Tafuta

Papa Francisko: Maadhimisho ya Sinodi XVI ya Maaskofu 1-29 Oktoba 2023! Awamu ya Pili Oktoba 2024 Papa Francisko: Maadhimisho ya Sinodi XVI ya Maaskofu 1-29 Oktoba 2023! Awamu ya Pili Oktoba 2024 

PAPA: Maadhimisho Ya Sinodi XVI: 1-29 Oktoba 2023 & Oktoba 2024

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI yamegawanywa sasa katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili ni Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi kama chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 16 Oktoba 2022 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ametangaza mabadiliko makubwa ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu sanjari na kuendelea kujizatiti zaidi katika utamaduni wa kusikiliza na kufanya mang’amuzi ya pamoja. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamegawanywa sasa katika awamu kuu mbili.

Awamu ya kwanza ni tarehe 1-29 Oktoba 2023.
Awamu ya kwanza ni tarehe 1-29 Oktoba 2023.

Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa watu wa Mungu katika ujumla wao kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Maadhimisho ya Sinodi ni wakati muafaka wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, ili hatimaye, kuhamasisha umoja na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka katika ngazi mbalimbali za maisha, kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau. Wafuasi hawa baada ya kukutana, kuzungumza na kutembea na Yesu Kristo Mfufuka, walirejea wakiwa wamesheheni furaha, imani na matumaini kedekede, tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka aliyewafufua kutoka katika makaburi yao ya kutoamini na kujikatia tamaa. Kwa kukutana na Kristo Mfufuka wakapata nafasi ya kufafanuliwa utimilifu wa Maandiko Matakatifu, Sheria na Unabii na hatimaye, kufahamu kwa kina maana ya Kashfa ya Fumbo la Msalaba.

Awamu ya Pili ni Mwezi Oktoba 2024: Kusikiliza na Mang'amuzi ya pamoja.
Awamu ya Pili ni Mwezi Oktoba 2024: Kusikiliza na Mang'amuzi ya pamoja.

Kwa mang’amuzi ya Fumbo la Msalaba wakaweza kufikia ukweli wa Ufufuko kiini cha matumaini mapya. Watu wa Mungu wanaitwa kusali na kuiombea Sinodi ya Maaskofu. Huu ndio mwelekeo mpya wa wainjilishaji waliojazwa na Roho Mtakatifu, ambao wako tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuinjilisha kwa ushupavu! Rej. EG 259. Baba Mtakatifu Francisko anasema, dhana ya Sinodi kama asili, mtindo wa maisha na utume wake inapata chimbuko lake kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume na maana yake ni kutembea kwa pamoja. Hii ni historia ya Kanisa kuanzia Yerusalemu na hatima yake ni mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 10 Oktoba 2021 akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alizindua rasmi maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Awamu ya kwanza ilikuwa ni kwa ajili ya Makanisa mahalia pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki nayo yalianza tarehe 10 Mwezi Oktoba 2021 hadi tarehe 15 Agosti 2022.

Ushiriki mkamilifu wa watoto wa Kanisa katika maisha na utume wa Kanisa
Ushiriki mkamilifu wa watoto wa Kanisa katika maisha na utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu katika ngazi ya kijimbo ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha utambuzi wa imani “Sensum fidei” unaofumbatwa katika unyenyekevu. Ni mwaliko kwa viongozi wa Kanisa kushikamana na waamini, ili hatimaye, kuwatia shime ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba, jukumu la kinabii na ushuhuda wa Kikristo si tu kwa ajili ya viongozi wa Kanisa lakini pia waamini walei wanapaswa kushirikishwa kikamilifu. Huu ni ushiriki wa mtu binafsi na ushiriki wa Kanisa mambo ambayo yanategemeana na kukamilishana. Utambuzi wa imani “Sensum fidei” ni mchakato unaowahusisha watu wote wa Mungu, wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na watu wasiokuwa na matumaini, hawa ndio waliotumia na Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Kristo Yesu. Utambuzi wa imani “Sensum fidei” ni matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya kukoleza majadiliano kwa ajili ya wokovu! Baba Mtakatifu anawataka waamini kuendelea kujiaminisha kwa Mungu ili awaoneshe miujiza kwa kuisikiliza sauti yake. Ni muda muafaka wa kutubu na kumwongokea Mungu ili kuachana na mielekeo ya maisha ambayo ni tenge mbele ya Mwenyezi Mungu.

Sinodi: Ushiriki na uimarishaji wa urika wa Maaskofu na ushiriki wa walei.
Sinodi: Ushiriki na uimarishaji wa urika wa Maaskofu na ushiriki wa walei.

Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu ni kuanzia Mwezi Septemba 2022 hadi Machi 2023. Mapendekezo kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yanaendelea kukusanywa na Sekretarieti Kuu ya Sinodi ya Maaskofu na hatimaye itachapisha na kwa mara ya kwanza Hati ya Kutendea Kazi “Instrumentum Laboris." Na katika hatua hii, kutakuwepo pia Mratibu wa Sinodi atakayekuwa anawasiliana na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Sifa za waamini walei na Maaskofu watakaoshiriki kwenye maadhimisho ya Awamu ya Tatu, zitabainishwa. Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu yatawasilisha Nyaraka zao, muswada utakaotumika kuandika sasa Hati ya Kutendea Kazi “Instrumentum Laboris.” Maadhimisho ya Awamu ya Tatu na ya mwisho chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na katika muktadha huu itaadhimishwa kuanzia tarehe 4-29 Oktoba 2023 na awamu ya pili itakuwa ni Mwezi Oktoba 2024. Baba Mtakatifu anawataka waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, kwa kusikilizana, kutembea kwa pamoja kati yao kama watoto wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Katika kipindi hiki cha janga kubwa la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Mama Kanisa anahamasishwa kuwa ni Sakramenti ya Uponyaji. Dunia imepaaza kilio chake, imeonesha udhaifu wake sasa inataka kutibiwa na kugangwa.

Papa Sinodi 2021-2024
17 October 2022, 16:53