Tafuta

Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948. Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948.  

Vipaumbele vya Diplomasia ya Vatican Katika Medani za Kimataifa

Uhuru wa kidini, utu, heshima ya binadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Vatican katika medani mbalimbali za Kimataifa. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, inatoa kipaumbele cha pekee kwa: Uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Vatican katika medani mbalimbali za Kimataifa. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu. Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbalimbali za maisha. Haki inakwenda sanjari na wajibu! Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, kichocheo muhimu sana cha amani, utulivu na maridhiano miongoni mwa binadamu.

Diplimasia ya Vatican: Utu, heshima na haki msingi za Binadamu.
Diplimasia ya Vatican: Utu, heshima na haki msingi za Binadamu.

Kanisa linapenda kusimama kidete: kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya tunu msingi za Kiinjili! Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948. Mwamini anapaswa kukiri na kushuhudia imani yake inayomwilishwa katika matendo. Uhuru wa kidini ni kati ya mambo ambayo hayapewi tena kipaumbele cha pekee katika vyombo vya utekelezaji wa sheria na hata wakati mwingine kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kuna haja ya kuwajulisha walimwengu kwamba, kuna nyanyaso na dhuluma za kidini zinazoendelea kutendeka sehemu mbalimbali za dunia, kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu. Kumbe, Kanisa, Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake wa karibu wanapozungumzia masuala ya vita sehemu mbalimbali za dunia wanaongozwa na kusimamiwa na kanuni, sheria na taratibu zilizotajwa hapo juu. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kukoleza misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mungu.

Madhara ya vita ni makubwa sana katika maisha ya mwanadamu
Madhara ya vita ni makubwa sana katika maisha ya mwanadamu

Tangu Urussi ilipoivamia Ukraine, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa karibu wamekuwa wakitoa hotuba za kulaani vita; wameonesha madhara yake na kutoa mwaliko wa kusitisha vita na kuanza kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hakuna vita ya haki na kamwe vita haiwezi kukubalika kama suluhu ya matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Vita ni kitendo cha kikatili sana ni dhuluma dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Diplomasia ya Vatican katika vita na migogoro mbalimbali, daima inapania kulinda maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu na kamwe haina mafungamano ya kisiasa na nchi yoyote yote. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu alisikitishwa na mauaji ya msichana mmoja huko nchini Urussi, kitendo ambacho kilichochea maneno makali kutoka kwa taasisi na viongozi wa kisiasa nchini Ukraine dhidi ya Baba Mtakatifu. Lakini, ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu anatetea uhai, utu, heshima ya wote na wala hafungamani na upande wowote. Msimamo wa Baba Mtakatifu kuhusu vita kati ya Urussi na Ukraine, uko pale pale na wala haujabadilika. Vita hii ni kinyume cha maadili, ni jambo lisilokubalika, ni ukatili na unyama na kufuru kwa utakatifu wa maisha ya mwanadamu!

Diplomasia Vatican
10 September 2022, 16:00