Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu Bikira Maria wa Rimedio alipovikwa taji tarehe 7 Septemba 1952. Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu Bikira Maria wa Rimedio alipovikwa taji tarehe 7 Septemba 1952. 

Kumbukizi la Miaka 70 Tangu Bikira Maria Rimedio Avikwe Taji: Upendo!

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Mauro Gambettikuwa Mwakilishi wake wa kitume, katika Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu Bikira Maria wa Rimedio alipovikwa taji tarehe 7 Septemba 1952, kama sehemu ya mkesha wa Sikukuu ya Kuzaliwa Bikira Maria inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 8 Septemba ya kila mwaka: Ushuhuda wa imani na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba mwaka 1854 katika Waraka wake wa Kitume “Ineffabilis Deus”, alitangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha usafi na mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Malaika Gabrieli “Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.” Lk 1: 28-32. Baba Mtakatifu Francisko asema, Bikira Maria kwa kusikia salamu hii, akafadhaika sana na kushangaa na wala hakujikweza. Anausikia uzito wa salamu na kujisikia mdogo sana ndani mwake mbele ya Mwenyezi Mungu. Unyenyekevu wa Bikira Maria ni kivutio kikubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Bikira Maria Amekingiwa Dhambi ya Asili kwa Mastahili ya Mwanaye Kristo Yesu
Bikira Maria Amekingiwa Dhambi ya Asili kwa Mastahili ya Mwanaye Kristo Yesu

Ni katika mazingira ya familia nyumbani, Bikira Maria anapokea sifa ambazo hakuwahi hata siku moja kujipatia mwenyewe na kuyapokea yote haya kwa moyo wa unyenyekevu pasi na makuu, kwa kutambua kwamba, yale yote aliyokirimiwa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Uhuru binafsi wa Bikira Maria anausadaka kwa ajili ya Mungu na mafao ya wengine. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili amejaliwa macho kwa ajili ya Mungu pamoja na jirani zake. Fadhila ya unyenyekevu inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwenye kuta za familia na katika hali ya kificho na wala si katika maeneo ya wazi au kwenye barabara kuu za mji wa Nazareti. Hii ndiyo habari kuu kwa waamini wote kwamba, Mwenyezi Mungu anatenda miujiza na mambo makuu kwa watu wanyenyekevu, wanaotoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na jirani zao. Ni katika kuta za nyumba ndogo ya Bikira Maria, Mwenyezi Mungu ametenda makuu na kubadili historia ya mwanadamu. Hata leo hii, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mwenyezi Mungu anapenda kutenda maajabu pamoja na watu wake, ili kuleta mabadiliko katika: familia, maeneo ya kazi na katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu, mahali ambapo neema na baraka ya Mungu inatenda kazi.

Papa Pio XII katika Waraka wake wa “Fulgens corona” wa Mwaka 1950, wakati wa kutangaza Maadhimisho ya Mwaka wa Bikira Maria, alimtaja Bikira Maria kuwa ni chemchemi ya: imani, furaha na Malkia wa Mashuhuda wa imani, mwaliko kwa waamini kuwa ni wanafunzi wa nyenyekevu wa Kristo Yesu, kwa kutekeleza yote wanayo amriwa na Kristo Yesu kama ilivyokuwa kwenye Harusi ya Kana ya Galilaya; kielelezo cha upendo na uaminifu wa Mungu kwa waja wake. Mwinjili Yohane anamweka mbele ya macho ya waamini Bikira Maria anayeguswa na mahitaji ya wanandoa wapya waliotindikiwa na divai na hivyo kuomba huruma na upendo wa Yesu kwa niaba yao! Rej. Yn 2:5. Divai ni ishara ya furaha na upendo, lakini wakati mwingine, mwanadamu anatindikiwa na divai, kumbe, katika muktadha huu, waamini wajifunze kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, atakayewaonesha uwepo wa Mungu katika safari ya maisha yao ishara ya: Imani, furaha na upendo. Ujio wa Kristo Yesu ni chemchemi ya: upendo, furaha, amani, msamaha, huruma na utakaso katika maisha.

Bikira Maria ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo
Bikira Maria ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu amemteua Kardinali Mauro Gambetti, O.F.M, CONV., Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kuwa Mwakilishi wake wa kitume, katika Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu Bikira Maria wa Rimedio alipovikwa taji tarehe 7 Septemba 1952, kama sehemu ya mkesha wa Sikukuu ya Kuzaliwa Bikira Maria inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 8 Septemba ya kila mwaka. Ibada kwa Bikira Maria wa Rimedio ina chimbuko lake kunako mwanzoni mwa Karne ya Kumi na Tatu, hasa kutokana na ushuhuda wa huduma ya upendo pamoja na ukombozi wa watumwa, uliowarejeshea tena: utu, heshima na haki zao msingi. Kumbumbukizi ya Miaka 70 tangu Bikira Maria wa Rimedio avikwe taji, ni muda muafaka wa kupyaisha tena: Imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili sanjari na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Iwe ni fursa ya kuweka katika matendo Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani hasa katika mazingira ya kifamilia na katika taasisi mbalimbali za umma, kama ushuhuda wa imani katika matendo. Kwa njia ya Bikira Maria, waamini waweze kumjifunza Kristo Yesu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu.

B.Maria Miaka 70
06 September 2022, 16:22