Mtakatifu Papa Pio V, aliyejulikana kwa wakati ule kama Antonio Michele Ghislieri, alizaliwa tarehe 27 Januari 1504, huko Bosco Marengo, Alessandria, Kaskazini mwa Italia. Mtakatifu Papa Pio V, aliyejulikana kwa wakati ule kama Antonio Michele Ghislieri, alizaliwa tarehe 27 Januari 1504, huko Bosco Marengo, Alessandria, Kaskazini mwa Italia. 

Papa Francisko Jumuiya ya Kikristo Inasimikwa Katika Ubatizo na Kipaimara: Ushuhuda wa Imani

Ni kwa njia ya Liturujia waamini wanashiriki ule Ukuhani wa wabatizwa wote na kukamilisha ndani mwao, kile kinacho pungua katika mateso ya Kristo Yesu. Kwa njia ya Liturujia ya Kanisa, waamini wanapata neema ya kubeba ndani mwao Misalaba ya maisha, tayari kumfuasa Kristo Yesu. Baada ya kushiriki karamu ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, wanatumwa kuinjilisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Papa Pio V, aliyejulikana kwa wakati ule kama Antonio Michele Ghislieri, alizaliwa tarehe 27 Januari 1504, huko Bosco Marengo, Alessandria, Kaskazini mwa Italia.  Mwaka 1528 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Akateuliwa na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 14 Septemba 1556, huku akiongozwa na kauli mbiu ya Kiaskofu “Utinam dirigantur viae meae ad custodiendas iustificationes tuas” yaani kwa “Kiswahili cha chapuchapu” ni "Njia zangu zielekezwe ili kuitunza haki yako.” Tarehe 15 Machi 1557 akateuliwa na hatimaye kusimikwa kama Kardinali na Papa Paulo IV. Akachaguliwa kuwa Papa tarehe 7 Januari 1566 na Mei Mosi, 1572 akaitupa mkono dunia, huku akiwa na umri wa miaka 68. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Papa Pio V alikuwa ni Papa wa 225 katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, utume ambao aliufanya kwa takribani miaka sita. Ndiyo maana Mwaka 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 450 tangu alipofariki dunia. Anakumbukwa na Kanisa kwa mafundisho na ushuhuda wake wa maisha, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani tendaji; kwa kujikita katika mwelekeo sahihi wa maisha, ukarimu na uwezo wa kuzaa matunda ya toba na wongofu wa ndani. Alisimama kidete kutafuta na hatimaye, kuutangaza ukweli, ambao ni Kristo Yesu. Hii ni njia ya mfuasi mmisionari inayorutubishwa na mwanga pamoja na nguvu ya Roho Mtakatifu. Alitoa kipaumbele kwa Katekesi makini, Neno la Mungu na Sala za Kanisa, ili kupokea hazina tukufu ya Neno la Mungu lililofunuliwa. Rej. Evangelii gaudium, 30. 50. 175.

Papa Pio V alikazia Katekesi Makini kwa watu wa Mungu
Papa Pio V alikazia Katekesi Makini kwa watu wa Mungu

Katika kipindi cha miaka sita ya uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alichapisha Misale ya Kiroma kwa ajili ya Ibada za Kanisa, Sala ya Kanisa, ie. “Breviari”, tafsiri mpya ya Biblia toleo la “Vulgate” pamoja na Sheria za Kanisa “Corpus Iuris Canonici.” Kama sehemu ya kumbukizi la Miaka 450 tangu Mtakatifu Papa Pio V, alipofariki dunia, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 17 Septemba 2022 amekutana na kuzungumza na watu wa Mungu kutoka katika Jimbo Katoliki la Alessandria, lililoko Kaskazini mwa Italia. Katika hotuba yake amekazia: Ukweli, Umuhimu wa Neno la Mungu na Fumbo la Ekaristi, Sala, Ushirika wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa na mang’amuzi thabiti katika maisha na utume wao, daima wakitafuta kuufahamu, kuutangaza na kuushuhudia Ukweli ambao ni Kristo Yesu. Upendo kwa Kristo Yesu, umwilishwe katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa kutambua kwamba, siri ya mafanikio haya imetunzwa katika vyombo vya udongo. Rej 2 Kor 4:7. Waamini wajibidiishe kushiriki kikamilifu katika Karamu ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, ili kukutana na Kristo Mfufuka katika maisha yao.

Mtakatifu Papa Pio V alijibidiisha katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kufanya mageuzi makubwa katika Liturujia ya Kanisa, na hatimaye, kuboreshwa zaidi na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaokaza kwa kusema kwamba, Liturujia ni kilele ambacho kazi ya Kanisa inaelekea, na papo hapo ni chemchemi zinamotoka nguvu zake zote. Maana bidii zote za kazi za kitume hukusudiwa ili wote, waliofanywa watoto wa Mungu kwa njia ya imani na ubatizo, wakusanyike pamoja, wamtukuze Mungu katika Kanisa, washiriki sadaka na kuila karamu ya Bwana. Rej. Sacrosantum concilium, 10. Ni kwa njia ya Liturujia waamini wanashiriki ule Ukuhani wa wabatizwa wote na kukamilisha ndani mwao, kile kinacho pungua katika mateso ya Kristo Yesu. Kwa njia ya Liturujia ya Kanisa, waamini wanapata neema ya kubeba ndani mwao Misalaba ya maisha, tayari kumfuasa Kristo Yesu. Baada ya kushiriki karamu ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, Jumuiya Injilishaji inajihusisha na kumwilisha imani katika matendo: kiroho na kimwili; kwa kufurahi na wale wanaofurahi, kuteseka na wale wanaoteseka, kwa kugusa Mwili wa Kristo unaoteseka katika maisha ya wengine. Rej Evangelii gaudium, 24. Mtakatifu Papa Pio V katika maisha na utume wake alikazia umuhimu wa waamini kusali Rozari Takatifu sanjari na kujenga utamaduni wa kusali kama msingi wa shughuli zote za kimisionari.

Papa Pio V alikazia Liturujia, Sala na Rozari Takatifu
Papa Pio V alikazia Liturujia, Sala na Rozari Takatifu

Baba Mtakatifu Francisko anasema kumbe, kuna haja kwa waamini kutekeleza kwa vitendo Mafundisho ya Mitume na ya Kanisa, kwa kujenga na kudumisha ushirika, amani, upendo na mshikamano katika Neno, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma katika ujumla wake, kama ushuhuda wa umoja wa shughuli za kichungaji. Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee kabisa wongofu wa kichungaji na kimisionari ili kuwashirikisha watu wengi zaidi katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, waamini wote wanaitwa na kutumwa na kwamba, umisionari ni changamoto ya daima, ili kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kujenga ushirika thabiti wa watu wa Mungu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 17 Septemba 2022 alikutana pia na wanafunzi wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Kipaimara kutoka Jimbo Katoliki la Spoleto-Norcia, lililoko nchini Italia, amesema, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanatajirishwa kwa mapaji ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuieneza na kuitetea imani kwa maneno na matendo kama mashuhuda wa kweli wa Kristo kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Kristo Yesu, Maria Madgalena, Martha na Maria ndugu zake Lazaro. Waamini wanaweza hata wao kuongeza majina yao kweye orodha hii. Maisha ya Kikristo yanajengwa na kusimikwa juu ya msingi wa Sakramenti ya Ubatizo.

Liturujia ni chanzo na kilele cha maisha ya Kanisa
Liturujia ni chanzo na kilele cha maisha ya Kanisa

Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, Mkristo anapakwa Krisma ambayo inabubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe, yule ambaye Mwenyezi Mungu alimtia Mafuta kwa Roho Mtakatifu. Kumbe, Sakramenti ya Kipaimara inadokeza kwamba, inathibitisha Ubatizo na kuimarisha neema ya Ubatizo. Kwa mpako wa Krisma iliyochanganywa na manukato, na kuwekwa wakfu na Askofu mahalia, waamini wanampokea Roho Mtakatifu na hivyo kufafana na Kristo aliyetiwa Mafuta na Roho Mtakatifu. Hapa mwamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo anazaliwa katika maisha ya Kimungu na hivyo anapaswa kuishi na kutenda kama mwana mpendwa wa Mungu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni. Bila nguvu ya Roho Mtakatifu hakuna kinachoweza kufanyika, kama ilivyokuwa hata kwa maisha na utume wa Yesu na ndivyo ilivyo hata kwa maisha na utume wa Kanisa. Wafuasi wa Kristo hata leo hii wako chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni kiunganishi cha mapendo kati ya Baba na Mwana. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, waamini ambao ni viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, wanampokea Roho Mtakatifu kadiri ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Hizi ni zawadi na karama za Roho Mtakatifu zinazowawezesha kulijenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa tayari kutoka kimasomaso ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa hotuba yake anawaalika waamini kutunza kumbukumbu zao za Siku ya Ubatizo kwani huo ni mwanzo wa mchakato wa ujenzi wa urafiki na Mwenyezi Mungu sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Waamini wajenge maisha yao juu ya mwamba thabiti ambao ni Kristo Yesu. Huu ni mwamba pia kwa ajili ya familia na medani mbalimbali za maisha.

Papa Ubatizo na Kipaimara
19 September 2022, 15:51