Tafuta

Kumbukumbu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Maprofesa na Wahadhiri wa Liturujia Nchini Italia. Kumbukumbu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Maprofesa na Wahadhiri wa Liturujia Nchini Italia. 

Umuhimu wa Liturujia Katika Maisha na Utume wa Kanisa: Ushiriki wa watu wa Mungu

Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu mageuzi makubwa yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Liturujia ya Kanisa; Ufahamu wa imani ya watu wa Mungu, Liturujia ni chemchemi ya furaha, Waraka wa Kitume wa “Desiderio Desideravi”: Kuhusu Majiundo ya Kiliturujia ya Watu wa Mungu pamoja na Mapokeo ya Kanisa. Liturujia ni chemchemi ya furaha na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Maprofesa na Wahadhiri wa Liturujia Nchini Italia “Associazione dei Professori e Cultori di Liturgia” ni matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kinachopania pamoja na mambo mengine: kukuza, kusasisha na kufundisha Liturujia ya Kanisa katika vitivo vya Taalimungu na Seminari, Nyumba za Malezi ya Watawa kwa kutambua kwamba, hili ni somo la lazima sana katika malezi na majiundo ya Kikasisi. Hili ni somo linalopaswa kufundishwa kadiri ya mwono wa: Kitaalimungu, kihistoria, maisha ya kiroho, kichungaji na kisheria. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Fumbo la Kristo Yesu na historia ya wokovu vina uhusiano na mafungamano ya pekee na Liturujia. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanahimiza malezi ya Kiliturujia na ushiriki hai wa waamini katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa kuzingatia marekebisho ya Liturujia Takatifu. Rej. SC, 16. Sanjari na kuendeleza malezi na majiundo endelevu kwa Wakleri nchini Italia katika uwanja wa Liturujia ya Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa kwa kusema kwamba, maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu.” Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waoneshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli.

Chama cha Maprofesa wa Liturujia Italia kinaadhimisha miaka 50 ya utume.
Chama cha Maprofesa wa Liturujia Italia kinaadhimisha miaka 50 ya utume.

Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana lakini lenye mambo yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kuhiji. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao tunakoelekea. Hivyo Liturujia kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe hekalu takatifu la Bwana, makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo.  Wakati huohuo kwa namna ya ajabu Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumhubiri na kumshuhudia Kristo Yesu; na kwa njia hiyo inawaonesha wale walio nje [nalo,] Kanisa lililo ishara iliyoinuliwa juu kati ya mataifa, ambayo chini yake watoto wa Mungu waliotawanyika wakusanyika katika umoja mpaka liwepo zizi moja chini ya mchungaji mmoja. Rej. SC, 2.

Ni Katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Maprofesa na Wahadhiri wa Liturujia Nchini Italia “Associazione dei Professori e Cultori di Liturgia”, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 1 Septemba 2022 amekutana na kuzungumza na wanachama hawa. Amegusia kuhusu mageuzi makubwa yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Liturujia ya Kanisa; Ufahamu wa imani ya watu wa Mungu, Liturujia ni chemchemi ya furaha, Waraka wa Kitume wa “Desiderio Desideravi”: Kuhusu Majiundo ya Kiliturujia ya Watu wa Mungu pamoja na Mapokeo ya Kanisa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Chama hiki kwa mchango wao katika tafakari kuhusu Liturujia ya Kanisa kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita na kwamba, wao ni matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mabadiliko haya yamepitia vipindi mbalimbali kama vile: Machapisho ya vitabu vipya vya Liturujia pamoja na kukusanya nyaraka mbalimbali za Kanisa kuhusu Liturujia, utume unaoendelea hadi wakati huu. Hii ni dhamana inayohitaji muda na utunzaji makini, shauku na subira; unahitaji akili ya kiroho na akili ya kichungaji; unahitaji malezi, hekima na busara, ili kuendelea kunogesha maboresho katika Liturujia ya Kanisa.

Umoja na ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu ni muhimu katika liturujia
Umoja na ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu ni muhimu katika liturujia

Baba Mtakatifu anasema, utume huu, hauna budi kuendelea kujikita katika tafiri makini, majadiliano ya kina katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, hata taalimungu na sayansi za kibinadamu zinaweza kuwa na mchango makini katika utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kutengeneza mtandao wa taasisi zitakazosaidia mchakato wa maboresho ya Liturujia ya Kanisa ndani na nje ya Italia. Ni katika muktadha huu kwamba, wanapaswa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini Jumuiya za Kikristo, ili utume wao uweze kuzima kiu ya matamanio halali ya watu wa Mungu. Hawa ni watu wanaopaswa kuendelea kuundwa, kukua na kukomaa kwani wao pia wana “utambuzi wa imani” “Sensum fidei” unaowawezesha kung’amua yale yanayotoka na kuwaelekeza kwa Mwenyezi Mungu hata katika masuala ya Liturujia. Ikumbukwe kwamba, Liturujia ni kazi ya Kristo Yesu na Kanisa lake, chemchemi ya furaha, sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu na kamwe, watu wasigeuze Liturujia ya Kanisa kuwa kama msiba. Liturujia ni kito cha thamani sana katika maisha na utume wa Kanisa. Inapaswa kutunzwa, kuendelezwa na kupaliliwa, kwa kuunganisha: taalimungu, shughuli za kichungaji, imani na maisha ya waamini.

Ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika liturujia ni muhimu.
Ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika liturujia ni muhimu.

Mama Kanisa anahitaji kuona Liturujia ambayo itawawezesha waamini kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani; Liturujia inayogusa mahitaji ya watu wa Mungu; kwa kutambua fika maana halisi ya Taalimungu na Tasaufi ya Liturujia. Majiundo ya Kiliturujia ni shughuli pevu katika maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, kuna haja ya kuunganisha upembezi yakinifu sanjari na kuendeleza mwingiliano wa masomo mbalimbali huku wakiwa na mwono wa kielimu. Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa hayana budi kuwa na mwendelezo wa Mapokeo ya Kanisa kwa kujikita katika mizizi yake na kamwe Liturujia isiadhimishwe kwa mazoea. Liturujia lazina iwe hai katika maisha na utume wa Kanisa. Mwishoni Baba Mtakatifu anakitaka Chama cha Maprofesa na Wahadhiri wa Liturujia Nchini Italia “Associazione dei Professori e Cultori di Liturgia” kujikita katika sala, manga’muzi na maisha ya Kanisa. Hii ni taalimungu inayoandikwa kwa akili na kusali. Lakini hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa katika masomo yote, ili kuwasaidia waamini kugundua uzuri na utakatifu wa Fumbo la Maisha ya Mungu, anayejitoa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu.

Liturujia ya Kanisa
02 September 2022, 16:47