takatifu unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu na utu wa ndani dhidi ya dini inayojimwambafai kwa mwonekano wa nje. Ni mwaliko wa kudumisha upendo kwa jirani, kwani Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo inayowabidiisha waamini kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu kama kielelezo makini cha ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ili kupambana na upweke hasi na umaskini.

Mwaliko wa kushikakama na Kristo Yesu katika maisha na utume wa Kanisa
Mwaliko wa kushikakama na Kristo Yesu katika maisha na utume wa Kanisa

Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya matumaini mapya yanayomweka Kristo Yesu kuwa ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya furaha inayowawezesha waamini kushirikishana tunu msingi za maisha ya kiroho, kuimarishana na hatimaye, kujenga ushirika wa watoto wa Mungu. Kwa bahati mbaya sana, matamanio halali yanayobubujika kutoka katika Meza ya Chakula cha Bwana, yamekwenda kinyume kabisa cha mchakato wa ujenzi wa ushirika na matokeo yake ukosefu wa haki unatawala, kwa maskini wa hali na kipato kuendelea kuongezeka kila kukicha. Mama Kanisa anawaalika watoto wake kuhakikisha kwamba, Fumbo la Ekaristi Takatifu linakua ni chanzo na kilele cha maisha ya Wakristo, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha na utume wao. Waamini wasitende kamwe kama yule tajiri anayesimuliwa na Mwinjili Luka 16: 19-31 aliyepoteza jina na utambulisho wake, kwa kumezwa na malimwengu na hivyo kutambulikana kwa vitu alivyokuwa anavimiliki na wala si utu na heshima yake; bali mavazi yake ya zambarau na kitani safi. Maskini analo lina kamili na utambulisho wake unaomaanisha kwamba, “Mwenyezi Mungu anasaidia.” Hata katika umaskini na hali yake mbaya kiuchumi na kijamii, lakini bado: utu, heshima na utambulisho wake vinamfuata na kumwandama na kwamba, ndani mwake kuna matumaini ya uwepo angavu wa Mungu anamyemsaidia!

Kristo Yesu awe chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Kristo Yesu awe chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Haya ni matumaini yasiyo danganya hata kidogo. Changamoto pevu kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, katika maisha na utume wao, wanajitahidi kumwabudu Mwenyezi Mungu na wala si kujitafuta wao wenyewe; wasimezwe na utajiri pamoja na malimwengu yake, vinginevyo watageuka na kuwa ni watumwa wa mambo yanayoonekana kwa nje, lakini utu wao wa ndani si mali kitu! Waamini wamwangalie Kristo Yesu anayeishi ndani mwao, kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu na kuendelea kutambua kwamba, anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu. Kwa huruma na upendo wake wa daima, wamemvika vazi la uzuri, heshima na uhuru kamili na kamwe hataki kuwaachilia watumbukie kwenye mifumo mbalimbali ya utumwa, kwa sababu utu na heshima yao vinapata asili na hatima yake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo, inayowaunganisha waamini kuwa ndugu wamoja. Ni katika Ekaristi, Kristo Yesu anajimega na kujitoa sadaka, changamoto na mwaliko kwa waamini kujisadaka bila ya kujibakiza, ili hatimaye, waweze kuwa ni mkate unaoganga njaa na divai inayozima kiu ya maisha ya mwanadamu.

Kristo Yesu asaidie kupyaisha maisha na matumaini ya watu
Kristo Yesu asaidie kupyaisha maisha na matumaini ya watu

Tajiri anayesimuliwa katika Injili la Luka alipungukiwa na tunu hizi msingi na hatimaye, akazama katika mavazi na kujibovusha kwa “madikodiko ya anasa” kiasi hata cha kushindwa kusikia kilio cha maskini Lazaro, aliyekuwa anawekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, akatamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; mbwa wakamramba vidonda vyake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kule kuzimu, tajiri akayainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro kifuani mwake. “Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.” Lk 16:24-27. Waamini wanakumbushwa kwamba, hapa duniani ni wapita njia, makao ya kudumu yako mbinguni. Ni mwaliko kwa waamini kutojifungamanisha sana na malimwengu pamoja na upweke hasi, unaoweza kuwaandama hata baada ya maisha ya hapa duniani.

Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi: Kristo Yesu
Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi: Kristo Yesu

Huu ni wito wa kutenda haki, kusikiliza na kujibu kilio cha maskini; kwa toba na wongofu wa ndani; kwa kushirikiana na kushikamana katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayovunjilia mbali tabia ya uchoyo na ubinafsi kwa kujenga na kuimarisha mshikamano na udugu wa kibinadamu. Waamini wanandoto ya ujenzi wa Kanisa la Kiekaristi, linalowawezesha kujimega na kujisadaka kupambana na upweke hasi na umaskini; kwa kuwatangazia na kuwashuhudia watu Injili ya matumaini, huruma na mapendo kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; kwa kuganga na kufunga madonda ya wale wote wanaoteseka. Ibada ya kweli ni ile inayowajali na kuwahudumia maskini wa ulimwengu huu. Huu ni wito na mwaliko kwa waamini kujizatiti katika ujenzi wa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi, kwa kusimama kidete dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubaguzi, nyanyaso na dhuluma dhidi ya maskini, ili hatimaye, waweze kuwa ni Mitume wa udugu wa kibinadamu; haki na amani duniani. Wawe ni Kanisa linalotoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu, ili siku moja, waweze kushiriki maisha na uzima wa milele pamoja na Kkristo Yesu mbinguni. Kristo ni njia, ukweli na uzima kwa mateso na kifo chake ameshinda nguvu ya kifo. Kamwe waamini wasizimishe moto wa matumaini unaoendelea kuwaka ndani mwao kwa kuendekeza upweke hasi, dhambi, woga na wasi wasi wa kutoweza kutekeleza yale wanayopania. Huu ni wakati anasema Baba Mtakatifu Francisko: "Turudi Kwenye Ladha ya Mkate kwa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi." Ni Kristo Yesu peke yake mwenye nguvu ya kushinda mauti na kupyaisha maisha ya waamini wake.

Ekaristi Kongamano

 

25 September 2022, 16:10