Papa Francisko Sala Ni Nguvu ya Amani: Waamini Kamwe Msichoke Kuombea Amani Ulimwenguni
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Yohane XXXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa tarehe 11 Aprili 1963 anasema, amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Professa Andrea Riccardi, akiwa kijana mbichi bado, hapo tarehe 7 Februari 1968, yaani miaka 54 iliyopita alianzisha Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma na kujikita katika mambo makuu matatu yaani: Sala, Maskini na Amani duniani. Kanisa kuu la Bikira Maria wa Trastevere yakawa ni makao makuu ya sala, maisha na utume wao sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni mchakato unaopaswa kujikita kwa namna ya pekee kabisa katika Tafakari ya Neno la Mungu na kuendelea kusoma alama za nyakati ili kukuza na kudumisha utandawazi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu na maisha ya kiroho unaofumbatwa katika mtazamo wa Uso wa huruma ya Mungu. Jumuiya hii inapaswa kuwa na ari na mwamko mpya zaidi wa Kiinjili ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa kuwa na moyo wazi kwa wote bila ubaguzi kwa kisingizio cha uadui, ili kuendeleza maisha ya binadamu hadi kufikia utimilifu wake!
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kuanzia tarehe 23 hadi 25 Oktoba 2022 inaendesha Mkutano wa Kimataifa wa Amani, Dini na Tamaduni katika Majadiliano, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kilio cha Amani.” Mkutano huu pamoja na mambo mengine unaendelea kugusia kuhusu: Dunia Mama, Sayari Moja, Binadamu wamoja; Wakimbizi na wahamiaji ni fursa adhimu kwa sasa na kwa siku za usoni: Mtu anayeokoa maisha ya mwanadamu, anaokoa ulimwengu. Sala ni msingi wa amani duniani na kwamba, vita na kinzani ni changamoto pevu kwa Bara la Ulaya. Umuhimu kwa Wakristo kusherehekea Pasaka ya Bwana, wakiwa wameungana, kama ishara ya kuunganisha ulimwengu wote. Neno la Mungu ni chemchemi ya ndoto kuu. Wajumbe wanaendelea kujadili kuhusu: dini, majadiliano na aman. Machafuko ya Kisiasa nchini Cuba tangu mwaka 1962 hadi 2022, hatari ya mashambuizi ya Silaha za Kinyuklia, kama ilivyokuwa jana, na leo. Bahari ya Mediterrania na changamoto zake na kwamba, kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwani hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe.
Kumbe, kuna umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano katika ulimwengu uliosambaratika na kumeguka na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kujifunza mengi kutoka katika uzoefu na mang’amuzi ya maambukizi makubwa ya Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Viongozi wa dini wanao wajibu na dhamana kubwa katika ulimwengu wa utandawazi, kama ambavyo pia vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii inavyoweza kujibu kikamilifu kilio cha amani katika ulimwengu mamboleo. Kumbe, huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuombe amani katika maeneo tofauti tofauti mjini Roma. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 25 Oktoba 2022 majira ya jioni, akiwa kwenye Magofu ya Colosseo mjini Roma, anashiriki pamoja na viongozi wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine. Hii ni fursa pia kwa waamini sehemu mbalimbali za mji wa Roma, kusali na kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni sala inayopania kujibu kilio cha damu. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 23 Oktoba 2022 ametumia fursa hii, kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga naye kwa ajili ya kuombea amani. Kwa sababu kilio cha amani kinachoinuka kutoka sehemu nyingi sana za ulimwengu kinaweza kuziba kelele za silaha na vita. Sala ni nguvu ya amani na kamwe waamini wasichoke kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani.