Papa Francisko Amemtumia Salam za Rambirambi Irina Mikhail Gobarciov: Kiongozi wa Mabadiliko
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Rais mstaafu Mikhail Gorbaciov wa Urussi aliyefariki dunia Jumanne tarehe 30 Agosti 2022, akiwa na umri wa miaka 91 baada ya kuugua kwa muda mrefu anazikwa kwa heshima zote za kitaifa Jumamosi tarehe 3 Septemba 2022. Rais Vladimir Putin wa Urussi, Alhamisi tarehe 1 Septemba 2022 ametoa heshima zake za mwisho kwa Rais mstaafu Mikhail Gorbaciov wa Urussi. Waombolezaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameendelea kutuma salam zao za rambirambi. Rais mstaafu Mikhail Gorbaciov wa Urussi anazikwa pembeni mwa mke wake Raissa.
Ni katika muktadha wa kifo cha Rais mstaafu Mikhail Gorbaciov wa Urussi, Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambirambi Irina Mikhail Gorbaciov, Mtoto wa Rais Mstaafu Gorbaciov na kumwomba amfikishie salam zake za rambirambi kwa ndugu, jamaa, marafiki pamoja na watu wote wa Mungu nchini Urussi, walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito. Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Mungu kwa kumwezesha Rais mstaafu Mikhail Gorbaciov wa Urussi, kuwa na mwono mpana, pamoja na kujizatiti kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu; akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Urussi. Alikuwa ni chombo na shuhuda wa mageuzi makubwa sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anamwombea ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumjalia amani, maisha na uzima wa milele, Apumzike kwa Amani.