Papa Francisko ameomba kuendelea kusali kwa ajili ya Ukraine
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumatano tarehe 21 Septemba 2022 mara baada ya tafakari ya Katekesi ya Papa Francisko, mawazo yake bado yamekwenda kwa nchi ya Ukraine na watu wake. Kwa huzuni, mkubwa Papa Francisko ameonesha wazi hali mbaya ya Ukraine inayoteswa
Kabla ya kuwaaga waamini waliokusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Francisko Papa amewasimulia juu ya utume wa mwakilishi wake,Kadinali Konrad Krajewski, ambaye alimtumwa nchini Ukraine kwa mara ya nne ili kuonesha ukaribu wake kwa watu waliojaribiwa vikali na mzozo na Urussi. Jumamosi iliyopita, tarehe 17 Septemba 2022 Kadinali huyo pia alikumbana na hatari hiyo, akihatarisha maisha yake mwenyewe kwa sababu Bus lake lililokuwa na chakula na rozari za Papa, karibu na Zaporizhia, lilipigwa na risasi, lakini hakukuwa na madhara makubwa na msaada uliweza kufika.
“Alinipigia simu, anatumia muda wake akiwa huko, huku akisaidia katika eneo la Odessa, kwa kutoa ukaribu sana”. Ndivyo Papa Francisko alisimulia maelezo ya mazungumzo yake na Kardinali Krajewski, ambaye alimweleza kile anachokiona siku hizi. Akiendelea Papa alisema: “Alinisimulia kuhusu uchungu wa watu hawa, vitendo vya kishenzi, uharibifu, maiti zilizoteswa ambazo wanazipata”. Ni katika eneno la Izyum ambalo Papa alidokeza, mahali ambapo mabaki ya watu wapatao 500 yalipatikana katika Kaburi la Halaiki na ambapo Kadinali Krajewski alishuhudia ugunduzi wa maiti kadhaa za Waukraine waliopigwa na kuawa na alipigwa butwaa na hofu nyingi.