Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia ulitiwa saini kwa mara ya kwanza tarehe 22 Septemba 2018., ukapyaishwa 2020 na 2022. Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia ulitiwa saini kwa mara ya kwanza tarehe 22 Septemba 2018., ukapyaishwa 2020 na 2022. 

Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi Kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu 2022

Papa anapenda kuonesha uvumilivu unaosimikwa katika matumaini, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linaipatia Jumuiya ya Waamini Wakatoliki nchini China wachungaji bora na waaminifu. Lengo ni kuendeleza maisha na utume wa Kanisa. Pili ni kuwapata wachungaji wema, bora na waaminifu watakaotekeleza utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiongozwa na ukarimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia ulitiwa saini kwa mara ya kwanza tarehe 22 Septemba 2018. Kwa kutambua umuhimu wake, ukapyaisha tena tarehe 22 Oktoba 2020 na hatimaye, Oktoba 2022 Mkataba umeongezwa tena kwa muda wa miaka miwili. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha uvumilivu unaosimikwa katika matumaini, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linaipatia Jumuiya ya Waamini Wakatoliki nchini China wachungaji bora na waaminifu watakaotekeleza vyema utume wao. Lengo la Vatican ni kuendeleza maisha na utume wa Kanisa Katoliki, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini China. Pili ni kuwapata wachungaji wema, bora na waaminifu watakaotekeleza dhamana na utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiongozwa na ukarimu katika huduma kwa watu wa Mungu, katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kanisa liko makini sana katika maisha, historia na maendeleo ya Kanisa nchini China.

Huu ni mchakato wa majadiliano ya kina ulioasisiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ukaendelezwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Papa Francisko anaendelea kushuhudia matunda ya juhudi hizi katika ukweli na uwazi na kwamba, leo hii, Wakatoliki nchini China wanajitahidi kuuishi Ukristo wao kwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili; kwa kupata katekesi na mafundisho msingi ya Kanisa, huku wakiendelea kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa kwa furaha, imani na matumaini, kielelezo makini cha imani inayomwilishwa katika upendo na ukarimu kwa watu wa Mungu nchini China. Hii ni hatua kubwa ya ushirikiano na mshikamano kati ya Vatican, Serikali kuu ya China, Maaskofu mahalia na waamini wao pamoja na viongozi mahalia.

Majadiliano kati ya Vatican na Serikali kuu yanasimikwa katika uvumilivu
Majadiliano kati ya Vatican na Serikali kuu yanasimikwa katika uvumilivu

Kipaumbele cha pekee ni kuhusu shughuli za kichungaji na kitume, ili kuwawezesha waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchakato huu pamoja na mambo mengine unapania kukoleza: imani na matumaini; umoja na mshikamano wa kidugu. Uteuzi wa Maaskofu kwa ushirikiano kati ya Vatican na Serikali kuu ya China ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini China na kwamba, huo ni mwanzo wa ushirikiano mpana zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni. Serikali kuu ya China inatambua na kunathamini dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kama Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki. Huo ni mwanzo wa amani na utulivu miongoni mwa watu wa Mungu nchini China. Kumbe, Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia hauna uhusiano na masuala ya kisiasa bali unajikita zaidi katika maisha na utume wa Kanisa nchini China, kama kielelezo cha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican anasema, tangu mwaka 2018 kumekuwepo na mafanikio makubwa chini ya Mkataba huu. Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki nchini China wanateuwa na hatimaye kuwekwa wakfu kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Katika Ibada ya Misa Takatifu Mapadre wote kwa sasa wanasali ile sala ya kuombea Kanisa isemayo: Tunakuomba, Ee Bwana, sadaka hii ya kutupanisha nawe ilete amani na wokovu duniani kote. Upende kuliimarisha katika imani na mapendo Kanisa lako linalosafiri hapa duniani, pamoja na mtumishi wako Baba Mtakatifu wetu “Francisko”, na Askofu wetu… Maaskofu na watumishi wako wote pamoja na taifa lako lote. Sehemu hii ya Sala miaka kadhaa iliyopita haikusemwa. Tayari kuna Maaskofu mahalia 6 walioteuliwa na kuwekwa wakfu kwa Kanisa Katoliki nchini China na Baba Mtakatifu anao uamuzi wa mwisho. Maaskofu waliowekwa wakfu wanatambuliwa rasmi na Serikali kuu ya China na hivyo ni fursa ya kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kitaasisi na kitamaduni kwa kutambua umuhimu wa maisha na utume wa Kanisa nchini China mintarafu: Uhalali wa Sakramenti zinazoadhimisha nchini China na kwamba, waamini hawa bado ni raia wema wa China.

Mkataba ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa China
Mkataba ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa China

Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema tangu Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia ulipotiwa mkwaju hapo tarehe 22 Septemba 2018 tayari Maaskofu sita wamekwisha kuchaguliwa na mchakato bado unaendelea sanjari na upatanisho wa majimbo kadiri ya maelekezo ya kichungaji na kitume yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Kanuni msingi ni kuhakikisha kwamba wanateuliwa watu makini watakaowekwa wakfu kwa ajili ya Kanisa na China katika ujumla wake. Vatican inatambua changamoto ambazo bado zinaendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa nchini China. Vatican ina matumaini kwamba, hatua kwa hakua, mambo mengi yataweza kupata ufumbuzi wa kudumu.

Kwa upande wake Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu anakaza kusema, Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia unakazia asili ya Kanisa kama Sakramenti ya wokovu na umuhimu wa kuendeleza Mapokeo ya Kanisa kuhusu urika wa Maaskofu ambao ni waandamizi wa Mitume. Mama Kanisa anataka kuendeleza mchakato wa upatanisho unaosimikwa katika ukweli na uwazi kwa Kanisa Katoliki nchini China, kwa sababu kuna madonda mengine ni makubwa na yanahitaji faraja na uponyaji kutoka kwa Mungu mwenyewe, ili hatimaye, kuweza kuwa na ushirika mkamilifu na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hali kama hii imewahi kujitokeza katika historia na maisha ya Kanisa Katoliki nchini Ufilippin.

Kardinali Tagle: Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu
Kardinali Tagle: Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu

Jambo la msingi ni kuzingatia kanuni, taratibu na sheria za Kanisa, daima Maaskofu wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na kuendeleza mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu kati ya watu wa Mungu nchini China, ili kukuza ufahamu wa imani ya watu wa Mungu “Sensus fidei” na upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake unavyoshuhudiwa na watu wa Mungu nchini China. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema Maaskofu kwa kuwekwa wakfu wa Kisakramenti na kwa ushirika wa kihierarkia pamoja na Kichwa cha Urika na viungo vyake, wanafanywa washiriki wa Umoja huo wa Maaskofu. Urika wa Maaskofu ni urithi wa urika wa Mitume katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, huku wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu.

Mkataba wa Vatican na China
22 October 2022, 14:41