Huduma Kwa Vijana Wanaoishi Katika Mazingira Magumu na Hatarishi: Utu, Malezi na Michezo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Dhamira ya Jumuiya ya Mstari wa Mbele “Comunità Frontiera" ni kusaidia malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya ili wasitumbukizwe kwenye vitendo vinavyokwenda kinyume cha maadili na utu wema na hasa katika matukio ya uhalifu. Hii ni Jumuiya ambayo imekita mizizi yake Kusini mwa Italia, kwa kuwahudumia watoto zaidi ya 100, imekwisha kujenga makazi kwa ajili ya vijana maarufu kama “Città dei Ragazzi” ili kutoa fursa kwa watoto na vijana kushiriki michezo mbalimbali na kwamba, Kituo hiki kinatambuliwa rasmi na Wizara ya Mambo ya Ndani kama mradi wa majaribio katika mchakato wa kuzuia ukosefu wa maadili na uhalifu miongoni mwa watoto na vijana wa kizazi kipya. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Mstari wa Mbele “Comunità Frontiera" inayounganisha karama ya Mtakatifu Francisko wa Assisi inayojikita katika huduma kwa: maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Pili ni karama ya Mwenyeheri Giuseppe Puglisi, aliyesadaka maisha kama ushuhuda wa upendo kwa watu na hasa zaidi watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Viongozi hawa wawili wa Kanisa ni watu waliojisadaka bila ya kujibakiza, kama kielelezo cha ushuhuda wa maisha yao yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo Yesu katika Fumbo la Umwilisho, alijinyenyekesha na hivyo kuamua kukutana na binadamu, aliyekengeuka na kutopea katika dhambi, ili aweze kumkirimia tena Injili ya matumaini.
Mtakatifu Francisko wa Assisi alijivua kabisa na mali, utajiri na malimwengu, akajisadaka na kujiaminisha katika ulinzi na maongozi ya Mungu katika maisha yake; akajinyenyekesha na kuwa mdogo, ili kuwaonjesha maskini, wagonjwa na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii: huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao tayari kuwaganga kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Mwenyeheri Giuseppe Puglisi, alisadaka maisha na utume wake kwa ajili ya vijana na watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Akawachukua, akawalea na kuwaelimisha, kujisadaka kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani zao na kamwe si kuwa mateka wa Kikundi cha Mafia. Baba Mtakatifu anasema, leo hii kuna mashuhuda ambao wameonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, wamebadilika na kamwe hawezi kurudi tena nyuma na kuwa ni mateka wa Kikundi cha Mafia. Karama zote hizi zinaunganishwa na uzi wa dhahabu ambao ni upendo unaoshinda uovu na hivyo kuwa ni chemchemi ya maisha mapya. Huu ni upendo unaosimikwa katika ukarimu, utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kusaidia malezi na makuzi ya watoto na vijana wa kizazi kipya.
Karama ya Mtakatifu Francisko wa Assisi na Mwenyeheri Giuseppe Puglisi zinakamilishwa na karama ya Mtakatifu Don Bosco, yaani karama ya Wasalesiani wanaojisadaka kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto na vijana wa kizazi kipya, ili kuwasaidia wawe “wakristo wema na watakatifu pamoja na kuwa ni raia waaminifu. Katika malezi na makuzi ya watoto na vijana, karama hizi tatu zinapaswa kupewa msukumo wa pekee amekaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu awe ni chemchemi ya matumaini kwa wale waliopondeka na kuvunjika moyo, chachu ya maisha mapya ya Jumuiya ya Mstari wa Mbele “Comunità Frontiera.” Ni mwaliko kwa wanajumuiya kuwa ni mashuhuda wa Injili ya mwanga, ili wale wote wanaotembea gizani waweze kuiona nuru ya Mataifa ambayo ni Kristo Yesu, tayari kuzaliwa katika upya wa maisha. Kumbe, mambo makuu ya kuzingatia katika huduma kwa watoto na vijana ni: Ukaribu wa Mungu; Huruma na Upendo.