Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani Kwa Mwaka 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesisitiza haja ya kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi ili kupunguza tishio la silaha za nyuklia baada ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kushindwa kufikia maafikiano katika mkutano wa kuupitia Mkataba wa kihistoria wa kuzuia kusambaa kwa silaha za nyuklia (NPT). Mkutano wa kumi wa mapitio ya nchi wanachama NPT ulihitimishwa hivi karibuni bila ya kufikia muafaka kwa sababu Urusi ilipinga kutuma ujumbe kuhusu udhibiti wake kwenye vituo vya nyuklia vilivyoko nchini Ukraine. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea kusikitishwa kwake kwamba nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hazikuweza kufikia makubaliano juu ya "matokeo muhimu", na kutumia fursa ya kuimarisha mkataba huo uliodumu kwa miaka 52 na hatimaye kuendeleza malengo yake na kwamba, kwa sasa hatari hii inazidi kuongezeka maradufu na hivyo kutishia, amani, usalama na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anaendelea kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kutumia kila njia ya majadiliano na diplomasia ili kupunguza mivutano, hatari ya nyuklia na kuondoa tishio la nyuklia mara moja na kwa wote! Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza cha kutokomeza silaha za kinyuklia duniani.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani kwa mwaka 2022 anatamka kwa mara nyingine tena kwamba, matumizi ya nguvu za atomic kwa ajili ya vita, kwa wakati huu, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu ni kwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu na tishio kubwa kwa mustakabli wa mazingira nyumba ya wote. #Peace #NuclearDisarmament #TimeofCreation. Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Septemba inaadhimisha Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani, changamoto iliyovaliwa njuga na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1946 kwa kuanzisha Tume ya Nguvu ya Atomic, iliyofutwa kunako mwaka 1952 na hatimaye kukaanzishwa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic, IAEA. Umoja wa Mataifa umeendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa kutokomeza silaha za nyuklia duniani. Hadi leo hii, kuna silaha 14,000 za nyuklia sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, majadiliano kuhusu kutokomeza silaha za nyuklia bado yanaendelea.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kama sehemu ya maadhimisho ya Siku hii kwa mwaka 2021 alisikitika kusema kwamba, mashindano ya silaha, zikiwemo silaha za nyuklia yanaendelea kukomba rasilimali za dunia ambazo zingeweza kutumika vyema zaidi kwa ajili ya kunogesha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Kunako mwaka 1996 Jumuiya ya Kimataifa ilipitisha azimio la kuacha mchakato wa utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia kwani zina madhara makubwa kwa binadamu. Hii ni siku ambayo imeanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuendelea kuragibisha umuhimu wa kutokomeza silaha za nyuklia kama kipaumbele cha Umoja wa Mataifa. Ni muda muafaka wa kuelimisha jamii umuhimu wa kutokomeza silaha hizi na faida zake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni siku muafaka kwa Jumuiya ya Kimataifa kuzungumzia changamoto hii, ili kutafuta na kudumisha misingi ya amani na usalama duniani kwa kuondokana na silaha za nyuklia. Bwana António Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia kwa Mwaka 2021 alisema huu ni wakati wa kuondoa silaha za nyuklia kutoka kwenye ulimwengu huu, na kuanzisha enzi mpya ya majadiliano, uaminifu na amani.
Changamoto ya silaha za kinyuklia imekuwa ni msingi wa shughuli za Umoja wa Mataifa tangu kuanzishwa kwake na azimio la kwanza la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1946 lilikuwa ni kuondolewa kwa silaha zote za atomiki na zile zinazoweza kusababisha maafa makubwa duniani kote! Silaha za nyuklia zimeendelea kupungua kila mwaka, lakini bado kuna silaha 14, 000 sehemu mbalimbali za dunia. Kuna nchi ambazo zinaendelea kuimarisha vituo vya silaha za nyuklia sanjari na mashindano ya silaha za nyuklia, jambo ambalo ni hatari sana na wala halikubaliki na Jumuiya ya Kimataifa. Hivi karibuni, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa nchi zote zinazoshikilia teknolojia ya nyuklia kutia saini mkataba wa kina wa kupiga marufuku matumizi ya nyuklia (CTBT), ambao ulipitishwa mwaka 1996, na kutiwa saini na nchi 185. Ili Mkataba wa CTBT uanze kutumika, lazima utiwe saini na kuridhiwa na nchi 44 zilizo na teknolojia ya nyuklia, ambazo nane bado hazijaridhia mkataba huo nazo ni: China, Misri, India, Iran, Israel, Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea, Pakistan na Marekan. Kumbe, uamuzi wa Urusi na Marekani kuongeza muda mpya wa kuanza mkakati wa kupunguza silaha na kushiriki mazungumzo kuwa kama ishara ya matumaini. Mkataba huu umeanza kutumika rasmi tangu mwezi Januari 2021, hatua muhimu sana inayopaswa kupongezwa na wapenda amani duniani. Umoja wa Mataifa unasema, huu ni wakati wa ujenzi wa enzi mpya inayojikita katika majadiliano, uaminifu na amani kwa watu wote duniani!
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu, Jumapili, tarehe 24 Novemba 2019 alizungumzia kuhusu mateso na maafa makubwa yaliyosababishwa na mashambulizi ya mabomu ya atomiki, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya: usalama, amani na utulivu kwa kuondokana na wasi wasi pamoja na hofu inayotawala akilini na nyoyoni mwa watu kiasi cha kushindwa kuaminiana, na hivyo, kudhohofisha mafungamano ya watu wa Mataifa pamoja na mchakato wa majadiliano. Amani na utulivu wa kimataifa vinaweza kujengeka katika msingi wa mshikamano na ushirikiano wa haki kwa ajili ya huduma kwa kutambua kwamba, watu wanategemeana na kukamilisha; na wanapaswa kuwajibika kama wamoja kwa ajili ya ustawi wa familia nzima ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, Nagasaki ni mji ambao umeshuhudia maafa makubwa kwa binadamu sanjari na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; kielelezo cha mashindano ya utengenezaji wa silaha za maangamizi; upotevu mkubwa wa rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kuchochea maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Rasilimali fedha inayotumika kwa ajili ya kutengeneza, kuboresha na kuhifadhi na hatimaye, kuuza silaha za maangamizi, nyuma yake kuna kilio cha watoto na familia nyingi duniani. Watu wanatamani amani ya kudumu ili kuondokana na vitisho vya silaha za maangamizi na kwamba, hii ni changamoto inayowahusisha watu wote; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuaminiana na wala si katika tabia ya kupimana nguvu. Kuna haja ya kudhibiti biashara ya silaha kimataifa na maendeleo makubwa ya teknolojia kuhusu masuala ya kijeshi. Hii ni dharura inayohitaji kushughulikiwa na viongozi wote wa Jumuiya ya Kimataifa.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuhimiza umuhimu wa watu wa Mataifa kudumisha amani. Kanisa linaunga mkono Kanuni ya Sheria ya Kimataifa kuhusu Silaha za Nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu! Baba Mtakatifu anasema, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumza “dhana ya silaha za nyuklia”. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika kubuni sera na mikakati itakayosaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.
Kunako mwaka 1964, Mtakatifu Paulo VI alishauri kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo kwa Nchi Maskini, ambao ungechangiwa kwa kuchukua sehemu ya bajeti ya serikali mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya kijeshi. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutengeneza mazingira ya kuaminiana, kwa sababu hii ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa majadiliano; toba na wongofu wa ndani, ili utamaduni wa uhai, upatanisho na udugu viweze kutawala katika akili na nyoyo za watu. Baba Mtakatifu Francisko baada ya hotuba yake, aliwaomba waamini wa dini mbalimbali duniani kuungana pamoja naye kwa ajili ya kusali ile sala ya Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya kuombea amani duniani: Ee Bwana unifanye kuwa chombo cha amani. Palipo chuki nieneze upendo. Palipo na mashaka pawe na imani. Palipo na tumaini pawe na matumaini. Palipo na giza pawe na mwanga. Palipo na huzuni pawe na furaha. Ee Bwana Mungu unijalie; Nisitafute kufarijiwa bali kufariji Nisitafute kupendwa bali kupenda. Kwani ni katika kutoa ndipo tunapopokea Ni kwa kusamehe ndipo tunaposamehewa. Na ni kwa kufa ndipo tunazaliwa katika uzima wa milele, AMINA. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuongoka na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwageuza kuwa ni vyombo vya amani na hivyo kutorudia tena kwenye makosa ya zamani.